moja

Responsive Advertisement

 


Na Veronica Mrema

Ufanyaji mazoezi kwa ajili ya kujenga afya ya mwili na jamii kwa ujumla, unachukua ‘sura mpya’ nchini Tanzania, sasa imeteuliwa siku maalum ya michezo kwa wote [‘Sports 4 All’].

Jumamosi ya kila wiki kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 3 asubuhi Serikali imetangaza itakuwa ni siku ya michezo kwa wote.

Barabara ya Daraja la Tanzanite itafungwa ndani ya muda huo kupisha watu kwa ajili ya kufanya mazoezi na matembezi.

Waziri Mkuu [PM] wa Tanzania Kassim Majaliwa ameweka wazi hilo mapema leo mbele ya mamia ya watu walijitokeza viwanja vya Farasi kushiriki matembezi ya hisani ‘Run4Autism’.

Ni msimu wa tatu wa matembezi hayo ulioandaliwa na Taasisi ya Lukiza Autism, PM Majaliwa amesema hatua hiyo inalenga kulinda na kuimarisha usalama barabarani kwa wafanya mazoezi.

“Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa wananchi wake kushiriki michezo mbalimbali, mimi nimeshiriki ‘marathon’ nyingi hapa … nimeona wananchi wanavyoshiriki.

“Lakini pia kila siku jioni ninapofanya mazoezi mjini hapa huwa napishana na makundi ya watu rika mbalimbali wakifanya mazoezi,” amesema na kuongeza,

“Nimeona makundi ya vijana wakiunda, vikundi vya ‘jogging’, Temeke, Kinondoni, Kigamboni Ubungo na Ilala tuna makundi mengi.

“Wapo watu wenye umri mkubwa wanahitaji kufanya mazoezi, vijana na wana-familia [pia] wanahitaji kufanya mazoezi.

‘BEATS NCD’s’

Ufanyaji mazoezi ni miongoni mwa mambo yanayohimizwa na wataalamu wa afya ili kupunguza na hatimaye kutokomeza janga la ongezeko la Magonjwa Yasiyoambukiza [NCD’s].

Baadhi ya mataifa nchini Afrika ikiwamo Rwanda kwa miaka mingi imekuwa na siku maalum ya ufanyaji mazoezi wa pamoja kwa raia wake.

Ni agenda ya dunia kupambana dhidi ya NCD’s kwani magonjwa hayo yanachangia idadi kubwa ya vifo kwa zaidi ya 70% hususan katika nchi zinazoendelea Afrika, Tanzania ikiwamo.

Nchini Tanzania NCD’s huchangia 40% ya vifo vyote kila mwaka na kutafuna bajeti ya afya kwa zaidi ya 40%.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaeleza mwaka 2023 Shinikizo la Damu na Kisukari ambayo ni miongoni mwa magonjwa hayo yamechangia idadi kubwa ya waliohudhuria kliniki mbalimbali.

‘SPORTS 4 ALL’

PM Majaliwa amesisitiza “Serikali tulikuwa hatujaweka mipango vizuri nchi za wenzetu wapo mbali mno, sasa na sisi tunaanza Tanzania na Jiji la Dar es Salaam.

“Kila siku ya jumamosi ya kila wiki ni siku ya michezo kwa wote ‘Sports 4 All’.

“Siku ambayo itawaweka pamoja watu wenye familia na watoto wao, mume na mke, vijana makundi mbalimbali.

“Waendesha baiskeli, nimeona pia tunapishana na magari na bodaboda jambo ambalo linaweza kuleta athari kubwa ya watu kugongwa wakiwa wanafanya mazoezi,” amesema.

Ameagiza “Mkuu wa Mkoa [wa Dar es Salaam] na wakuu wa wilaya [Kinondoni na Ilala] kila jumamosi tutakuwa tunaifunga barabara moja.

“Kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa 3 asubuhi. Kutoka [makutano ya] Ocean Road Hospital mpaka Agha Khan Hospital.

“Tunapita Daraja la Tanzanite tunafika makutano kwenda mpaka ‘coco beach’ [fukwe za Coco].

NJIA MBADALA

PM Majaliwa amebainisha barabara hiyo kila jumamosi watumiaji kwa njia ya magari kwenda mjini watapita katika njia nyinginezo ndani ya muda huo.

“[Hii itafungwa] ili iwalete pamoja wana-familia, makundi ya ‘jogging’, vijana, kufanya mazoezi kuanzia saa 12 asubuhi mpaka 3 asubuhi,” amebainisha.

Amesema wanaotoka barabara ya ‘Sea Cliff’ kuingia jijini wakifika mwanzo wa ‘coco beach’ pale barabara ya Tumbawe, waingie pale kuelekea mjini.

“Wakatokea Kenya [KCB Bank] kupitia salnder bridge. Kwa maana hiyo Mkuu wa Wilaya Ilala na Kinondoni mtafunga eneo lile ili watu watembee.

“Ikifika saa 3 asubuhi fungua ili watu waendelee na shughuli zingine,” ameagiza.

Amebainisha eneo la viwanja vya Farasi litumike kwa michezo kila jumamosi kama sehemu ya maandalizi kwa watembeaji, wakimbiaji na waendesha baiskeli.

“Eneo la fukwe za Agha Khan na ni la ‘ku-park’ [kuegesha] magari [kwa] watakaoamua kutumia fukwe au barabara [hiyo kwa mazoezi] mpaka kule Ocean Road.

“Eneo la ‘coco beach’ kuanzia hapo mwanzo [eneo la mabanda ya biashara’ [nalo] liwe la ‘ku-park’ magari na wakimbiaji waanze mbio zao,” ameagiza.

SI JAMBO GENI

PM Majaliwa amesisitiza [Sports 4 All na kuteua barabara ya kufunga] si jambo geni na kwamba Tanzania ndiyo nchi ambayo imechelewa kuchukua hatua.

“Tunaanza sasa watu watembee kwa uhuru mkubwa, vyombo vitakavyotumika [katika barabara inayofungwa] ni ‘ambulance’ [gari la kuhudumia wagonjwa],” ameagiza.

Amesema ‘ambulance’ hiyo itateuliwa kwa ushirikiano kati ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na Mkuu wa Wilaya ya Ilala.

Amesema wengine wanaoruhusiwa kupita njia hiyo ni wafanya mazoezi kwa njia ya baiskeli.

“Bodaboda hapana [hawataruhusiwa] isipokuwa ile inayochukua kumbukumbu za kundi fulani.

“.., na kwa kibali maalum kwa wale wanaokuwa wanasimamia zile njia. wengine watapita zile barabara zingine zipo nyingine na zipo nyingi,” amesisitiza.

Ameagiza wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kuhakikisha maeneo yote ambayo watu wataegesha vyombo vyao vya usafiri yanakuwa salama wakati wote wa mazoezi.

HATUA MADHUBUTI

Hatua hii ni mahususi na mwendelezo wa Serikali kupitia Wizara ya Afya ambayo tangu mnamo mwaka 2017 imekuwa ikihimiza jamii kujenga desturi na utamaduni wa kufanya mazoezi.

Awali akisoma taarifa yake mbele ya PM Majaliwa katika matembezi ya Run4Autism, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alimuomba,

“Tumekimbia kuongeza uelewa kuhusu Usonji lakini pia tumekimbia kuimarisha afya zetu kwa sababu mazoezi ni

Ameongeza “Leo tumekimbia kwa amani, hakukuwa na bodaboda au magari ambayo yametuzuia tusitembee au kukimbia kwa amani.

“Tunaomba kila jumamosi barabara hii ya Tanzanite ifungwe kila jumamosi saa 12 asubuhi hadi 3 asubuhi tukimbie/tutembee kuanzia Farasi, Agha Khan hadi Ocean Road,” amewasilisha.

Ameongeza “Tutoke jasho, nikiangalia takwimu za malipo ya Mfuko wa Bima ya Afya [NHIF] kwa NCD’s mwaka 2015/16 ililipa Tsh. Bil. 26.4 sawa na 12% ya malipo yote.

“ Mwaka 2021/22 fedha zinazohusu NCD’s ziliongezeka kutoka Tsh. Bil 26.4 hadi Tsh. Bil. 99.08 sawa na 15% ya malipo yote ya NHIF,” amebainisha.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement