Alhamisi, 24 Novemba 2016

FOMU ZA USAJILI WA WAGANGA TIBA ASILI ZAZINDULIWA DAR

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, amezindua fomu ya usajili wa dawa za tiba asili, kundi la pili

TAMKO LA MHESHIMIWA UMMY A. MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO WAKATI WA UZINDUZI WA FOMU YA USAJILI WA DAWA ZA TIBA ASILI, KUNDI LA PILI

Kama mnavyofahamu, Serikali inatambua umuhimu wa Tiba Asili ambayo ni tiba kongwe zaidi nchini, imekuwepo toka enzi na enzi. Pia, watanzania zaidi ya asilimia sitini (60%) wanatumia huduma hii ya Tiba Asili. 

Hivyo, ni muhimu kuhakikisha kuwa inaboreshwa na kuendelezwa ili kupanua wigo wa watumiaji, huku tukiwa na uhakika wa ubora na usalama wa huduma hii. 

Katika kutekeleza hayo, Serikali imerasimisha Tiba Asilia kwa kujumuisha Tiba Asili na tiba Mbadala kwenye Sera ya Afya pamoja na kutunga Sheria.

Ndugu Wananchi,

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lilianzishwa kisheria chini ya Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Na.23 ya Mwaka 2002, kwa lengo la kusimamia, kudhibiti na kuendeleza huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini. Baraza lilizinduliwa rasmi mwaka 2005.


Usajili wa Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, Wasaidizi na vituo vya kutolea huduma ulianza rasmi mwaka 2011. Hadi sasa Baraza limefanikiwa kusajili waganga zaidi ya elfu kumi na nne (14,000) na vituo mia moja na themanini (180). 

Ndugu Wananchi,

Pamoja na mafanikio hayo, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali limeweka mfumo unaoweza kuwasaidia walaji kuhakikisha kuwa wanatumia dawa za asili zilizo salama kwa kuzipima katika maabara zinazotambulika na Serikali. 


Dawa zitakazopimwa zitawawezesha waganga kusajili dawa zao, na hivyo kuwasaidia kufanya kazi kwa kujiamini na kupata soko ndani na nje ya nchi na kuongeza kipato chao binafsi na kwa Taifa.

Ndugu Wananchi,
Usajili wa dawa za tiba asili utategemea vigezo vifuatavyo:


Mtaalamu wa tiba asili lazima awe amesajiliwa kisheria na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na ana leseni ya kufanyia kazi iliyo hai. 


Kituo cha kutolea huduma lazima kiwe kimesajiliwa na kina leseni iliyo hai. Sehemu ya kuzalishia dawa iwe imekaguliwa na kuthibitika kuwa inafaa kwa kuzalishia dawa. 


Mtaalamu wa tiba asili anapaswa kuwasilisha katika Ofisi ya Msajili wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, taarifa sahihi za uchunguzi wa dawa yake kutoka katika taasisi zilizoainishwa katika fomu ya usajili wa dawa.
 

 
Taasisi hizo ni BRELA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Chakula na Lishe, Maabara ya Taifa ya Afya, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu.

Serikali linawaasa waganga wa tiba asili na tiba mbadala wote kufuata sheria na kuhakikisha kuwa dawa zinaandaliwa kwa ubora na zinasajiliwa kwa mujibu wa sheria ili kuinua tiba asili nchini. Naliagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kusimamia suala hili kikamilifu.

Kwa kusema hayo nazindua rasmi usajili wa dawa za tiba asili leo tarehe 24/11/2016.
Ahsanteni kwa kunisikiliza