Ujauzito/mimba, kawaida hukaa ndani ya tumbo la mama
kipindi cha miezi tisa, tangu pale yai lake lililopevuka lilipoungana na mbegu
ya baba na uumbaji wa kiumbe kipya kufanyika hadi kuzaliwa.
Ki-uhalisia miezi tisa ni kipindi kirefu mno, lakini si
kwake Theresia Mushi katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG hivi karibuni ndani ya Hospitali ya Taifa
Muhimbili {MNH}, anasimulia magumu aliyoyapitia kipindi cha mwezi mmoja
alicholazwa wodini akiuguza mwanawe.
“Mimba yangu haikunisumbua kabisa, nilikuwa nakula kama
kawaida tofauti na wengi huchagua chakula, mimi sikuwa nachagua na nilikuwa nakula haswa.. sikuwa naumwa-umwa, niliendelea na shughuli zangu kama kawaida,
nilikuwa nimeajiriwa duka moja la vifaa vya simu huko Kariakoo.
Anasema alipojihisi u mjamzito, ilipofika miezi mitatu ndipo alianza mahudhurio ya kliniki huko alifanyiwa uchunguzi kwa kipimo cha Ultra Sound
awamu mbili tofauti na nyakati zote mtoto alionekana amekaa vizuri tumboni.
“Desemba 24, 2016 nilijifungua kwa upasuaji katika Hospitali
ya Palestina, nilikuwa nashuhudia kila kinachoendelea, nilikuwa naweza
kuzungumza na wataalamu {sikuchomwa sindano ya kulala moja kwa moja}.
“Walipomtoa walinionesha, nilimuona mwanangu utumbo wake ulikuwa
upo nje,” anasimulia.
Theresia anasema aliogopa mno, alishangaa na maswali lukuki
yalianza kukatisha kwenye ufahamu wake moja baada ya jingine, hakuwa na majibu…
alikosa raha, furaha na amani ilimtoka.
“Ni mtoto wangu wa kwanza, nilishtuka… sikuwahi kuona hata
kwenye familia yetu haijawahi kutokea wala sijawahi kusikia, tatizo hili,”
anasema.
Anaongeza “Wataalamu waliniambia mwanangu atawahishwa
Muhimbili huko atapata msaada zaidi, walinieleza wazi kupona ni 50% kwa 50%,
niliogopa.. walinipa moyo niombe Mungu, atapona.
“Walimpeleka huko, mimi nilibaki Palestina, ndugu
walipofika nilikosa cha kuwaeleza… niliishia kuwaambia mwanangu ana tatizo
kubwa na amepelekwa Muhimbili.
“Walinisihi nisihofu kwa kuwa amewahishwa huko, atapona. Nilipumzishwa
kwa muda kiasi baadae nilipelekwa Muhimbili, nilikuta tayari wamempa huduma ya
kwanza.
“Ingawa utumbo bado ulikuwa nje lakini sasa ulifunikwa na
mfuko mbadala,” anasimulia.
NINI
KILITOKEA?
“Kitaalamu tatizo la kuzaliwa utumbo nje/ tumbo wazi huitwa
‘Gastroschisis’,” anasema Daktari Bingwa
wa Upasuaji wa Watoto Muhimbili Zaitun Bokhari.
Dkt. Bokhari anafafanua zaidi “Ni miongoni mwa matatizo ya
kuzaliwa nayo ambayo hata hivyo yanaweza kuepukwa katika kipindi cha miezi
mitatu ya mwanzo ya mimba.
“Kipindi cha miezi mitatu ya kwanza, ni cha muhimu mno mama
kukizingatia, kimsingi mama ndiye anaweza kupredict ‘kubashiri’ afya ya mtoto
wake.
“Mtindo wake wa maisha… aina ya vyakula anavyokula kipindi
hicho, jinsi anavyohudhurfia kliniki ndivyo afya ya mtoto wake.
Anaongeza “Ki-baiolojia katika miezi mitatu ya kwanza, kitaalamu
tunaita ‘Organogenesis’ ni kile kipindi ambacho zile ‘organs’ {viungo muhimu
vya mwili ikiwamo utumbo’ hutengenezwa yaani zina-forms ile ‘mesoderm’ na ile
‘physiology’ inaanza kuonekana.
“Ndiyo maana ile miezi mitatu ya mwanzo ni muhimu sana
ikiwa mtu anataka kupata mtoto mzuri, kwa sababu pia akiwahi kuanza mahudhurio
ya kliniki na kuzingatia kule ataelekezwa jinsi ya kula na atapewa dawa za
kumuepusha mtoto na magonjwa mbalimbali.
“Kimsingi, kipindi cha ujauzito kile chakula anachokula
mama hakimsaidii tu yeye, kinamsaidia mpaka mtoto aliyembeba tumboni mwake,
kadhalika zile dawa ambazo anakuwa anazitumia.
“Ni kipindi muhimu kuzingatia ulaji unaofaa na kuacha
mtindo mbovu wa maisha kwa mfano unywaji wa pombe kupitiliza, nakadhalika.
Anasema hata hivyo changamoto ni pale wakina mama wengi huanza
kiliniki kwa kuchelewa yaani ile miezi
mitatu inakuwa imeshapita mno. Si sahihi.
TAKWIMU
ZILIVYO
Inakadiriwa kila mwaka duniani mtoto mmoja hadi wawili kati
ya 100,000 huzaliwa na tatizo hilo na Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara
{Tanzania ikiwamo} takwimu zinaonesha tatizo ni kubwa zaidi, kulingana na
tafiti mbalimbali.
“Miaka ya nyuma uliweza kuisha mwaka hatujapokea mtoto
mwenye tatizo hili, wengi walifichwa majumbani na kupoteza maisha, lakini sasa
kwa mwezi tunaweza kuona mtoto mmoja hadi watano.
“Kwa sababu ya teknolojia duni pia hatukuweza kuokoa maisha
yao, wengi walipoteza maisha kwa 95% hadi 100%, lakini sasa tuna mbinu ya
kisasa zaidi na mafunzo tumeweza kuokoa uhai kwa 38%,” anasema.
KIPINDI
KIGUMU
Theresia anasema walikaa Muhimbili kipindi cha mwezi mmoja
mwanawe akihudumia, anakumbuka namna ilivyokuwa changamoto kubwa kwake nyakati
hizo.
“Mtoto alikuwa wodi namba 36 kule mnakwenda tu kuwaona na
nyie wazazi kurudi katika jengo la Magufuli {Hayati Rais wa Awamu ya Tano wa
Tanzania}.
Anasimulia, mwanzoni nilizuiwa kumnyonyesha moja kwa moja,
maziwa yalikuwa mengi niliumia roho kwa kweli kwa kushindwa kumpa ziwa mwanangu.
“Nilielekezwa jinsi ya kuyakamua, nilimpa kwa kipimo
maalum, roho ilikuwa inaniuma… lakini sina jinsi… ule utumbo ulikuwa
unarudishwa ndani kidogo kidogo.
“Katika ile wodi ya wazazi kulikuwa na vitanda vya watu
sita, nakumbuka ‘round’ ya kwanza, ya pili na ya tatu, wenzangu walikuja na
watoto wao wenye matatizo mengineyo ikiwamo kichwa kikubwa, ‘njiti’, matatizo
ya moyo na mengineyo, walifariki dunia.
“Nilikuwa namuomba
Mungu, nasema Mungu wangu ni jaribu gani, mbona hivi, unakuta mwengine
anaruhusiwa kabisa kesho mtandoka, lakini mwanawe anafariki.
Anaongeza “Nilijikuta nawaambia ndugu zangu, nia yangu ya
kuomba nihamishwe kutoka wodi ile na ikibidi niondoke kabisa kurudi nyumbani,
ila walinitia moyo na huku madaktari wakijitahidi mno, kumsaidia mwanangu.
“Hatimaye tuliruhusiwa baada ya hali yake kuonekana ipo vizuri, siku tuliyoondoka wodini kurudi nyumbani wengi walinipongeza wakisema mimi ni mwanamke jasiri
HATUA
ZA UKUAJI
Theresia {Pichani na mwanawe huyo hivi sasa} anasema ni kipindi ambacho kilimpa wakati mgumu pia, kile cha ukuaji.
“Nilikuwa nawaza mno ataweza kutembea?, ataweza kutambaa?... niliwaza
mno zile hatua za mtoto, ataweza kuongea? Nakadhalika.
“Kumbuka kule wodini mwezi mzima alikuwa tu amelala,
nilikuwa namnyoosha nyoosha viungo, nilikuwa kumuuliza Mungu atatembea kweli?
Basi hata asipoongea aweze kutembea japo nitaweza kumtuma mahala.
“Nilipoondoka hospitali nilisema nitamnyonyesha mwanangu
hadi afikishe miezi sita, alipolia nilihisi vibaya, lakini nilimpenda na
kujitahidi kumsaidia, nilishauriwa nianze kumpa chakula baada ya miezi sita.
KLINIKI
YA CHANJO
Anasema siku ya kwanza alipompeleka wataalamu walimshangaa
kwani alikuwa na uzito wa gram 900 huku kadi yake ikionesha alizaliwa na
kilogram 3.
“Walinihoji kwanini, niliwaeleza alizaliwa na tatizo na
Muhimbili waliniaelekeza aendelee na chanjo kwani hamna tatizo lolote,
waliwasiliana nao ndipo walianza kumpa huduma.
“Sikuwa naweza kumueleza kila mtu, maana nilipomvalisha
nguo alionekana tu kama mtoto wa kawaida, japo wapo pia walioniuliza au
nilijifungua ‘njiti’ {kabla ya wakati}, alipungua mno.
“Lakini sasa ni kijana mkubwa, aliweza kupitia hatua zote
za ukuaji kama watoto wengine, sasa yupo shule kwa kweli nina furaha, mama
yangu alikuwa akinitia moyo na kuniombea, namshukuru mno Mungu.
Anaongeza “Darasani yupo vizuri anapenda kuchora katika
mtihani wake amepata 95% kwa somo hilo, somo la ‘reading’ amepata 95% na hesabu
69%, ila kuchora ndilo analolipenda zaidi.
“Nilipojifungua, nililazimika kuacha kazi niliyokuwa
nafanya kariakoo, nilikaa kwa muda wa miaka minne nikimuhudumia mwanangu,
nilihisi nahitaji kuwa karibu naye zaidi.
“Kwa kuwa sasa amekua, nimehamia Dodoma huko nimeajiriwa
huko na mama yangu anaishi na mjukuu wake, napambana kwa ajili ya maisha yangu
na yake ili asome.
“Nawashukuru wataalamu waliomsaidia, naishukuru pia
Serikali kwa kuboresha huduma za afya na hapa Muhimbili walinisaidia mno maana
sikuwa na bima ya afya kipindi hicho.
“Sasa natamani naye siku moja awe daktari bingwa aokoe uhai
wa watoto wengine wanaozaliwa na matatizo,” anasema.
Dkt. Zaitun ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Watoto
Muhimbili anasema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kuwawezesha kuokoa uhai wa mtoto
huyo ni mafanikio ambayo Muhimbili, inajivunia.
“Lakini bado nasisitiza pamoja na mafanikio haya, wito
wangu kila siku kwa wanawake ni muhimu mno kuzingatia kipindi cha kwanza cha miezi
mitatu ya mimba unapojihisi ni mjamzito.
“Nitoe rai kwa jamii pia, linapotokea tatizo la ki-afya
mara nyingi nimeshuhudia mama akikimbiwa na mwenza na kuachiwa kulea mtoto peke
yake, hili si jambo linalofurahisha.
Anaongeza “Ni muhimu wenza kuendelea kuwa pamoja kulea
mtoto, baba akiwa karibu na mama wakilea pamoja, inamsaidia hata mama kuwa na
afya njema ya akili.
“Wengi wanaokimbiwa huwa na msongo wa mawazo na hata kushindwa kupata matokeo chanya ya tiba mapema kuliko wale ambao wenza {wanaume} huwa karibu zaidi,” anasisitiza.
Chapisha Maoni