moja

Responsive Advertisement


Kutokuvaa kofia ngumu huongeza uwezekano wa kuugua. Waathirika wafikishwa Mirembe wakikabiliwa na Sonona 

NA VERONICA MREMA - ALIYEKUWA DODOMA

Ndani ya kipindi cha miezi mitatu, watu wawili hadi watatu walioathiriwa na ajali za barabarani hufikishwa katika Hospitali ya Mirembe iliyopo jijini hapa, wakikabiliwa na ugonjwa wa Sonona.

Sonona (msongo wa mawazo) ni ugonjwa wa akili ambao madhara yake huweza kusababisha mgonjwa husika kujiua au hata kuua mtu mwingine.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza takriban watu 800,000 hujiua kila mwaka duniani wengi wao wakiwa vijana kati ya umri wa miaka 15 hadi 29.

Vifo vitokanavyo na kujiua vinashika nafasi ya pili duniani, nafasi ya kwanza ikishikwa na vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.

Akizungumza katika mahojiano haya maalum Daktari Godfrey Mkama wa Hospitali ya Mirembe na Taasisi ya Isanga jijini Dodoma anafafanua zaidi,uhusiano uliopo kati ya ajali za barabarani na magonjwa ya akili.

“Mirembe tunapokea wagonjwa ambao wanakabiliwa na Sonona kutokana na athari za ajali za barabarani," anasema na kuongeza,

".., wengi huanzia huko katika hospitali nyingine baada ya kupata ajali, wanapoanza kuonesha dalili ambazo si za kawaida (za magonjwa ya akili), ndipo huletwa huku kwetu.

“Wengi ambao nimewaona hapa ni wale ambao walipata tatizo la kifafa kutokana na kupata ajali inawezekana ni hivi karibuni au miaka mingi iliyopita,”.

ATHARI INAVYOTOKEA

Anaongeza “Hakuna muda maalum kwamba baada ya muda huo kupita ndipo muhusika aanze kuonesha dalili za magonjwa ya akili tangu alipopata ajali.

“Kimsingi mtu anapopata ajali ya barabarani na kuumia sehemu ya kichwa, yupo kwenye uwezekano mkubwa wa kupata tatizo la kifafa na hata magonjwa ya akili, siku zijazo katika maisha yake.

“Mtu anaweza kupata kifafa ambacho husababishwa na kovu ambalo limepatikana baada ya kupata ajali ya sehemu ya kichwa,” anabainisha.

Anasema ukubwa wa tatizo na muda wa kuanza kujitokeza huwa inategemea ukubwa wa ajali aliyoipata mtu husika na ukubwa wa athari aliyoipata kwenye ubongo wake.

Anasisitiza upo uhusiano mkubwa kati ya ajali za barabarani na matatizo ya akili hasa ikiwa muhusika anakuwa amepata athari sehemu ya kichwa au anapokuwa amepoteza kiungo fulani cha mwili wake.

Anaongeza “Kwa mfano ikiwa amefanyiwa upasuaji kuondoa mguu au mkono wake, asipopewa ushauri nasaha vizuri, hali hiyo inaweza kumsababishia kupata msongo wa mawazo.

“Baada ya kuondolewa kiungo chake anaweza kuathirika kisaikolojia, lazima asaidiwe kupatiwa ushauri namna gani ataweza kuishi pasipo kiungo chake kilichoendelewa,” anasema.

TAFITI ZA DUNIA

Uvaaji kofia ngumu (Helmet) kwa watumiaji wa usafiri wa pikipiki (bodaboda) hupunguza hatari ya kupata majeraha kichwani kwa asilimia 70 na vifo kwa asilimia 40 endapo ajali inapotokea.

Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linaeleza kutokuvaa kofia ngumu ni miongoni mwa mambo yanayochangia vifo vitokanavyo na ajali za bodaboda.

Tafiti zinatilia mkazo kwamba uvaaji kofia ngumu kwa watumiaji wa usafiri huo ni muhimu kwani zinaweza kuzuia majeraha makubwa kichwani ajali inapotokea.

Kulingana na ripoti ya WHO 2018, ajali barabarani husababisha vifo vya takriban watu milioni 1.35 kila mwaka ikiwa ni sawa na vifo 3,400 kila siku.

Shirika hilo linaeleza vifo vitokanavyo na ajali za barabarani katika nchi zilizopo Barani Afrika ni mara tatu zaidi ya ajali zinazotokea Barani Ulaya.

MTIZAMO WA MADEREVA

Ndani ya Kituo cha Nanenane jijini hapa, Mussa Ismail, hupaki bodaboda kila siku akisubiri abiria, awasafirishe kutoka eneo hilo kuelekea maeneo mengine jijini humu.

Namfuata na kumsihi anipeleke katikati ya jiji baada ya kupata kiwango cha nauli, anawasha bodaboda yake tayari kwa kuanza safari.

Ismail ana kofia ngumu moja tu, wapi ilipo kofia ya pili kwa ajili ya abiria wake anayembeba?

“Dada ni muda mrefu sasa sina kofia ya pili, hata hii moja unayoiona huwa si mara zote naivaa, inakaa tu hapa mbele.

"Kama unahitaji sema nikupe, mimi huwa naendesha hivi hivi bila kuvaa kofia, hakuna tatizo lolote,” anasema huku akinipatia kofia hiyo.

Tunaendelea na safari akinieleza “Awali nilikuwa nabeba kofia mbili lakini abiria wangu huwa hawahitaji kuvaa.

"Wanasema wanaogopa magonjwa ya ngozi, mimi mwenyewe navaa basi tu, sioni kama kuna ulazima sana kuivaa.

“Jiji letu bado halijakua, hakuna magari mengi, tunaendesha kwa ustaarabu, tuvae kofia ya nini?,” anahoji Ismail.

Nilipanda pia bodaboda ya John Kaisanga, tofauti na Ismal, huyu anazo helmet mbili, anasema moja kwa ajili yake na nyingine kwa ajili ya abiria wake.

“Mimi nabeba zote lakini simlazimishi abiria wangu avae au asivae, huwa namshauri avae ili tuepuke kukamatwa kamatwa kwa kosa la kutokuvaa helmet.

"Hasa ikiwa anaelekea maeneo ya katikati ya jiji,” anasema Kaisanga.

HALI HALISI

Takwimu za Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani zinaeleza katika kipindi cha miaka 10 tangu 2009 hadi 2018 watu 8,004 wamefariki dunia kutokana na ajali za bodaboda, watu 35,231 wakijeruhiwa.

 Takwimu hizo zinaonesha madhara makubwa yatokanayo na ajali za bodaboda ambazo zimesababisha vifo vya watu wengi na kuacha wengine wakibaki na ulemavu wa kudumu.

Mwanasheria wa Kikosi hicho, Mrakibu wa Polisi, Deus Sokoni katika mahojiano maalum nasi anasema kutokuvaa kofia ngumu ni miongoni mwa vitu vinavyochangia vifo kwenye ajali za pikipiki.

“Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 inasisitiza juu ya uvaaji wa kofia ngumu, bado  ina upungufu.

"Kwani inamtaka dereva wa chombo cha moto chenye magurudumu mawili au matatu kuvaa kofia ngumu bado kimya kwa abiria anayebebwa katika chombo hicho,” anasema

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) zilizoridhia kukabili na kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za barabarani kwa kiwango cha asilimia 50 ifikapo 2020.

UN inataka kila mwanachama kuwa na Sheria Madhubuti katika eneo la matumizi ya mikanda kwa watu wanaosafiri na magari, vizuizi vya watoto na matumizi ya kofia ngumu.

Vile vile, matumizi ya vileo na namna ya kudhibiti mwendokasi na matumizi ya simu za mkononi wakati dereva akiendesha gari barabarani.

Inasisitiza kwamba ikiwa juhudi hazitafanyika lengo la kupunguza idadi ya vifo na ajali za barabarani hazitoweza kutimia ifikapo 2030.

JAMBO LA MUHIMU

Dk. Mkama anaongeza “Jambo muhimu ni kuhakikisha mtu aliyepata ajali anafikishwa mapema hospitalini ili apatiwe matibabu mapema.

"Hatua hiyo huweza kusaidia kumuepusha kuishia kupata magonjwa ya akili," anasisitiza.

Anabainisha “Kwa sababu wanavyochelewa kwenda hospitali na wanavyochelewa kupata matibabu ndivyo wanavyofanya ule uwezekano wa kupata magonjwa akili unaongezeka zaidi,”.

MZIGO KWA TAIFA

“Hili ni tatizo kubwa nchini, tuna wimbi kubwa la ajali za barabarani hasa kwa vijana kupitia bodaboda, uendeshaji wa magari si mzuri.

"Watu wanaenda mwendo kasi, wanaendesha wakiwa wamelewa si waangalifu wanagonga wapita njia, magari yanagongana, yanaanguka, watu wanakufa, wanapata ulemavu.

“Yote hata yanachangia kuongeza mzigo kwenye magonjwa yasiyoambukiza, sasa hivi  yanachukua karibu asilimia 40 ya Bajeti ya afya.

"Fedha ambazo zinatumika kutibu magonjwa haya,” anasema Mkurugenzi wa Idara ya Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Grace Magembe.

Dk. Magembe anasema kuna ongezeko la vifo vitokanavyo na magonjwa hayo kwa kiwango cha asilimia sita, kutoka asilimia 27 mwaka 2015 hadi kufikia vifo asilimia 33 mwaka 2017.

“Kuna ongezeko la wagonjwa wanaopata huduma katika vituo kutokana na magonjwa haya kwa kiwango cha asilimia 24, kutoka watu milioni 3.4 mwaka 2016 hadi watu milioni 4.2 mwaka 2018.

“Magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na saratani, kisukari, moyo, shinikizo la damu, kiharusi na mengineyo, matatizo yatokanayo na ajali yamo humu kwenye magonjwa haya.

"Watoto wanagongwa, vijana wanajeruhiwa, yanachangia kuongeza mzigo wa gharama za matibabu,” anasema Dk. Magembe.

Anaongeza “Gharama za kutibu magonjwa haya ni kubwa, tofauti na magonjwa ya kuambukiza, ambayo mengi mtu huweza kupona baada ya kutibiwa.

"Magonjwa yasiyoambukiza mtu hutibiwa maisha yake yote, hata gharama za ugunduzi ni kubwa.

TUNATOKAJE?

Dk. Magembe “Haya ni magonjwa mtambuka, kila mtu anawajibu wa kuhakikisha tunajikinga kuanzia mwananchi mmoja mmoja, wadau na Taasisi za Serikali.

“Kuelekea 2030 tunakusudia tuwe tumepunguza kiwango cha magonjwa haya na ajali za barabarani," anasema.

Anabainisha "Novemba 14, mwaka huu Serikali ilizindua Mpango Mkakati wa Kuzuia na Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza, kuongeza nguvu.

“Kwa kiwango kikubwa yanatokana na mtindo mbovu wa maisha, ulaji usiofaa yaani vyakula vyenye chumvi nyingi, mafuta mengi, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na kutokufanya mazoezi.

"Kwa upande wa ajali za barabarani asilimia kubwa ni makosa ya kibinadamu. Utaona hapo kuna sekta mbalimbali zinahusika katika kuongeza nguvu kupambana na magonjwa haya.

"Ikiwamo ya michezo, mazingira, kilimo, ujenzi, uchukuzi na mawasiliano  na sekta nyinginezo, tunaona kila mmoja wetu akiwajibika tunaweza kufikia lengo ifikapo 2030.

“Suala la ajali za barabarani, tukizingatia Sheria ya Usalama Barabarani, uendeshaji unaozingatia alama za barabarani.

"Kuepuka vilevi wakati wa uendeshaji, kuepuka mwendo kasi, kuwa wastaarabu barabarani, tutaweza kudhibiti na kuzuia,” anasema.

Anaongeza “Tunatambua kuna watu wanafanya mazoezi lakini barabara zetu nyingi zilizojengwa miaka iliyopita si rafiki.

"Katika hili tunawaomba madereva waendeshe kwa ustaarabu ili wale wanaofanya mazoezi wawe salama.

“Lakini pamoja na hayo, hivi sasa katika miji ambayo inajengwa, suala la mazingira rafiki ya barabara kwa kila mtumiaji linazingatiwa,  ndiyo maana kupitia Mpango huu uliozinduliwa sekta zote zinahusishwa.

“Sasa hivi miji inayojengwa inapangwa vizuri, kwa sababu Serikali imeona changamoto hii, hakuna mji unaojengwa pasipo kuainishwa maeneo ya michezo, ya kupumzika.

Dkt. Maghembe anaongeza "Hata barabara zetu zinazojengwa zina sehemu ya watembea kwa miguu.

“Tunaendelea kuhimiza matumizi sahihi ya barabara hasa wale wenye magari kuzingatia Sheria ya Usalama Barabarani, si tu kwa sababu wao wana magari basi waendeshe vibaya, lazima wazingatie Sheria,”.

1 Maoni

  1. Hongera Vero, kazi zako ni nzuri.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement