Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Mwandishi Maalum

Ushindi mnono umezidi kuing'arisha zaidi Tanzania katika ramani ya Afrika kwenye tuzo za umahiri wa uandishi wa habari zinazotolewa na Wakfu wa Merck Foundation - Germany.

Tangu mwaka 2017 imekuwa ikiandaa tuzo kwa wanahabari zenye agenda zinazolenga kuimarisha afya ya jamii, kumkomboa mtoto wa kike kielimu, mwanamke na jamii kwa ujumla.

Tanzania ni nchi iliyopata washindi wengi zaidi kwa idadi ya 11 kutoka vyombo mbalimbali vya habari ikiwamo redio, runinga, magazeti na mitandaoni.

Akitangaza washindi wa tuzo hizo [Merck More than A Mother] na [Diabetes and Hypertension] Media Recognation Awards 2023, Mkurugenzi Mkuu Seneta Dkt. Rasha Kelej amewapongeza washindi wote.

Miongoni mwa walioibuka kidedea katika tuzo hizo za mwaka 2023 [Diabetes and Hypertension MRA] kwa mtandaoni ni Mmiliki wa Matukio na Maisha Blog [M24 Tanzania Media] Veronica Mrema.

Tangu mwaka 2017 amekuwa akishiriki tuzo hizo, hii inakuwa mara yake ya tano kutajwa orodha ya washindi [2019 - 23] vipengele cha mshindi wa kwanza, pili na tatu.

Tuzo nyingine alizoshinda ni ile ya More Than a Mother na Stay at Home [During CORONA pandemic] kwa vipengele vya magazeti hadi radio.

Washindi wengine kutoka Tanzania ni Lucy JohnBosco aliyeshinda nafasi ya kwanza [Mwananchi Online] na Tulinagwe Malopa [Gazetini].

Kwa upande wa radio Mwanaisha Makumbuki [Highlands Fm] na upande wa magazeti mshindi ni Christina Mwakangale [Nipashe].

Seneta Rasha amesema waliona umuhimu kuanzisha tuzo ya Diabetes and Hypertension [Kisukari na Shinikizo la Damu] kwani ni magonjwa yanayogharimu uhai wa wengi hivi sasa Barani Afrika.

"Tunahimiza wanahabari kuendelea kuelimisha jamii kuhusu magonjwa haya ili watu wawe na mtindo bora wa maisha, waweze kuyaepuka," amesema.

Tuzo ya More Than a Mother 2023 washindi kutoka Tanzania upande wa magazeti ni Marco Maduhu [Nipashe], Shaban Njia [Nipashe], Beatrice Mukocho [Guardian].

Kwa upande wa radio Adam Hhando [CG Fm], Olga Lungala [Moshi Fm] na mtandaoni ni Aveline Kitomary [Habari Leo].

Seneta Rasha amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kupitia wanahabari wake kusaidia jamii zao kupunguza na kukomesha unyanyapaa kwa waliokosa watoto na ukeketaji.

Amesema bado vina nafasi kubwa pia kukemea na kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii na kusisitiza elimu kwa mtoto wa kike ili kumkomboa mwanamke.

Jumla ya wanahabari 83 wameibuka washindi kwa mwaka 2023 kutoka mataifa 22 ikiwamo Tanzania [11], Ghana [10], Burundi [10], Malawi [8], Kenya [6], Zambia [5], Zimbabwe [4] na Namibia [4].

Nchi nyingine ni Cabo Verde [3], Cameroon [2], DRC [2], Togo [2], Nigeria [2], Uganda [2], Benin [2], Niger [1], Gambia [1], Rwanda [1], Liberia [1], Mali [1] na Mozambique [1].

Washindi wote hao wamejinyakua zawadi ya fedha kuanzia Dola 500 pamoja na medali kutoka kwa Wakfu huo wa Merck Foundation.

Seneta Rasha amesisitiza wataendelea kushirikiana kwa ukaribu na wanahabari ikiwamo kuandaa tuzo hizo na tayari 'pazia' kwa ajili ya ushiriki wa tuzo za 2024 limefunguliwa.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement