Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
 
NI takriban mwezi mmoja sasa umepita tangu Rais Dk. John Magufuli alipotangaza kupiga marufuku vijana kuonekana wakicheza mchezo wa ‘pool table’ wakati wa saa za kazi.

Agizo hilo Rais Magufuli alilitoa Machi 16, mwaka huu Ikulu jijini Dar es Salaam punde tu baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa 26.

“Niwaombe wakuu wa mikoa kusimamia maeneo yenu, watu hasa vijana wafanye kazi. Haiwezekani nchi hii kijana acheze ‘pool table’ asubuhi halafu huko mashambani wanaolima ni wazee na akina mama. Kama wamezoea kucheza washikeni na wapelekeni katika makambi wakalime kwa nguvu na wakitoka watakuwa wameshaelewa kwamba asiyefanya kazi na asile,” aliagiza.

Kabla ya agizo hilo la Rais Magufuli ilikuwa ni jambo la kawaida kuwaona vijana wakiwa wamejazana kuzunguka meza za mchezo huo wa kubahatisha kuanzia asubuhi hadi jioni hususan kwenye maeneo ya starehe ikiwamo ‘bar’.

Lakini baada ya agizo hilo hali imekuwa tofauti kwani ni nadra sasa kukuta vijana wakiwa wamejazana kwenye maeneo hayo katika saa za kazi kucheza mchezo huo wakati wengine wakiwajibika.


Ni katika hali hiyo MTANZANIA liliamua kufuatilia zaidi ili kujua namna ambavyo wamiliki wa biashara hiyo wanavyoendesha biashara yao hiyo hivi sasa baada ya kutolewa kwa agizo lile la Rais Magufuli.


Kauli yao

Mmoja wa wafanyabiashara Donald Kavishe ambaye ni Meneja wa bar maarufu ya Lubumbashi iliyoko Mbezi Mwisho jijini hapa.

Kavishe anasema tangu Rais Magufuli alipotoa agizo biashara yake imekuwa ngumu kila kukicha tofauti na hapo awali.

“Biashara imekuwa ngumu dada...  Kabla ya agizo lile nilikuwa na uwezo wa kukusanya Sh 20,000 hadi 25,000 kila siku lakini sasa nakusanya Sh 7,000 hadi 8,000 mara chache sana kupata angalau Sh 10,000,” anasema.

Anasema fedha hizo ni zile ambazo hutolewa ndani ya meza hiyo wakati wa kufunga bar ambazo kila mchezo hulazimika kutumbukiza ndani ili kupata 'coin'  (vipira vya mchezo.

“Si kwamba tunakusanya fedha hizo,  bali kila mchezaji hutakiwa kutumbukiza Sh 200 ndani ya meza ili vile vipira vya mchezo vitoke,” anasema.

Anasema idadi kubwa ya wateja wake ni madereva wa boda boda, bajaji na wale wanaoleta mizigo kutoka mikoani.

“Kama unavyoona bar yangu ipo karibu na kituo cha bodaboda na bajaji...  Vijana wale walikuwa wanapenda kuja kuvheza pool table hapa kwangu wakati wakisubiri foleni ya kupakia abiria ifike.

“Lakini pia hapa jirani kuna soko hivyo wale madereva wanaoleta mizigo kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wanakuja hapa kucheza na kupata viburudisho wakati madalali walipokuwa wakishusha mizigo hiyo, lakini hivi sasa hawaji,” anasema.

Kavishe anasema hali hiyo imechangia pia kushuka kwa mauzo ya bidhaa nyingine.

“tunalazimika kuuza supu, maji na soda kuanzia asubuhi hadi saa kumi muda ambao Rais alisema.....  Mauzo yangu yamepungua nilikuwa kwa siku naweza kuuza Sh 700,000 hadi Sh 800,000 lakini siku hizi nauza Sh 300,000 hadi 400,000.

“Hali ni mbaya kwa kweli, nina wafanyakazi wanane ambao natakiwa kuwalipa mshahara najaribu kutafakari ingekuwaje kama na sehemu ya biashara ningekuwa nailipia huenda ningefunga kabisa ila kwa bahati nzuri eneo hili la biashara ni langu mwenyewe,” anasema.

Anasema wanalalamika kuuza vinywaji laini pekee kwani maofisa afya wa serikali ya mtaa wa kata ya Mbezi Luis pamoja na askari hupita kukagua na iwapo mtu atakutwa akiwa amelewa saa za kazi hutozwa faini. 

“Faini hiyo ni Sh 50,000 ambapo yule aliyelewa hutakiwa kulipia lakini na yule aliyemuuzia kilevi hutozwa Sh 50,000 sasa fikiria akikutwa wamelewa zaidi ya mtu mmoja utatozwa Sh ngapi,” anahoji.

Kavishe anaiomba serikali iwaruhusu angalau kuuza bia moja hadi mbili kwani wapo wateja wengine huhitaji ili kutuliza mawazo.

“ kwa mfano wenzetu ambao shughuli zao ni za ulinzi wale saa yao ya kazi ni usiku lakini akija tunaogopa kuwauzia tusije tukapigwa faini ,” anasema.

Naye Asha Hashim ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa ‘Pub’ maarufu ya Kwa Mkwere iliyoko Manzese jijini hapa anasema  ingawa biashara yao ya bar na mgahawa haijatetereka hata hivyo wanapata hasara upande huo wa biashara ya pool table.

“Biashara inaendelea vizuri kama kawaida labda pengine kwa sababu tupo sehemu ambayo ina watu wengi huwa tunauza na chakula lakini kwa upande wa pool table tunataka hasara awali tulikuwa tunapata kuanzia  Sh 20,000 leo hii baada ya agizo lile tunapata mara nyingi 8,000 na mara chache 10,000,” anasema.

Wasemavyo vijana

Fred Halla ni mmoja wa Vijana ambaye anavutiwa na mchezo huo wa pool table anasema alianza kucheza mchezo huo tangu mwaka 1998.

“Wakati huo nilikuwa nikifanya kazi kwenye kampuni iliyokuwa ikchapisha gazeti fulani ofisi zetu zilikuwa huko Mnazi mmoja Posta jijini hapa,  tulikuwa tunakwenda hoteli ya 'continental'  kucheza wakati huo uliitwa smoka....  Unafanana sana na pool table tofauti yake ni sheria Tu,” anasema.

Halla anasema ingawa agizo la serikali lililenga nia nzuri ya kuwataka vijana kujishughulisha kiuchumi hata hivyo limewabagua.

“ Rais Magufuli ameagiza bar zifunguliwe saa 10 baada ya kazi lakini wengi wanajua asubuhi hadi jioni ndio muda wa kazi jambo ambalo si kweli kwa sababu wapo wenzetu walinzi ambao tunajua muda wao wa kazi ni jioni hadi asubuhi.

“Kwa maana hii basi binafsi naona agizo lile lina mapungufu kwa sababu kuna matabaka mengi ya wafanyakazi na lazima wapewe haki kwa usawa,” anasema.

Anasema ingefaa zaidi kabla serikali haijatoa agizo lile ingefanya utafiti kujua namna hali halisi ilivyo na si kupiga marufuku pekee kwa hali hii ni wazi wanaofanya kazi usiku hasa walinzi hawatambuliki kisheria.

“ Kwa mfano mimi nipo likizo sasa hivi huwezi kusema sifanyi kazi. Wanasema watakaokamatwa wakicheza wakamatwe wakalime hii siafikiani nayo ni vyema serikali ikawafanya vijana wapende kilimo lakini si kwa kuwalazimisha wataona kilimo ni sawa na adhabu.

“Naamini kwamba leo hii serikali kwa mfano ikisema inagawa mashamba ya kilimo sidhani kama kuna kijana atakaa pembeni badala ya kujitokeza kupatiwa eneo la kulima.

“Pale ninapoishi kuna kituo cha bodaboda na bajaji nilitaka nifungue kijiwe changu cha pool table ili wakati wakisubiri abiria 'wa-reflash mind' ambapo ningeajiri kijana mmoja asimamie lakini imebidi nighairishe mpango wangu huo,” anasema.

Naye Juma Karim anasema agizo la Rais Magufuli limemfanya kuwa muoga wa kusogelea meza za mchezo huo na kwamba siku hizi zinaweza kupita hata siku mbili hajaucheza.

“ Aisee ninaogopa kubebwa 'msobe msobe'  kwenda kulima, nimeshazoea biashara yangu ya bajaji hivyo ni bora nitii amri ya serikali,  anasema Karim.

Anasema vijana wengi wanasikitishwa na agizo hilo kwani wakiwa kwenye vijiwe waliweza kukutana na wenzao wa sehemu mbalimbali na kupeana mipango ya kazi.

“Yaani kwa mfano kijana anakuja kwenye pool table hana kazi lakini pale kwa kuwa mpo wengi anaweza kuja mwenzenu na kuwajulisha kutakuwa na kazi labda ya kumwaga zege mahali au kushusha mzigo sokoni hivyo kijana anajikuta akinufaika mwisho wa siku,” anasema.

Naye Mussa Sanga anasema kwa jinsi walivyojawa na hofu ya kukamatwa kupelekwa kulima vijana wengi wasiokuwa na kazi huona heri wakae nyumbani  wapumzike.

“Wengi wanaona bora walale nyumbani maana ajira hawana huko walikuwa wanakwenda kubadilishana mawazo wafanye nini watoke kimaisha,”  anasema

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement