Na Veronica Mrema
Historia kubwa Barani Afrika kwa mara ya kwanza imeshuhudiwa, watafiti nguli, wataalamu wa masuala ya Magonjwa Yasiyoambukiza [NCD’s], watunga sera na
watu wenye NCD’s wakijadili kwa kina pamoja.
Mjadala ulioangazia namna gani Bara hilo litaongeza kasi katika
kukabili NCD’s kwani idadi kubwa ya raia wake hivi sasa wanaugua na wengi wanapoteza
uhai, kila mwaka.
Ni magonjwa ambayo mtu yeyote anayeugua hawezi kumwambukiza
wengine, ingawa katika kundi hili la magonjwa yapo pia baadhi yanayorithiwa.
Yaani mtu anaweza kuzaliwa na ugonjwa kwa kurithi vinasaba
vya ugonjwa husika kutoka kwa mzazi / wazazi wake, kwa mfano Siko Seli.
“Nikiwa ‘ki-changa’ mno muda mwingi nilikuwa nalia sana,
wazazi wangu hawakuelewa kilichokuwa kinanisumbua,” anasema Edith Mukantwari.
Ni raia wa Uganda anasimulia maisha yake halisi ya utotoni,
ilikuwa kipindi kigumu zaidi alichopitia, muda mwingi na mara kwa mara alilazwa
hospitalini kupatiwa matibabu.
Aliishi hivyo hadi alipofikia umri wa miezi minane,
alipofanyiwa uchunguzi wa kina na kugundulika hospitalini, amezaliwa na ugonjwa
wa Kisukari aina ya kwanza [T1D].
Shirika la Afya Duniani [WHO] inautaja ugonjwa wa Kisukari
ni muuaji wa kimya-kimya kwa raia wengi Barani Afrika.
WHO inaeleza kipindi cha 2011 hadi 2021 Afrika ilirekodi
ongezeko la juu mara tano zaidi la T1D kwa kundi la watoto na vijana balehe
chini ya umri wa miaka 19.
WHO inasisitiza ikiwa juhudi hazitafanyika hali hiyo huenda
idadi itaongezeka kutoka watoto wanne katika kila watoto 1,000 wenye T1D hadi
watoto 20 kwa kila watoto 1,000.
Ni 36% ya nchi za Afrika zilizoweza kuweka dawa muhimu
katika vituo vyake vya kutolea huduma za afya kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya
mwaka 2019.
Edith anasema bado kuna kundi kubwa la watu wenye T1D bado hawajatambuliwa
lakini pia hata waliotambuliwa wengi hushindwa kumudu gharama za matibabu kwani
ni kubwa.
“Nakumbuka, hata mimi kabla sijagundulika nimepata kutibiwa
mara nyingi homa, hata nilipokuwa katika shule moja ya bweni niliwahi kuugua
lakini nilipopelekwa hospitalini hawakutibu inavyopaswa.
“Ilipelekea kupoteza kwa kiasi fulani uwezo wangu wa uoni, usiku
niliteseka mno kwa kupata haja ndogo mara nyingi kila baada ya dakika 30.
Anasimulia “Nilikuwa nalala na ndoo chumbani kwangu ili
nijisaidie humo, ni miaka 16 sasa naishi na T1D.
“Si maisha mepesi … ni lazima nipate sindano kila siku ili hali yangu iwe sawa na niweze kuendelea na maisha yangu mengine kama watu wengine wasio na ugonjwa,” anasimulia.
‘NILIKIONA KIFO’Saratani ni kati ya NCD’s ambazo zinaathiri pia raia wengi wa
Afrika na hata kusababisha vifo.
Akiwa na umri wa miezi 9 Mosses Echodu aligundulika ana ugonjwa
wa Saratani na tayari ulifika hatua ya nne, ambayo kwa kawaida ni ngumu
kutibika na kupona.
“Nilikuwa naishi na bibi yangu, mama yangu alikuwa amerudi
shule,[alijifungua mimi akiwa na umri mdogo],” anabainisha.
Anasimulia “Siku moja nilipokuwa nikicheza na wenzangu
ghafla nguvu ziliniishia, nilijihisi vibaya, nilirudi nyumbani.
“Nilipelekwa hospitalini mara kadhaa, walikuwa wakinitibu
homa niliyokuwa nayo,” anasema.
Anasema ni hadi pale mjomba wake mmoja alipofika,
alimchukua kutoka kijijini huko Entebbe na kumpeleka hospitali moja iliyopo
Kampala, Uganda.
“Kipindi kile, usafiri ulikuwa changamoto kubwa, tulisafiri
takriban saa sita kufika Kampala kutokea Entebbe tofauti na sasa unaweza kufika
kwa saa mbili,”.
Anasema ndipo aligundulika ana saratani na kuongeza, “Hali
yangu haikuwa nzuri, nilijua mwisho wangu umefika .., ninakufa, lakini
namshukuru Mungu bado nipo hai hadi leo.
‘BETRI
YA MOYO’
‘Rheumatic Heart Disease’ ni ugonjwa wa moyo ambao mtu
huzaliwa nao, Ruth Wahu Ngwaro akiwa na umri wa miezi mitatu aligundulika ana tatizo
hilo.
Anasema si safari nyepesi kuishi, akikabiliana nao, anakumbuka
akiwa na umri wa miaka 15 ilikuwa nyakati ngumu zaidi.
“Familia yangu ni duni na baba yangu alihitaji kiasi cha
Dola 200,000 kwa ajili ya kufanikisha upasuaji wangu.
“Nilishindwa kabisa kwenda shule, ilibidi ahangaike kuomba huku na kule hadi tukapata fedha hiyo nikapandikizwa ‘betri’ ya moyo [pacemaker] ambayo naishi nayo hadi leo,” anasema.
‘SI HALI INAYOTABIRIKA’Arafa Said yeye amezaliwa na ugonjwa wa Siko Seli anasema
si hali inayotabirika na kuzoeleka hata kidogo juu ya ugonjwa huo.
“Ni kama vile ‘there is a ghost in my body’ [kuna kitu
kigeni, kikubwa na kibaya mno ninaishi nacho ndani ya mwili wangu], kinaendesha
maisha yangu.
“Yaani unaniona hapa mbele yako sasa hivi ni mzima lakini
punde naweza kuugua na nikalazimika kulazwa wodini kwa matibabu,”.
Ni raia wa Tanzania anasimulia, “Ni hali ambayo nyakati
nyingine hutusababishia changamoto lukuki tunapata ‘complications’ [madhara
yatokanayo na ugonjwa huu].
“Yaani [complication] inaweza kukushambulia popote pale
ikaathiri figo zako na kila kitu,” anasema.
‘MZIGO
MZITO’
Ni wachache kati ya wengi wanaopambana na NCD’s Afrika kila
siku ya maisha yao, walipata nafasi ya kupaza sauti zao mbele ya dunia.
Tanzania ilichaguliwa na WHO Kanda ya Afrika [AFRO-WHO] kuandaa
mkutano huo mkubwa wa kwanza wa aina yake ICPPA, washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa zaidi ya 15 walijadili pamoja.
PEN-Plus huu ni mpango mahususi unaangazia zaidi magonjwa makuu matatu ya NCD’s yanayoathiri kundi kubwa la watoto wa Afrika [Kisukari aina ya kwanza, Siko Seli na Magonjwa ya Moyo].
NCD’s, takwimu za WHO zinaeleza huchangia zaidi ya 70% ya
vifo vinavyotokea kila mwaka Barani Afrika na wengi wanaofariki ni watoto na vijana.
Nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ndiko haswa vifo
vingi hurekodiwa, ikiwamo Tanzania, Taifa hilo la Afrika Mashariki kila mwaka Wizara
ya Afya hurekodi zaidi ya vifo 40% kwa NCD’s.
“Ni vigumu mno kuishi na T1D nchini Uganda pia, nimewahi
kukutana na mwanamke mwenye Kisukari na wanawe wawili pia waligundulika wana
T1D,” anasema Edith.
Anaongeza “Mama yule alifariki, wanawe walibaki wakihangaika wenyewe siku moja mmoja wao alinitafuta na kuniambia [“Dada tunakosa hata hela ya kwenda hospitali kupata dawa,”].
HALI NGUMU“Aliniambia nisichoke kuwasaidia kwani wananihitaji mno,
ilikuwa siku ngumu kwangu, napenda mjue ilivyo vigumu kuishi na NCD’s.
“Ikiwa hutapata tiba stahiki unakuwa kwenye hatari ya
kupata magonjwa mengine ya NCD’s hata 3 au 4.
“Ukweli tunahitaji kuifikia jamii na kuielimisha kuhusu
magonjwa haya ili wayaepuke na kuwasaidia pia wale wanaohitaji kupata huduma,”
anasema.
Ruth anasimulia alipata wakati mgumu pia alipokutana na
mgonjwa mmoja wa moyo aliyeshindwa kumudu kununua dawa zake, ilibidi amsaidie
kununua siku hiyo.
“Nilimkuta wodini hakuwa na uwezo nilitoa za kwangu, ni
lazima nchi za Afrika ziimarishe mifumo yake ya upatikanaji wa huduma lakini
pia kupunguza gharama za matibabu,” anasisitiza.
‘PEN-Plus
VOICES’
Arafa anasema kwa upande wa Tanzania inafanya vema katika
kuukabili ugonjwa wa Siko Seli hata kuimarisha huduma za tiba za kibingwa na
bobezi, hatua ambayo ni ya kupongeza.
Anasema pamoja na hayo bado kuna uhitaji mkubwa wa uelimishaji
huku akibainisha kwa sababu ya uelewa duni kumekuwa na muendelezo wa vitendo
vya unyanyapaa kwa wagonjwa ndani ya jamii.
“Sisi tunaishi na magonjwa haya, tunafahamu lugha ya
kuzungumza na jamii zetu na wakatuelewa kwa urahisi zaidi,” anasema.
Hoja ambayo ‘inaungwa mkono’ na Echodu anasisitiza “Ni
muhimu tafiti zikaendelea kufanyika pia ili kuboresha huduma lakini ni muhimu
pia nchi za Afrika zikatuhusisha katika upelekaji elimu.
“Ninyi [wataalamu/watafiti] mnaijua sayansi [ya NCD’s] ila
sisi tunaishi na magonjwa haya, tunaijua safari hii, tushirikisheni …
tukasaidie jamii,” anatoa rai.
Ruth anaongeza “Tunahitaji tuwe sehemu ya kuleta mabadiliko na matokeo chanya kwa Bara la Afrika katika ‘vita’ dhidi ya NCD’s, tushirikishwe lakini si tu kuachwa pembeni na kuletewa kila kitu.
MWANZO IMARAUmoja wa Mataifa [UN] kupitia Malengo Endelevu umedhamiria
kutokomeza NCD’s ifikapo 2030.
Mtafiti mbobezi wa magonjwa ya damu hasa Siko Seli Barani
Afrika Profesa Julie Makani anasema mkutano wa ICPPA umekuwa mwanzo iimara na
madhubuti kwa Bara la Afrika.
“PEN-Plus ni mkakati unaoendana na malengo ya WHO Kanda ya
Afrika, inaiweka nchi za Afrika kwenye nafasi nzuri zaidi katika kupambana na
NCD’s,” anasisitiza.
Anasema mpango huo wa PEN-Plus umeweka msisitizo kwa nchi
za Afrka kuanzisha kliniki za NCD’s hadi katika ngazi ya huduma za afya za
msingi.
Anasema nchi za Afrika zimekuwa zikifanya tafiti nyingi
kuangazia magonjwa hayo ili kusaidia kuboresha huduma za uchunguzi na tiba kwa
raia wake.
“Kupitia mkutano huo imesisitizwa umuhimu wa wataalamu na
watafiti kuzidi kushirikiana katika kukabili magonjwa hayo.
Anatolea mfano Tanzania inaweza kushirikiana na Msumbiji
katika kutoa huduma, Kenya na Uganda na si wataalamu wa nchi moja ‘kujifungia’
milango peke yake.
“Kusema sisi [nchi fulani] tutakaa tu kupambana na Saratani
au Kisukari, uwezekano wa kufikia malengo ni mdogo,” anasisitiza na kuongeza,
“.., umeonesha pia ni muhimu kushirikiana na watu wenye
haya magonjwa, washiriki mapambano haya.
“Kuhakikisha wanajipanga na wanakuwepo kwenye kongamano,
mikutano, mijadala,” anasema na kuongeza,
“Ni muhimu
kuhakikisha wanashiriki tafiti, kushauri huduma zinakuwaje na hata kwenye
kuongea na viongozi na jamii ili tuweze kwenda mbele zaidi.
Chapisha Maoni