Na Veronica Mrema
Siku chache zikiwa zimesalia kufikia matembezi ya hisani [MEWATA WOGGING], Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameweka wazi kwamba atashiriki ipasavyo kwani yana nia njema ya kujenga jamii yenye afya bora.
Akizungumza mapema leo baada ya kuhitimika kwa matembezi ya hisani [Walk the Talk] ya Shirika la Afya Duniani [WHO Tanzania], Waziri Ummy amesisitiza, yupo tayari kushiriki matembezi yoyote ili kuhimiza jamii kujenga desturi ya mtindo bora wa maisha.
MEWATA WOGGING imeandaliwa na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania [MEWATA] April 20, 2024 inatarajiwa kufanyika huko Mbweni JKT - Dar es Salaam.
"Mmeniona nimepungua na niseme nitaendelea kupungua zaidi, [kimsingi] tule ila tusiendekeze tabia bwete [tufanye mazoezi ya kushughulisha mwili]," amesema.
Ameongeza "Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha tunaendelea kuhimiza Watanzania kufanya mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha.
"Wiki ijayo nitashiriki MEWATA, tutatembea kuunga mkono mapambano dhidi ya saratani za wanawake.
Amebainisha "Wikiendi nyingine nitatembea na LUKIZA Autism [April 28, 2024] ... kwa hiyo mimi watanzania kama kuna mtu anataka kutembea na waziri wa afya nipo tayari.
"Tutembee iwe sehemu ya kuhamasisha kujilinda na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.,".
Awali amesisitiza mambo mengine ya msingi ambayo Serikali itaendelea kuyazingatia katika sekta ya afya ili kuiimarisha zaidi, Tanzania.
Ameongeza "Tutaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya watoa huduma za afya ikiwamo kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa ngazi zote.
"Tutaendelea kuwekeza katika kuimarisha upatikanaji wa rasilimali watu ya afya kwa ngazi zote kuanzia huduma za msingi hadi ubobezi.
"Tutaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na elimu ya afya kwa umma," amesisitiza Waziri Ummy.
Chapisha Maoni