Ijumaa, 19 Januari 2018

WAGONJWA WA MOYO HAWATUMII DAWA WALIZOANDIKIWA IPASAVYO - UTAFITI

*Matokeo yabainisha sababu.

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

MAGONJWA yasiyo kuwa ya kuambukiza (NCD’s) ni yale ambayo mtu anapoyapata huwa hawezi kumwambukiza mwingine na ataishi nayo hadi siku atakapofariki dunia.

Kundi hilo linajumuisha magonjwa ya saratani, magonjwa ya moyo, magonjwa sugu ya njia ya hewa, seli mundu (sickle cell disease), magonjwa ya akili na dawa za kulevya, figo, kisukari, ubongo, macho na mengineyo.

Utafiti uliofanywa mwaka 2005 duniani na Shirika la Afya Duniani (WHO) ulionesha kati ya vifo milioni 58 vilivyokuwa vimetokea, vifo milioni 35 vilitokana na magonjwa yasiyo kuwa ya kuambukiza.

Nchini Tanzania utafiti uliofanyika katika wilaya nne kuanzia mwaka 1994 hadi 2002 ulionesha asilimia 18 hadi24 ya vifo vilivyokuwa vimetokea, vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Magonjwa hayo yanatajwa kuchangia asilimia 27 ya vifo vyote duniani na tafiti zinaonesha yanazidi kuongezeka hasa katika nchi zilizopo chini ya Ukanda wa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.

WHO linakadiria kuwa asilimia 20 ya vifo vyote vilivyotokea nchini mwaka 2005 vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Utafiti huo unabainisha magonjwa ya moyo yalichangia vifo kwa asilimia tisa, saratani asilimia nne, mfumo wa hewa asilimia mbili, kisukari asilimia moa na magonjwa mengine sugu asilimia nne.

Utafiti wa viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) mwaka 2012 ulionyesha kuna ongezeko kubwa la viashiria vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Serikali za nchi mbalimbali sasa zimeelekeza nguvu zake katika kufanya kampeni kuelimisha jamii kuhusu magonjwa hayo ambayo yanatajwa kugharimu maisha ya watu wengi.

Magonjwa hayo yanaweza kuepukika kwa watu kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara, matumizi yanayostahili ya dawa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Changamoto kubwa inayotajwa katika kukabili magonjwa haya ni gharama kubwa za matibabu ambazo mtu hukabiliana nazo hasa pale anapokuwa hana bima ya afya.

Mgonjwa

Hamis Ibrahim Mkazi wa Singida anamuuguza mtoto wake ambaye amefanyiwa upasuaji katika taasisi hiyo hivi karibuni.

“Mwanangu aligundulika kuwa na tatizo la moyo mwaka 2004 kabla ya kufika hapa nilizunguka hospitali nyingi mno lakini tatizo halikugundulika.

“Hadi pale nilipokwenda katika hospitali moja ya rufaa ipo huko Manyoni ndiko ikagundulika kwamba ana tatizo,  ‘valve’ zake zilikuwa zina-fail kusukuma damu na moyo wake ulionekana kuwa unatanuka,” anasema.

Anasema awali ilimgharimu fedha nyingi kulipia matibabu ya mtoto wake huyo ikafika wakati akashindwa kumudu gharama hizo.

“Nilikuwa natumia hadi zaidi ya Sh 200,000 kila nilipomleka  kufanyiwa uchunguzi pamoja na dawa, nikashauriwa kukata bima nikakata toto afya ya NHIF ambayo kidogo naona inanipunguzia mzigo wa gharama za matibabu,” anasema.

Anaongeza  “Nashukuru serikali naiomba isogeze huduma hizi karibu zaidi na jamii wawasaidie wanaougua ugonjwa huu wapo mikoani pia wengine hawawei kuja huku, ikiwezekana kila mkoa upate haya matibabu.

Utafiti

Pedro Pallangyo ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye hivi karibuni amefanya utafiti kujua hali halisi na changamoto zinazowakabili wagonjwa wa moyo nchini.

MTANZANIA limefanya naye mahojiano na anaeleza kwa kina kile alichokibaini kupitia utafiti wake huo, karibu.

Dk. Pallangyo anasema kwa kawaida wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo hupatiwa dawa zinazostahili kutibu magonjwa ya moyo yanayowakabili.

“Lakini kati yao wapo ambao wanaporuhusiwa kurejea nyumbani hushindwa kununua dawa wanazokuwa wameandikiwa na madaktari wanazotakiwa kuzitumia  kipindi chote wanapokuwa nyumbani kabla ya kurejea tena hospitalini,” anasema.

Anaongeza “Matokeo yake, kama wana tatizo la moyo kushindwa kufanya kazi, wakilazwa hospitalini huwa na hali nzuri lakini wakirudi nyumbani hali hubadilika na kuwa mbaya kuliko awali kwa sababu hawatumii dawa.

“Kutokana na hali hiyo wengi hurudishwa hospitalini, kwa kipindi cha miezi sita tulifanya utafiti huu kwa wagonjwa 459 kuangalia mwenendo wao wa matumizi ya dawa na mambo mengineyo,” anasema.
Dk. Pedro (anayezungumza pichani) anasema utafiti huo ulihusisha wagonjwa waliokuwa na umri wa kati ya miaka 46 na kuendelea na kwamba silimia 57 walikuwa wanawake huku asilimia 43 ikiwa ni wanaume.

“Kati ya wagonjwa hao asilimia 22 walikuwa na bima ya afya  na asilimia 68 walikuwa wakiishi katika maeneo ya mijini,” anasema.

Matokeo

Dk. Pallangyo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa JKCI anasema katika utafiti huo walibaini asilimia 80 ya wagonjwa wote 459 waliofanyiwa utafiti huo walikuwa na matumizi mabaya ya dawa.

“Hawakutumia dawa kama inavyotakiwa na walivyokuwa wameelekezwa na wataalamu na hiyo ilikuwa kisababishi kikubwa kilichochangia kulazwa mara kwa mara na kuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha,” anasema.

Daktari huyo anasema matokeo ya utafiti huo yalibainisha kwamba asilimia 85 ya wagonjwa waliohojiwa walieleza sababu kubwa iliyowapelekea kuacha kuzingatia matumizi ya dawa ni kukosa fedha za kununulia dawa hizo.

“Sababu nyingine ambayo ilitajwa na kushika nafasi ya pili ilikuwa ni usahaulifu, baadhi ya wagonjwa walieleza kwamba kuna wakati walisahau kumeza dawa walizoandikiwa,” anasema.

Anasema walitumia tool ya Morsw (kipimo cha kitaalamu) kinachoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kufanya tafiti za namna hiyo.

Sababu

Anasema sababu kubwa ambayo imeonekana kuchangia hali hiyo ni gharama za ununuzi wa dawa hizo ambapo utafiti unaonesha asilimia 87.3 ya wagonjwa waliohojiwa walieleza sababu hiyo.

“Kuhusu usahaulifu ilipatikana asilimia 53.9… utaona matokeo haya hayawezi kuleta jumla ya asilimia 100 na hii ni kwa sababu katika wagonjwa tuliohoji wengine walikuwa na sababu zaidi ya moja,” anasema.

Dk. Pallangyo anasema kati ya wagonjwa waliohojiwa asilimia 34.4 walieleza kuwa waliacha matumizi ya dawa kutokana na wingi wa dawa walizokuwa wameandikiwa kwa ajili ya kuzitumia kutibu tatizo walilonalo.

“Yaani kutokana na ule wingi walilazimika kuacha baadhi ya kupunguza au kupumzika, na asilimia 26 waliacha matumizi ya dawa kutokana na uzembe,” anasema.

Anasema kwa kupata matokeo hayo walijaribu kuangalia kwa kina nini hasa vilikuwa visababishi vilivyochangia wagonjwa hao kuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa walizotakiwa kutumia.
“Tulibaini umri haukuwa tatizo, jinsi haikuwa tatizo lakini kwa upande wa elimu tulibaini kulikuwa na tatizo, wagonjwa waliokuwa na elimu ndogo (Elimu ya Msingi kushuka chini) walikuwa na uzingatiaji mdogo kulinganisha na wagonjwa waliokuwa na kiwango cha Elimu ya Msingi na kuendelea,” anasema.

Anasema kwa upande wa kigezo cha ajira nacho kilikuwa ni sababu kwani utafiti ulibaini wale waliokuwa hawana ajira ya kuwaingizia kipato walikuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa kuliko waliokuwa na ajira ya kueleweka.

Anasema kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo wagonjwa waliokuwa wanaishi katika maeneo ya vijijini tulibaini walikuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa kulinganisha na wale waliokuwa wakiishi mijini.

Anaongeza “Aidha, wagonjwa ambao hawakuwa na bima walikuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa mara nane zaidi ya wale ambao walikuwa na bima.

“Hivyo vigezo vya msingi ambavyo tuliona vilichangia hali hiyo, ni elimu duni, tatizo la ajira, makazi wanakoishi na kutokuwa na bima afya,” anabainisha Daktari huyo ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya watafiti vijana Barani Afrika kwa mwaka 2017.

Hali mbaya

Dk. Pallangyo anasema katika utafiti huo walienda mbali zaidi na kuangalia maendeleo ya wagonjwa waliolazwa mara kadhaa baada ya mahojiano ya awali.

“Tulibaini baada ya mahojiano ya awali, wagonjwa ambao  hawazingatii matumizi ya dawa kama walivyotakiwa wana uwezekano wa kulazwa mara kwa mara huwa ni asilimia 70 kuliko wale ambao huzingatia,” anasema.

Anaongeza “Matokeo yanaonesha pia wagonjwa ambao huwa na uzingatiaji mbaya wa matumizi ya dawa hali inayopelekea kulazwa mara kwa mara hospitalini wapo kwenye hatari ya kufariki dunia mara tatu zaidi ya wale wanaozingatia matumizi sahihi ya dawa.

“Hii tuliibaini baada ya kuwafuatilia kwa ukaribu wagonjwa hao ambapo kati yao walikuwapo ambao walipoteza maisha ndani ya miezi sita ya utafiti huu,” anasema.

Dk. Pallangyo anasema kutokana na matokeo ya utafiti huo inawezekana sababu hizo zinachangia pia vifo vya wagonjwa kwa kutozingatia matumizi sahihi ya dawa katika magonjwa mengine.
Madaktari wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Apolo, India wakishirikiana kumfanyia upasuaji mgonjwa wa moyo kwa kumuwekea milango miwili ya moyo ya chuma

Umasikini huchangia?

“Huenda hii inatokea kwa sababu, jamii nyingi bado ni masikini, kusema ule ukweli bado wananchi hawawezi kumudu gharama  za kutibu magonjwa yasiyo kuwa ya kuambukiza,” anabainisha.

“Ukicha matokeo ya utafiti huu, sasa hivi tunafanya utafiti mwingine ambapo tayari tumehoji wagonjwa 500 na lengo ni kuwafikia 1,000 tukiangazia hasa kigezo hiki cha gharama na hali ya kipato cha mwananchi.

“Tunatarajia kukamilisha utafiti huu na kutoa matokeo yake ifikapo Januari, mwakani, lakini kwa kuzingatia utafiti huu tuliokamilisha, tunaishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwamba lazima watafute mbinu ama njia mbalimbali kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na bima ya afya.

“Ifike mahali bima ya afya iwe ni haki ya msingi kwa kila mwananchi badala ya wachache tu kuwa nayo, maana kwa matokeo haya inaonesha wazi kwamba mtu akiwa na bima ya afya anakuwa hana ‘stress’ za jinsi gani atamudu gharama za matibabu na dawa,” anasema.

Dk. Pallangyo anaongeza “Lakini pia itafakari jinsi gani kila mwananchi atakayekata bima ya afya atakuwa analipa kwa sababu sisi wafanyakazi tunakatwa kwenye mshahara lakini kuna kundi la watu ambao wamejiajiri wenyewe katika ajira ambazo si rasmi.

“Tunaona pia kuna haja zaidi ya kuwapatia elimu wananchi kuhusu umuhimu wa kukata bima ya afya na kuzingatia matumizi ya dawa kulingana na walivyoelekezwa na wataalamu wa afya katika kutibu magonjwa mbalimbali,” anasema Daktari huyo.

SAFARI YA MLOGANZILA NA ATHARI ZAKE SEKTA YA AFYA NCHINI

Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwasaidia wagonjwa kupanda katika gari tayari kwa safari ya kuhamia Hospitali ya Mloganzila hivi karibuni.

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

“Sitaki mnipeleke huko mnapotaka niende, mimi nilikuja hapa Muhimbili kutibiwa kama mmeshindwa bora ndugu zangu wanichukue na kunirudisha nyumbani,”.

Ni kauli ya mmoja wa wagonjwa ambaye alikuwa akisukumwa na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kupelekwa katika gari la wagonjwa tayari kwa safari ya kuhamishiwa kwenda Hospitali ya Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kampasi ya Mloganzila (MAMC) – Mloganzila.

Mgonjwa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, anasema hajui kwanini anahamishwa kwenda huko na anazidi kulalama kwamba arudishwe nyumbani kwake.

“Usijali mama, unapopelekwa (Mloganzila) ni pazuri zaidi ya hapa unapotolewa (Muhimbili), hautakwenda peke yako utakwenda na sisi (wauguzi) tutakuwa pamoja hadi utakapopona na kuruhusiwa kurudi nyumbani,” anaelezwa na Muuguzi mmoja aliyekuwa akisukuma kitanda hicho.

Nashuhudia wagonjwa waume kwa wake wakiendelea kutolewa katika wodi hiyo na kusaidiwa kupanda katika gari aina ya costa yenye namba T 563 CZX tayari kwa safari.

“Humo ndani mnatakiwa kupanda na msaidizi (ndugu) mmoja, hakikisheni kila mmoja amepanda na ndugu yake,” anasema Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Wateja Muhimbili, Aminiel Aligaesha aliyekuwa hapo kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa sawa.

“Mwishoni mwa mwaka jana Rais John Magufuli akizindua MAMC alisema baadhi ya wagonjwa waliolazwa Mwaisela wahamishiwe Mloganzila ili kupunguza msongamano,” anasema.

Anasema Muhimbili walianza kutekeleza agizo hilo mwishoni mwa Desemba, mwaka jana.

“Jengo hili lina vitanda 240 na wakati wote waliolala waliokuwa wapatao 250 hadi 300 unakuta wengine walilala wawili au chini.

“Wagonjwa walikuwa hawapungui humu ndani, na hiyo ndiyo sababu kuu iliyofanya wapunguzwe kutoka hapa kwenda Mloganzila, ndani ya mwezi mmoja tutakuwa tumepeleka wagonjwa wapatao 170,” anasema. 

Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwasaidia wagonjwa kupanda katika gari tayari kwa safari ya kuhamia Hospitali ya Mloganzila hivi karibuni.

Anaongeza “Muhimbili tunashirikiana kwa ukaribu na Mloganzila na tumepanga madaktari wetu zamu kuhakikisha wanakwenda huko kutoa huduma.

“Mloganzila ina vifaa vya kisasa na tunapofanya matengenezo vya kwetu tunasitisha huduma na kuwapeleka Mloganzila wagonjwa, hadi sasa tumewafanyia vipimo wagonjwa wapatao 30 huko.

“Hivyo, niwatoe hofu wagonjwa wanaohamishiwa Mloganzila kwamba hatua hii haitaathiri matibabu yao kwa namna moja au nyingine, watapa huduma zote zinazostahili,” anasisitiza.

Hayo yanajiri nje ya wodi ya Mwaisela Januari 10, mwaka huu saa kumi jioni ambapo nimefika na waandishi wenzangu punde tukitokea MAMC ambako Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alifanya ziara.

Waziri Ummy anasema serikali kupitia Wizara hiyo imehamisha rasmi Idara ya Magonjwa ya Ndani (internal medicine) ya Muhimbili katika kampasi ya Mloganzila (MAMC).

“Kutokana na hatua hiyo, tumeagiza madaktari bingwa 35 wa Idara hiyo kuhamia Mloganzila mara moja pamoja na wagonjwa  wapatao 270 waliolazwa katika idara hiyo kwa matibabu,” anabainisha.

Anasema hospitali hiyo ya MAMC sasa inatoa huduma saa 24 na kwamba ina vifaa vya kisasa vya kutosha na madaktari bingwa wa kutosha.

“Tunahamisha madaktari wote wa Idara hiyo, wauguzi pamoja na wataalamu wengine na kwa hatua hiyo. Naiagiza Muhimbili kuhakikisha wanakarabati jengo la Mwaisela wodi namba mbili hadi saba, wagonjwa watakaobaki huko ni wale walio mahututi,” anasisitiza. 

Waziri Ummy akizungumza jambo na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na hospitali ya MAMC, Profesa Said Abood hivi karibuni alipotembelea MAMC

Uhamisho Mkoani

Waziri Ummy anasema serikali imeanza kuwapangua madaktari bingwa 20 wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwenda katika Hospitali za rufaa za Mikoa.

Kutokana na hatua hiyo anawataka waganga wakuu wa Mikoa na wafawidhi katika Hospitali za Kanda kuanza kuwapeleka wagonjwa wa Magonjwa ya nje Mloganzila na si Muhimbili.

“Tumejipanga kuhakikisha hospitali zote za Mikoa zinakuwa na madaktari bingwa katika kada nane ikiwa ni pamoja na daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake, watoto, Magonjwa ya jumla, masuala ya radiolojia.

“Tumepokea rasmi Hospitali za Mikoa na tumefanya ya kutathimini  miundombinu iliyopo na madaktari bingwa waliopo kwa ajili ya kuanza kuwatawanya,” anabainisha.

Anaongeza “Hospitali ya Muhimbili itabaki kuwa Hospitali ya kibingwa kwa magonjwa yanayohitaji upasuaji, ingawa hivi sasa bado wataendelea pia kushirikiana kutibu pia magonjwa ya ndani.

Athari zake

Katika Kongamano la 49 la Afya Kitaifa na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Rais wa chama hicho, Dk Obadia Nyongole alisema Tanzania inakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa kwa kiwango cha asilimia 82.

Alisema ili kukidhi mahitaji wanahitaji madaktari bingwa 2,453 wa fani mbalimbali hata hivyo waliopo hivi sasa ni 451 pekee ambao wanahudumia nchi nzima.

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA lilihitaji kujua hatua iliyochukuliwa na serikali kuwahamisha madaktari bingwa waliopo Muhimbili, je ina athari gani.

Chama cha Madaktari

Dk Obadia kwanza anaipongeza serikali kwa hatua hiyo hata hivyo anasema suala la kuboresha ni mtambuka na kwamba linategemea vitu vingi.

“Madaktari hawa wanaotolewa Dar es Salaam huko wanapotoka wanaacha uhaba, nchi yetu ina uhaba mkubwa wa madaktari bingwa hivyo suluhu ya kudumu ni kusomesha madaktari bingwa wa kutosha zaidi.

“Kwa hiyo tunaiomba serikali iendelee kusomesha madaktari katika ‘level’ ya ubingwa,” anasisitiza.

Anaongeza “Upatikanaji wa vifaa tiba ni kitu muhimu ambacho nacho lazima kitazamwe na kufanyiwa kazi, ni mapema mno kusema madaktari wamelichuliaje lakini sisi kama chama tulikaa vikao vya ndani na tukalizungumza.

Mdahalo

“ Tuliita mdahalo wa kitaaluma na madaktari waliopo Dar es Salaam,  lakini kwa bahati mbaya kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu kongamano la kitaalamu halitaweza kufanyika.

“Hata hivyo tunaamini madaktari wataendelea kutupa maoni hilo liweze kufanya na kuwa na tija zaidi kwa Taifa na naamini serikali itaendelea kuweka milango wazi ili tuendelee kushauriana zaidi na sisi wanataaluma juu ya njia nzuri zaidi ya kuitumia kuhakikisha kwamba uhamisho huu hauleti sintofahamu kati ya wanataaluma na serikali ilivyopanga. 

Mfano hai

Dk. Nyogole (pichani) anasema wanayo mifano hai wa mwaka 2011/12 kwamba kuna madaktari waliotolewa na kupelekwa kwenye baadhi ya Hospitali za Mikoa hata hivyo walipofika huko mamlaka za ajira zilisema hazina bajeti za mishahara yao.

“Walihamishiwa kule bila wao kuandaliwa kwa hiyo mazingira yakawa si rafiki kwa wale madaktari ikabidi watafute sehemu zingine za kwenda kufanya kazi,” anasema.

Ushauri  

Dk. Obadia anasema ni muhimu wale ambao watawapokea madaktari hao wahakikishe wanakuwa na taarifa sahihi na kuweka mazingira rafiki kwao.

“Sisi ni chama cha kitaaluma tupo tayari kwa majadiliano na serikali, tutawasiliana na mamlaka husika ili kuweza kujadiliana namna gani hilo litafanyika vizuri zaidi liwe na tija kwa Taifa, jamii tunayohudumia na kwa madaktari wenyewe,” anasema

Waziri awatoa hofu

Waziri Ummy anasema madaktari watakaohamishwa, watahimishwa pamoja na viwango vyao vya mishahara waliyokuwa wakipatiwa awali.

“Katika hili niwatoe hofu kabisa, ni kweli pia kwamba tuna uhaba wa madaktari bingwa  lakini tunafundishwa  kuwatawanya wachache waliopo ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za kibingwa.

“Kwa sababu, kwa mfano... daktari bingwa wa wanawake Bugando anaona zaidi ya wagonjwa 20lakini wa Muhimbili anaona wagonjwa watatu na hospitali ya Rufaa ya Tanga hakuna daktari hata mmoja, lazima tuwatawanye waliopo,” anasisitiza.

Hatua zaidi

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na hospitali ya MAMC, Profesa Said Abood anasema hivi sasa kila mwaka chuo Cha Muhas, Bugando vinazalisha madaktari bingwa wapatao 150 hadi 180. 

“Tunatarajia madaktari hao watakaotoka vyuoni watasaidia kukabili uhaba wa madaktari bingwa ulipo hivi sasa nchini,” anasema.

Anasema pamoja na hayo wamejipanga kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wagonjwa wote watakaofika na wale watahamishiwa katika hospitali hiyo kutoka Muhimbili.

“Wagonjwa tutakaokuwa tunatibu ni wale ambao watakuwa hawahitaji huduma za upasuaji, magonjwa hayo kitaalamu huitwa magonjwa ya ndani kama vile malaria, figo, moyo, ngozi na mengineyo,” anasema.

Picha zote na Veronica Romwald

Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka kwenye gazeti la MTANZANIA ambalo pia nalitumikia Januari 18, 2018 

JKCI YAPATIWA NAFASI YA VITANDA 50 JENGO LA WATOTO MNH

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

KILIO cha muda mrefu cha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kuhusu ufinyu wa nafasi ya kulaza wagonjwa hasa watoto wenye matatizo ya moyo, hatimaye kimesikika na kuanza kufanyiwa kazi.

mapema wiki iliyopita kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Masoko, Anna Nkinda taasisi hiyo ilieleza inakabiliwa na ufinyu wa nafasi kwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi na nafasi ya kulaza wagonjwa hasa watoto.

Mapema wiki hii, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameipatia JKCI nafasi ya kuweka vitanda 50 vya wagonjwa.

Uamuzi huo ulitolewa hivi karibuni na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipofanya ziara ya kushtukiza Muhimbili.

Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa agizo alilotoa hivi karibuni kwa hospitali hiyo kuhamisha wagonjwa na Idara yote ya Magonjwa ya ndani kwenda Mloganzila.

Waziri Ummy aliuagiza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuipatia JKCI nafasi hiyo katika jengo la watoto.


"Nimekuja kukagua iwapo agizo nililotoa limetekelezwa, nimefurahi kwamba limetekelezwa na tayari baadhi ya wagonjwa na madaktari 15 na wauguzi zaidi ya 30 wamehamia Mloganzila," alisema na kuongeza

"Kwa hatua hiyo tunakuwa na nafasi pale wodi ya Mwaisela na hapa jengo la watoto," alisema.

Alisema kwa kuwa JKCI inafanya kazi nzuri ya kutibu magonjwa ya Moyo lakini wanakabiliwa na uhaba wa vitanda kwa sababu hawana nafasi Muhimbili ihakikishe inapa nafasi ya kuweka vitanda 50 vya kulaza wagonjwa ndani ya Jengo la Watoto.

Alisema hiyo itawezesha Taasisi hiyo kukabiliana na changamoto hiyo iliyopo hivi sasa.

YAJUE MADHARA YA TATOO ANAYOPATA MWANADAMU

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

TATOO ni michoro ambayo huchorwa sehemu mbalimbali katika mwili wa binadamu, vijana ndilo kundi ambalo hupendelea zaidi kuchora michoro hiyo.

Michoro hiyo hubeba ujumbe mbalimbali kulingana na matakwa ya wale waliojichora.

Juma Kassim kijana mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa Sinza Kijiweni amechora tattoo ya jina la mwenzi wake shingoni mwake.

“Nampenda mpenzi wangu niliamua kuchora tattoo hii shingoni ili kumuonesha jinsi gani nampenda na namthamini,” anasema.

Kassim anasema hakusudii kuja kuifuta tattoo hiyo kamwe katika maisha yake.

“Umesema ikiwa itatokea nikaachana na mpenzi wangu kwamba nitaifuta au la, siwezi kuifuta hata itokee jambo gani, hii nimeichora itakaa milele katika mwili wangu,” anasema.

Maria Elius anasema yeye amechora tattoo kwa kuandika jina la mama yake.

“Mama yangu amefariki mwaka 2013 nilijihisi mpweke mno, baba yangu simjui, sijawahi kumuona… nilielezwa na mama kwamba alimkimbia nikiwa bado sijazaliwa.

“Hivyo, alinikataa nikiwa tumboni mwa mama, nikaishi bila kumjua baba yangu hadi leo, mama alipofariki nilibaki kwa babu yangu, mwaka 2015 nikaamua kuchora tattoo hii,” anasema.

Anasema kila anapoitazama tattoo hiyo aliyoichora katika mkono wake wa kulia anahisi yupo karibu na mama yake.

“Najua si kweli lakini najihisi vizuri pale ninapomkumbuka naitazama tattoo hii najisikia faraja,” anasema.

Daktari

Hivi karibuni MTANZANIA limefanya mahojiano maalum na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Annete Kissongo.

Anasema vijana wengi hupenda kujichora tattoo katika miili yao bila kujua kwamba zinaweza kuwasababishia madhara mbalimbali.

“Kwa kawaida, mtu anapochora ile tattoo mwilini mwake ile rangi huenda moja kwa moja hadi katika sehemu ya ndani ya ngozi iitwayo dermis,” anabainisha.

Athari zake

Anasema tattoo huweza kusababisha magonjwa ya maambukizi hasa ikiwa chombo cha kuchorea kitatumika pasipo kusafishwa vema na kutumiwa na wengi.

“Kile chombo kinachotumika ikiwa kimetumika kwa kundi kubwa la watu, kama wana magonjwa ya maambukizi kwa mfano HIV, homa ya ini na mengineyo huwa inaongeza uwezekano wa kuambukizana magonjwa hayo na mengineyo,” anasema.

Dk. Anette anasema wakati mwingine mtu huweza kupata maambukizi ya bakteria (bacteria infection).
Anaongeza “Ile rangi inayotumika kuchora tattoo inaweza kumsababishia muhusika kupata allege (mzio).

Anasema athari huwa kubwa zaidi kwa muhiska ikiwamo kupata makovu makubwa yasiyokuwa ya kawaida kitaalamu yanaitwa keloids.

“Makovu hayo huwa makubwa kuliko kidonda cha kawaida au mchoro wa kawaida wa tattoo, haya hutokea zaidi kwa watu weusi na huharibu kabisa ule mwonekano wa ngozi ya muhusika,” anabainisha.

Anasema wapo ambao makovu hayo hufika mahali na kuanza kupungua hata hivyo wengi huwa yanaongezeka ukubwa.

Utafiti

Inaelezwa tattoo inaweza kumsababishia muhusika kupata saratani.

Hiram Castillo wa Kituo cha Radiation cha nchini Ufaransa ni miongoni mwa waandishi wa utafiti huo.

Wanasema kwamba kemikali za wino wa tattoo huweza kusafiri katika damu na kukusanyika katika mfumo wa lymph.

Hali hiyo huufanya mwili kuvimba na hivyo kuzuia uwezo wake wa kupambana na maambukizi dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Watafiti hao wanataja kemikali ya titan-dioksaidi ambayo hutumiwa kuunda wino mweupe ni miongoni mwa kemikali zinazoongeza hatari ya mtu kupata saratani.

“Mtu anapotaka kupata tattoo, mara nyingi huwa makini sana katika kuchagua sindano ambazo hazikutumika awali lakini hakuna mtu anayeangalia kemikali ya rangi, lakini utafiti wetu unaonesha wanapaswa kufanya hivyo,” anasema Castillo.

Wanasayansi hao wa Ufaransa na Ujerumani walitumia X-rays na kipimo cha fluorescence kuchunguza chembe ndogo, waliripoti ushahidi mkubwa unaoonesha kwamba wino wa tattoo huzunguka mwili kabla ya kujenga amana (depostis).

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika majarida mbalimbali pamoja na mtandao wa daily mail Septemba 12, mwaka huu.

Zinawatesa vijana

Dk Anette anasema katika kitengo chicho wamekuwa wakipokea vijana wanaohitaji huduma ya kufutwa tattoo walizojichora mwilini.

Anaongeza “Lakini kwa sasa hapa Muhimbili hatuna ‘procedure’ ya kufuta tattoo (Laser surgery) na huwa hazifutiki kirahisi.

“Wanakosa ajira kwa sababu zipo taaluma ambazo hazipokei watu wenye tattoo au makovu,” anasema.