Na Veronica Mrema
Sampuli ya
bangi aina ya skanka imepelekwa maabara ili kuchunguzwa kwa kina zaidi kujua
haswa ndani yake kuna kemikali gani nyinginezo zinazochanganywa na je athari
zake ni zipi?.
Ni bangi
ambayo ripoti za awali zinaeleza ina kiwango kikubwa mno cha kemikali yenye
sumu aina ya Tetrahyrocannainol [THC] ambayo huharibu mfumo wa fahamu na akili
ya binadamu.
THC inatajwa
pia kusababisha magonjwa yasiyoambukiza [NCD’S] kama ya moyo na figo.
Wajawazito wanapotumia huenda kuathiri kiumbe kilichopo tumboni ikiwamo kuvuruga kabisa maendeleo ya ubongo wa mtoto.
Kemikali
hiyo huweza kusababisha pia mtoto kuzaliwa na uzito pungufu, kabla ya wakati
wake kutimia.
Wakemia wa
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya [DCEA] wanashirikiana kwa ukaribu
na wenzao wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali [GCLA] kuichunguza Skanka.
Tanzania imeamua
kufanyia uchunguzi zaidi kwa bangi hiyo baada ya kumtia nguvuni mhalifu kinara
wa usafirishaji na uingizaji wa bangi hiyo nchini akiwa na kiasi cha kilogramu
1,815.
Hiyo ni sawa na shehena ya tani 1.8, zilizokamatwa katika oparesheni iliyofanyika Agosti 28, 2024 hadi Septemba 2, 2024 huko Luguruni Mbezi na Magomeni Jijini Dar es Salaam.
Jumla ya watuhumiwa
watano tayari wamekamatwa kwa dawa hizo, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo
amebainisha hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari.
“Wametueleza huko wanakozitoa, kuna maeneo wanakozisindika,”
amesema na kuongeza ..,
“Wanazitoa nchi
nyingine wanazileta nchi zingine wanasindika halafu zinafungashwa, zinaletwa
hapa nchini.
“Baada ya kuwakamata tumeshawasiliana na hizo nchi husika, katika hayo maeneo ambayo wanashirikiana nayo katika kuleta dawa za kulevya nchini,” amesema.
Amesema kwa kuwa
bado wanawatafuta hao wahalifu wengine wanashirikiana kwa ukaribu na nchi
zilizotajwa na wahalifu hao hivyo hawatazitaja hadharani hivi sasa.
“Kwa sababu
kulingana na taarifa tulizopata, zinatengenezwa kwengine, zinaletwa nchi
nyingine kama bangi ambako kuna viwanda vidogo vodogo zinatengenezwa hizo
skanka.
“Ndiyo maana tunafanya uchunguzi wa kimaabara, kule inakozalishwa oparesheni zinaendelea, ili kubaini pia hizo viwanda,” amesema.
Amewataja
waliokamatwa “Ni Richard Henry Mwanri [47] mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi
Makonde, Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam.
“Felister
Henry Mwanri [70] mkazi wa Luguruni Mbezi pia ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa
dawa hizo za kulevya.
“Watuhumiwa wengine ni Athumani Koja Mohamed [58] mfanyabiashara na mkazi wa Tanga, Omary Chande Mohamed [32] dereva bajaji na mkazi wa Buza Dar es Salaam.
“Juma Abdallah
Chapa [36] mkazi wa Kiwalani Dar es Salaam [zimekamatwa pia] gari aina ya
Mitshubishi Pajero yenye namba T 551 CAB na bajaji yenye namba MC 844 CZV.
Aina hiyo ya bangi inayoshika kasi biashara na
matumizi yake haitengenezwi nchini Tanzania.
Upo mnyororo
mkubwa wa biashara hiyo ukihusisha mataifa mbalimbali ambako huzalishwa,
huchakatwa na kisha kusafirishwa kuletwa Tanzania.
Amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo “Haitengenezwi Tanzania, zinatengenezwa nje baadae zinasafirishwa kimagendo, kwa njia za panya kuingiza nchini.
“Ndiyo
[maana] tunataka sasa tuone, kwenye ule mchanganyiko labda kama kuna kemikali
nyingine wanazoweka ili kuleta athari hasa katika mfumo wa fahamu.
“Baada ya
kusindikizwa inakuwa na kiwango kikubwa cha THC, Mamlaka ina ‘divisheni’ ya
sayansi jinai, ambayo inashughulika na masuala ya kimaabara ni wakemia.
“Ili kujua
viwango, athari pia na kemikali ambazo zinakuwa kwenye dawa mbalimbali za
kulevya ambazo tunazikamata wanachunguza.
“[Hivyo] matokeo yatakapopatikana, tutajulisha Umma kuhusiana na hilo suala,” amesisitiza.
Ameongeza “Viwango
halisi vya hizi skanka ambazo zinawekwa na hawa wafanyabiashara.
“Kwa sababu
hivi viwango vya kemikali wanavyoweka ni kwa ajili ya kufanya watu wawe waraibu
lakini pia wawe wategemezi yaani unavyotumia uwe na hamu na usiweze kuacha.
“Sheria yetu
hadi sasa hairuhusu uzalishaji wala usambazaji wa bangi hata nchi zilizoruhusu
nazo zimejiwekea masharti si kwamba ikilimwa isambazwe mtaani kuna masharti
yake.
Ripoti ya Shirika
la Umoja wa Mataifa UNDC kuhusu hali ya dawa za kulevya duniani inaonesha jinsi
baadhi ya maeneo ambako zimeruhusu matumizi ya bangi, hali haipo shwari hivi
sasa.
“Kiwango cha matumizi kimeongezeka duniani, walikoruhusu kulima matatizo ya akili na watu kujaribu kujiua, imeongezeka katika maeneo hayo.
Ameongeza “Taarifa
za matumizi ya dawa za kulevya zinaonesha pia uhalifu umeongezeka katika maeneo
hayo.
“Pengine faida
ya kuruhusu haya mambo inaweza ikawa ni ndogo kuliko hasara, kwamba hasara ni
kubwa kuliko faida.
“Unaweza ukapata
fedha lakini ile fedha ukaitumia katika kudhibiti uhalifu zaidi, unajikuta
unatoa hapa unaweka hapa.
“Ndiyo maana sisi Tanzania Serikali haijaruhusu kilimo, wala biashara wala matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini.
Chapisha Maoni