Ijumaa, 24 Februari 2017

DAKTARI: ULEVI WA UGORO, PETROL, GUNDI HATARI KULIKO UNGAhttp://4.bp.blogspot.com/_R2m6i0D8GUw/ScjpVTM4sBI/AAAAAAAAB28/VKivordDu6M/s400/5.JPGGundi ya viatu ikiwa kwenye chupa

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MATUMIZI ya ugoro, petrol na gundi yametajwa kuwa mabaya zaidi kulinganisha na dawa za kulevya huku ikielezwa kwamba hakuna dawa maalumu ya kumtibu mwathirika.

Imeripotiwa baadhi ya watu waliokuwa wakitumia dawa za kulevya nchini wamelazimika kugeukia vilevi hivyo ili kuiridhisha miili yao kutokana na kuadimika kwa dawa za kulevya nchini.

Hali hiyo inatokana na vita iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, vita ambayo ilikolevya moto na Rais Dk. John Magufuli ambaye alimteua Kamishna wa kupambana na Dawa za Kulevya ili aendeleze mapambano hayo nchi nzima.

Akizungumza na MTANZANIA jana Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Cassian Nyandindi (pichani) alisema matumizi ya vilevi hivyo viitwavyo kitaalamu inhalants husababisha madhara makubwa kwa binadamu.

“Vilevi hivi vimekuwa vikitumia kwa muda mrefu katika baadhi ya mikoa, awali kundi ambalo lilionekana kutumia zaidi ni wale watoto wa mitaani,” alisema.

Alisema hata hivyo wengi hawajui kwamba vina madhara makubwa kuliko hata dawa za kulevya.

“Mtu anayetumia dawa za kulevya anaweza kusaidiwa kwa kupewa methadone ili aachane nazo lakini hivi vilevi vya gundi na petrol hakuna tiba kabisa ambayo mwathirika anaweza kupewa ili aachane navyo,” alisema.
 http://www.bongo5.com/wp-content/uploads/2017/02/Cocaine-injections-300x194.jpg
Wengi hujidunga kwa njia ya sindano

Dk. Nyandindi alisema madhara ya matumizi ya vilevi hivyo yamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni madhara ya muda mrefu na mfupi.

“Madhara ya muda mfupi ni pamoja na kuchanganyikiwa, kutembea kwa kuyumba-yumba, kuhisi kizunguzungu, kuzungumza kwa lafudhi ya mlevi na maumivu ya kichwa,” alisema.

Aliongeza “Lakini muhusika anapopatwa na hali hiyo mwenyewe anakuwa anasikia starehe na wapo ambao baadae huona maluweluwe, hupata kifafa, hukosa hewa na hatimaye kuzimia au hata kufariki dunia.

Dk. Nyandindi alitaja madhara ya muda mrefu ni kutanuka mishipa ya damu, kuongezeka mapigo ya moyo, kuharibika ini na figo, kupungukiwa au kupoteza kabisa uwezo wa kufikiri.

“Madhara mengine yaliyopo katika kundi hili ni kupoteza uwezo wa kuona (upofu), kuwa kiziwi na kuharibika kwa mfumo wa kutengeneza chembechembe za damu kwenye mifupa mwilini,” alisema.

Alisema iwapo mjamzito atatumia vilevi hivyo, humuweka mtoto wake kwenye hatari ya kuzaliwa na mwili mdogo.

“Mtoto anakuwa hakui vizuri kama inavyotakiwa na anakuwa na mwili mdogo ambao haulingani kabisa na umri wake,” alisema.http://dewjiblog.co.tz/wp-content/uploads/2017/02/DSC_4114.jpg

Dk. Nyandindi alisema vilevi hivyo baadae humsababishia mtumiaji utegemezi (addiction) na pale anapovikosa huhisi kichefuchefu, hutokwa jasho jingi na kujikuna ovyo sehemu mbalimbali za mwili wake.

Alisema mwathirika wa vilevi hivyo hupata pia matatizo ya kukosa usingizi, huwa na hasira za karibu na kwamba tabia yake huwa haitabiriki kwani hubadilika badilika kila mara.

“Nimesema awali kwamba hakuna dawa kwa hiyo ili kumsaidia mwathirika huwa tunalazimika kuzitibu tu zile ‘complications’ ambazo hujitokeza. Hivyo tunamtibu kizunguzungu alichonacho, kifafa au maumivu ya kichwa basi,” alisema.

Dk. Nyandindi alisema tangu vita ya dawa za kulevya itangazwe na Makonda idadi ya waathirika wanaofika kwao kupata tiba imeongezeka.

Alisema awali walikuwa wakipokea waathirika wanne kwa siku, idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia waathirika kati ya 10 hadi 12.