moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema - Dar es Salaam 

Ni heshima kubwa na historia ya kipekee, hatua ya Wakfu wa Merck Foundation kuiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 11 unao waleta pamoja mabalozi wake kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mkutano huo wa aina yake katika sekta ya afya unatarajiwa kufanyika kwa siku mbili [Oktoba 29 na 30, 2024] Dar es Salaam.

Unatarajiwa kufunguliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, utahudhuriwa na washiriki wapatao 600 hawa watakuja moja kwa moja Tanzania.

Tayari wenza wa marais kutoka nchi 22 za Afrika ambao ni mabalozi wa juu wa Merck Foundation wamethibitisha ushiriki wao.

Washiriki wengine ni wataalamu na watafiti nguli katika sekta ya afya, mabalozi wanaowakilisha nchi ambazo wenza wa marais wanatoka, watunga sera na waandishi wa habari. 

"Tumeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu kwani tumevutiwa mno na uwekezaji mkubwa uliofanywa  na Serikali katika sekta ya afya,".

Yameelezwa hayo na Mtendaji Mkuu wa Merck Foundation Dkt. Rasha Kelej mapema leo katika mkutano maalum na waandishi wa habari.

Ameongeza "Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mfano wa kuigwa, ndiyo maana hatujasita kuja Tanzania.

Amesema kwa miaka mingi Merck Foundation imekuwa ikishirikiana bega kwa bega na Tanzania hasa katika kufadhili masomo kwa wataalamu wa sekta ya afya.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ametaja nchi ambazo wenza wa marais wamethibitisha kuhudhuria mkutano huo.

"Ni kutoka Angola, Botswana, Burundi, Cape Verde, Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo [DRC], Gambia, Ghana na Kenya.

Ametaja nyingine ni "Liberia, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Nigeria, Sao Tome, Principe, Rwanda na Siera Leone.

"Afrika Kusini, Comoro, Eswatini, Zambia, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania ambapo tutawakilishwa na Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariam Mwinyi.

Amesema mkutano huo utahudhuriwa pia na mawaziri wa afya, jinsia, mawasiliano, elimu, ustawi wa jamii kutoka nchi zilizoalikwa.

"Wajumbe 45 wataalamu watakaoambatana na wenza wa marais kutoka nchi hizo, wataalamu wa afya 500, wasomi, watunga sera na waandishi wa habari.

Ameongeza "Mabalozi wanaowakilisha nchi ambazo wenza wa marais wamealikwa na mabalozi wa Tanzania kutoka nchi hizo pia watahudhuria mkutano huo.

"Wajumbe wengine takriban 500 kutoka sehemu mbalimbali duniani watashiriki mkutano huo kwa njia ya mtandao," amesema.

Amesema mkutano huo unatarajiwa utafungua njia ya utekelezaji wa ahadi mpya zitakazotolewa na wenza wa marais, mawazidi na timu ya Merck Foundation.

"Ni katika kuhakikisha upatikanaji wa suluhu bora na usawa wa huduma za afya na watu wa Afrika hasa kutoka nchi zitakazokuwepo katika mkutano huu, ikiwamo Tanzania.

Amesema mkutano utatumika kama jukwaa la kuchukua hatua mahususi katika kushughulikia unyanyapaa na mtazamo wa kijamii wa utasa.

"Kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi salama iliyodhibitiwa na yenye ufanisi kwa wanawake na wasichana," amesema.

Amesema washiriki watanufaika na maarifa na uzoefu unaotolewa na wataalamu mbalimbali na watafiti ambao watazungumza kwa kina mada zitakazowasilishwa.

Nchi zingine ambazo mkutano wa namna hiyo umefanyika kwa awamu zilizopita ni pamoja na Ujerumani, Kenya, Cote d'Ivoire, Misri na Mauritius.

Mkutano huo pia umekwisha fanyika katika nchi za Senegal, Ghana, Zambia, Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na India.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement