moja

Responsive Advertisement

 Arusha

Jopo la wanaharakati 25 wa masuala yanayoangazia ugonjwa wa Siko Seli, kutoka mataifa mbalimbali duniani, lipo njiani kuelekea kilele cha Mlima Kilimanjaro. 

Miongoni mwao wapo watafiti nguli, jamaa / marafiki wa mashujaa wa Siko Seli, madaktari na viongozi kutoka Biotech.

Licha ya kwamba watafurahi kuupanda mlima huo mrefu zaidi Barani Afrika, safari yao ni ya kipekee na kihistoria, inatoa mchango chanya pia katika utalii tiba, Tanzania.

Hii itasalia alama bora mithili ya mvuto wa theluji iliyopo juu ya kilele cha mlima huo, mashujaa wanaoishi na Siko Seli ni wazi hawataisahau thamani yake ndani ya mioyo yao.

Agenda yao kuu ni kuhamasisha uchangiaji fedha ambazo zitakwenda kutumika kusaidia kuokoa uhai kwa watu wanaoishi na Siko Seli Barani Afrika.

Takwimu zinaeleza kila mwaka duniani watoto 300,000 huzaliwa wakiwa Siko Seli huku 75% ni wapo Barani Afrika hasa Ukanda huo wa Kusini mwa Jangwa la Sahara. kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za Kisayansi.

Watafiti wanaeleza kutokana na ukosefu wa mfumo imara wa uchunguzi wa awali na tiba husababisha vifo vya watoto chini ya miaka mitano.

Ikiwa  hatua na juhudi hazitachukuliwa, nchi zilizopo katika Ukanda huo zitaendelea kupoteza 50% hadi 90% ya watoto hao kabla hawajafika umri wa miaka mitano.

Hivyo, nchi zilizopo Ukanda huo ndizo zimewekwa kipaumbele katika mpango huu kukwea kilele cha Mlima Kilimanjaro, kwa awamu ya sasa.

"Tumekusudia kukusanya kiasi cha Dola za Kimarekani Mil. 1.2 [sawa na Tsh. Bil. 3.27]  kusaidia nchi hizo," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Sickle Forward la Marekani Dkt. Allan Anderson.

Amebainisha fedha hizo zitapelekwa ili kusaidia kuongeza utambuzi wa mapema kwa watoto wachanga.

Amesema fedha hizo zitatumika pia kusaidia vitendanishi vya uchunguzi kwa watoto wachanga na wadogo, katika nchi hizo.

Amesema hatua hiyo itaibua mapema waliozaliwa wakiwa wamerithi vinasaba vya ugonjwa huo wataanza matibabu mapema hivyo kuokoa maisha.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopo Ukanda huo wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na ambazo zina idadi kubwa ya wagonjwa wa Siko Seli Afrika.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaeleza kila mwaka kuna watoto 8,000 hadi 11,000 wanaozaliwa na ugonjwa huo, Tanzania.

Wizara hiyo inaeleza Siko Seli ni miongoni mwa magonjwa yanatajwa kuchangia idadi kubwa ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano.

"70% hadi 90% ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu hufariki dunia kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano," amesema Mtendaji Mkuu wa Tanzania Sickle Cell Disease Alliance Dkt. Deogratius Soka.

Watafiti wa masuala ya magonjwa ya damu wanasisitiza uchunguzi wa mapema wa hali za vinasaba ni muhimu na lazima ili kuvunja mduara wa ugonjwa huo.

Hatua hiyo inapaswa kutekelezwa kabla ya mtu/wenza kuamua kuanza kupata mtoto/watoto.

"Tumekuwa tukienda kwa jamii kupeleka elimu ya kufanya uchunguzi wa mapema," amesema Mkurugenzi wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Siko Seli Tanzania Arafa Said.

Amesema huko huwapatia watu taarifa sahihi kuhusu Siko Seli ili pia kutokomeza unyanyapaa uliopo ndani ya jamii dhidi ya watu wanaoishi na ugonjwa huo.

Amesema kitendo cha wanaharakati hao kukwea mlima Kilimanjaro kinazidi kuongeza nguvu ya ziada katika mapambano dhidi ya Siko Seli.

"Kwa sababu lengo ni kuhakikisha wanaongeza uelewa pamoja na upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa wenye Siko Seli," amesema.

Ameongeza "Tunajua changamoto tunazopitia, tunaziishi kila siku katika maisha yetu.

"Ndiyo maana ifikapo Septemba, kila mwaka tunautumia mwezi mzima kuifikia jamii na kuielimisha kwa namna mbalimbali ili iwe na uelewa sahihi," amesisitiza.

Safari hiyo ya kuelekea kilele cha Mlima Kilimanjaro ilianza Septemba 11, 2024 na inatarajiwa waliokwenda, watarejea Septemba 17, 2024.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement