moja

Responsive Advertisement

Ni kosa kwa mujibu wa Sheria kujihusisha na biashara au matumizi ya dawa za kulevya ikiwamo bangi, nchini Tanzania adhabu yake inaweza kukugharimu hata miaka 30 jela.

Na Veronica Mrema - Tanga

Ukirudi nyuma miaka 98 iliyopita, mnamo 1906 kipindi ilipoanzishwa Hospitali ya Afya ya Akili Lutindi ripoti zinaeleza idadi kubwa ya wagonjwa waliofikishwa hapa waliugua, kwa sababu ya asili zao.

Yaani walipata magonjwa mbalimbali ya akili kutokana na kurithi vinasaba ndani ya mnyororo wa vizazi vyao.

Lakini mambo ni kinyume sana kwa miaka ya karibuni, ripoti zineleza asilimia kubwa ya wagonjwa wanaoletwa Lutindi, kichocheo kikubwa ni matumizi ya dawa za kulevya na pombe.

Asilimia ndogo inayofuata wameugua kwa sababu ya tatizo la msongo wa mawazo ‘depression’ kutokana na mambo mbalimbali yaliyowasonga na kuwatatiza katika maisha yao.

“Niliambiwa nijaribu ni kitu kizuri, mimi bila kupinga nikatumia,” simulizi ya kijana mmoja kati ya tuliowakuta hapa Lutindi.

Jina lake halisi ameomba lihifadhiwe, kwa mantiki hiyo ndani ya makala haya tumempa jina Wenado.

Aliletwa na nduguze baada ya akili yake kuathirika, kisababishi cha yote haya, anasema ni matumizi ya bangi.

Hii ni aina ya dawa ya kulevya ambayo kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2023, inaeleza takribani watu milioni 219 waliitumia mwaka 2021.

Hiyo ni sawa na 4% ya idadi ya watu waliopo ulimwenguni na ndani ya kipindi cha muongo mmoja uliopita idadi ya watumiaji bangi imeongezeka kwa 21%.

Barani Afrika, inatajwa huko Afrika Kaskazini ndipo kitovu cha biashara haramu ya bangi ambayo husindikwa ‘cannabis resin’ [kuandaliwa] kuelekea Ulaya Magharibi.

Matumizi ya juu zaidi yapo Afrika Magharibi na kati, karibu 10% ya watu waliripotiwa kutumia bangi katika kipindi cha mwaka 2020, hususan Nigeria.

Ripoti hiyo inaeleza nchi nyingi Afrika zina uzalishaji wa bangi na imeendelea kuwa moja ya dawa za kulevya inayosababisha athari kubwa miongoni mwa watu wanaopatiwa matibabu ya uraibu.

VIJANA ‘SHIMONI’

Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 16 kote ulimwenguni 5.3% sawa na watu milioni 13.5 walitumia bangi mwaka 2021.

Ripoti hiyo inaeleza athari za matumizi ya bangi kwa vijana ni kubwa zaidi kwa ubongo na afya yao ya akili.

Wenado, ushawishi wa marafiki zake ndiyo hasa ‘mzizi’ wa yeye kuangukia katika matumizi ya bangi.

“Nilikuwa na umri mdogo [kipindi hicho] lakini baada ya pale [kuitumia] sikupenda,” anasema na kuongeza,

“Kwa sababu sikuwa na utulivu, sikuwa na heshima, [yaani] sina ile adabu ya kutumwa, nikaenda.., sina ule utiifu.

Tangu hapo hakuwa tena na ule utimamu wa akili, alipotumwa hakwenda na chochote alichoagizwa na wakubwa zake hakufanya.

“Nilikuwa nawajibu vibaya hata baba, mama na ndugu zangu wote,” Hali ilipofikia hapo familia yake ikafanya uamuzi wa kumfikisha Lutindi.

NDANI YA LUTINDI

Hii ndiyo hospitali ya kwanza kuanzisha huduma ya matibabu ya akili Tanzania, sasa inashuhudia tofauti kubwa!

“Asilimia kubwa [ya wagonjwa wanaofikishwa] ni watumiaji wa dawa za kulevya na pombe,”.

Kauli yake Mganga Mfawidhi wa Lutindi Dkt. Katyetye Marwa wakati wa mahojiano haya maalum yaliyofanyika hivi karibuni, hospitalini hapa.

Anaongeza “.., wenye matatizo kawaida ya asili ni wachache. Hii ni tofauti kabisa na miaka ya nyuma hospitali hii ilipoanzishwa.

Historia inachambua kwa kina, kipindi hicho wagonjwa wa akili waliofikishwa hapa chanzo ilikuwa ni kwa sababu ya kurithi vinasaba kutoka kwa vizazi vyao.

Chanzo kingine ni matatizo mbalimbali yaliyowasababisha msongo wa mawazo katika maisha yao.

Hata hivyo miaka ya sasa.., “75% [ya wagonjwa wanaoletwa Lutindi, chanzo] ni wa dawa za kulevya,” anafafanua Dkt. Marwa.

Wenado ni miongoni mwa 75% ya wagonjwa wa akili wanaotibiwa Lutindi baada ya kuathiriwa na dawa za kulevya.

Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa takriban milioni 7 wenye magonjwa mbalimbali ya akili kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani [WHO].

Tathmini ya Wizara ya Afya Tanzania inaonesha wengi wao wanapata magonjwa hayo kutokana na mtindo mbovu wa maisha ikiwamo matumizi ya dawa za kulevya na pombe.

Tanzania inakadiriwa pia ina watu milioni 7 wanaougua zaidi ya watu milioni1.5 wanaoishi na ugonjwa wa Sonona (Depression).

THC TISHIO ZAIDI

Mtu anapoanza kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya ubongo wake huathirika siku hadi siku.

Ripoti ya utafiti uliotolewa hivi karibuni na Mtaalamu wa Magonjwa ya Akili Dkt. Marta Di. Forti unaeleza utumiaji bangi ya kila siku, unachangia ongezeko la matatizo ya akili, 

Dk. Adrian James kutoka Chuo cha Royal Kitengo cha Magonjwa ya Akili, Uingereza anaitaja bangi yenye kemikali nyingi ya THC husababishia hali inayoitwa ‘psychosis’.

Hali hiyo humfanya mtu kushindwa kutambua mambo, mtumiaji anasikia sauti, kuona visivyokuwapo au mawazo mchanganyiko.

Madaktari nao wanahofia kwamba kuongezeka matumizi ya bangi yenye nguvu zaidi yenye  kemikali aina iitwayo THC, inayowalewesha watumiaji.

Katika moja ya oparesheni zake DCEA ilinasa magunia haya ya bangi kavu ambazo ziliteketezwa kwa moto.

OPARESHENI TANZANIA

Ripoti ya Hali ya Matumizi ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2022/23 ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya [DCEA], inaeleza..,

Kwa mwaka 2023 kiasi cha tani 1.757.56 za dawa za kulevya aina ya bangi kilikamatwa kikihusisha watuhumiwa 8,803 kati yao wanaume ni 8,180.

Ndani ya kipindi hicho pia kuliibuka uingizaji na matumizi ya bangi mpya iitwayo ‘skanka’ ambayo inadhaniwa kuwa inazalishwa huko nchi za Kusini mwa Afrika.

Bangi hiyo mpya ni mchanganyiko wa aina mbili za bangi ikiwa na kiasi kikubwa zaidi cha kemikali iitwayo THC ambayo inatajwa kuwa na athari kubwa zaidi kwa watumiaji.

Kiasi cha bangi kilichokamatwa mwaka 2023 ni mara tano zaidi ya kiasi kilichokamatwa kwa miaka tisa iliyopita kuanzia 2014 hadi 2022, kulingana na ripoti hiyo.

“Tangu nimefika Lutindi na kutibiwa nafurahi, mtu akinielekeza jambo namuelewa,” anasema Wenado na kuongeza,

“Jamii yangu naieleza, kama kuna watu wapo huko na wazazi/walezi wao wanaona wamebadilika wawaulize na kuwafuatilia.

“Wawalete huku Lutindi pia waje kutibiwa, Serikali naomba wazidi kuboresha mazingira ya afya ya akili na kuzidi kuwafuatilia watu waliopo nje waletwe hapa kupata matibabu,” anatoa rai.

JAMII ISIWE ‘MWIBA’

Mgonjwa mwingine anayetibiwa hapa [jina linahifadhiwa] naye anasema “Jamii inatuchukulia vibaya kwamba tuna tabia mbaya bila kujua sababu kuu iliyosababisha tuingie katika tatizo hili ni ipi.

“Hii inaleta unyanyapaa kwa wagonjwa wa akili, jamii naomba ichukulie ugonjwa wa akili ni tatizo kama matatizo mengine na walete wagonjwa kwenye vituo vya matibabu.

Anasema yeye alipata tatizo la msongo wa mawazo lilisababisha kutumia pombe kupita kiasi huku muda mwingi akijitenga na wenzake.

Anasema bosi wake wa kazini alitambua hilo na kuamua kumpa likizo kisha kumpeleka Lutindi ili akatibiwe na sasa anaendelea vizuri.

Joel Zakharia ni mwanafunzi katika Chuo cha Uuguzi Korogwe aliye katika mafunzo kwa vitendo Lutindi anasema ni hatua nzuri kuhamasisha na kuelimisha jamii kulinda afya ya akili.

“Asilimia kubwa ya watu wakija kutibiwa hapa wakiruhusiwa kurudi nyumbani baada ya muda mfupi wanarudi tena hapa, ukiacha sababu nyingine zote, mtizamo hasi wa jamii unachangia hili.

Anaongeza “Labda alipotoka alisababisha madhara fulani sasa amerudi tena atasababisha tena tatizo.

“Jamii inamchukulia bado ni mtu mbadala kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii iwe kipaumbele kubaini watu wenye matatizo ya akili.

“Pia wakishapata tiba na kurudi majumbani, wajue wameshatibiwa na kurudi katika hali zao za kawaida,” anasisitiza.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement