Na Veronica Mrema
Ndoa 14,600 zipo ‘ICU’ migogoro tele imerekodiwa na bado haijapata ahueni/suluhu, 'ICU' ni chumba cha wagonjwa wahututi ambako mgonjwa huhitaji uangalizi wa karibu ili kunusuru uhai wake.
Idadi hiyo imerekodiwa kipindi cha Julai, 2023 hadi April,
2024 [yaani miezi 10] ofisi za Ustawi wa Jamii.
Migororo/mifarakano hiyo imerekodiwa pia ofisi nyinginezo
ambazo zipo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi
Maalum.
Waziri Dkt. Dorothy Gwajima amebainisha hayo alipozungumza
na waandishi wa habari punde baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa 21 wa Mwaka wa
Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania [MEWATA].
“.., na hizo ndizo zilizoripotiwa,” amesema na kusisitiza kwamba mifarakano,
migongano na migogoro imekuwa ikichangia visa vingi vya kikatili vinavyoshuhudiwa
ndani ya jamii.
Ameongeza “Mwisho wa siku tunaona ndoa imepasuka, lakini
chembechembe gani za afya ‘determinats’ za afya [vizingatio] vya afya vipo mule?.
“Ukirudi huku tunaona kuna ujeuri, kutokuwa na heshima …
kuna vitu vipo mule nani anavifanyia utafiti, [yaani] tuzuie nini [au] tufanyeje tuzui?.
“Hii ni nguvu ya MEWATA kuingia kwa jamii, kuleta ule
utengemao,” amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Kwa mantiki hiyo amekialika rasmi Chama hicho
kilichosheheni madaktari mabingwa na wabobezi katika nyanja mbalimbali za afya
ili kushirikiana na Wizara hiyo bega kwa bega kwenda kuisaidia jamii.
Amesema amefungua milango wazi kwa MEWATA kwani wana nafasi
kubwa na jamii inawaamini hivyo ni wakati mwafaka kwenda kuipatia maarifa
yatakayoikomboa.
Makamu wa Rais wa MEWATA na Mtaalamu wa Masuala ya Afya ya
Jamii Dkt. Mary Sando amesema wapo tayari kushirikiana na Serikali kupitia
Wizara hiyo kuihudumia jamii.
“Sisi kama wanawake tunaotamani kuona afya ya jamii
[inaimarika] na ukatili unatokomea tumefurahi kuwa naye [Waziri Gwajima]
akimsaidia Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Ameongeza “Kama mnavyofahamu sisi MEWATA huko nyuma
tulikuwa tunaitwa ‘wapiga debe’ [yaani watu wanaovalia njuga suala fulani kwa
maslahi mapana ya kuijenga afya ya jamii].
“Wote tunafahamu na tunaona ukatili wa kijinsia
unavyoendelea, tunaamini tukiweza kwa utaalamu wa kisayansi [tuliojaliwa tutashirikiana
na Wizara inayotengeneza miongozo.
“Tutaweza kusaidia kupiga hatua ambayo Wizara pamoja na
wadau mbalimbali wanajaribu kufanya ili kutengeneza jamii iliyo na ustawi
mwema,”.
Amesema Dkt. Mary ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Shirika la AAPH.
Chapisha Maoni