Alhamisi, 9 Machi 2017

DAKTARI: KUKOJOA KITANDANI NI TATIZO LA AKILI, LINATIBIKA

http://i2.wp.com/www.johnkitime.co.tz/wp-content/uploads/2016/10/Bedwetting-Man.jpg?resize=644%2C362NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

‘Kindumbwe ndumbwe chalia, kindumbwe ndumbwe chalia, kikojozi na nguo kaitia moto na ndani kuna viroboto, hilooo’.

Huu ni wimbo uliojizolea maarufu mno hasa katika mitaa yetu ya uswahilini, nyimbo hii huimbiwa mtu ambaye ana tabia ya kujisaidia haja ndogo kitandani mara kwa mara.

Wengi wanaokumbana na kadhia hii ni watoto na vijana, wazazi au walezi huamini kwamba kwa kumzungusha (kumtembeza) mtaani mtu anayetoa haja ndogo kitandani huwa ni moja wapo ya njia ya kumsaidia kubadili tabia na kuacha kukojoa kitandani.

Kwa sababu kamwe anayefanyiwa hivyo hatatamani tena atowekewe na hali hiyo kutokana na aibu kubwa atakayoipata wakati wa utekelezaji wa tukio hilo.

Simulizi ya John

John Wilfred (si jina halisi) mkazi wa Mbezi, jijini hapa ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 15 anasema alikuwa akikabiliwa na hali hiyo wakati wa ukuaji wake.

“Sijui kwanini nilikuwa natokwa na haja ndogo kitandani, mara nyingi nilikuwa naota nikiwa usingizi najisaidia chooni nikishtuka najikuta tayari nimekojoa kitandani,” anasema.
https://cdn-img.pressreader.com/pressdisplay/docserver/getimage.aspx?regionKey=B7WCGFqAlYulDKaAmefQnw%3D%3D&scale=100
Anasema alikuwa anatokewa na hali hiyo mara kwa mara na kwamba mlezi wake aliyekuwa anamlea hakukubaliana na jambo hilo.

“Nilikuwa naishi na shangazi yangu mkoani Pwani, alikuwa akinionya mara nyingi niache tabia hiyo lakini sijui kwanini nilikuwa nashindwa, kuna rafiki yangu alinishauri niepuke kunywa maji nikikaribia kwenda kulala lakini hata nisipokunywa maji nilipoamka nilijikuta tayari mambo yameharibika,” anasema.

Anaongeza “Siku moja shangazi yangu aliniambia amechoka na tabia yangu hiyo, wakati huo nakumbuka nilikuwa na miaka tisa aliwaita rafiki zangu nikaambiwa nijifunike shuka zilizokuwa zimelowa mikojo yangu.

“Nilianza kutembezwa mtaani huku wenzangu wakiniimbia wimbo wa kikojozi, nililia mno siwezi kuisahau siku hiyo. 
Nilikuwa nakaa ndani tu, niliona aibu kutembea hata kucheza na rafiki zangu, na ilipofika usiku nililala kwa wasiwasi mwingi,” anasema.

Anaongeza “Lakini pamoja na hayo yote bado hali ile kunitokea, yule rafiki yangu alinishauri tena nijisaidie kabla ya kwenda kulala na wapo watu walinishauri ninywe maji ya mchele kwamba ni dawa lakini bado niliendelea kukojoa kitandani.

John anasema mwisho wake alichoshwa na hali hiyo na kuamua kumuomba Mwenyezi Mungu ili amsaidie kuondokana nayo.

“Nilipofikisha umri wa miaka 12 hali hiyo ilianza kupungua taratibu na ilikoma kabisa nilipofikisha umri wa miaka 14, sijui nini kilitokea,” anasema.
https://1.bp.blogspot.com/-N3N1U85dcmI/V1dy9jgDZRI/AAAAAAAAcq0/6OyoA_M_G6gi-GPVGo-oSmFTtZLS5PaUgCLcB/s1600/jjjg.jpg
Mwathirika mwingine

Naye Miriam Joram (28) anasema kamwe hawezi kuisahau siku alipowekewa chura kitandani na ndugu zake kwa kile walichoelezwa kuwa ni dawa ya kumsaidia yeye kuacha kukojoa kitandani.

“Nilikuwa nalala chumba kimoja na dada zangu wawili, walichukizwa na tabia yangu ya kujikojolea kitandani, walikuwa wanalalamika kuwa nasababisha chumba kuwa na harufu mbaya.

“Lakini hata mimi sikuwa napenda kukojoa kitandani, ni hali iliyokuwa inanikuta tu nikiwa usingizini,” anasema.

Anasema pamoja na kuwekewa chura hali hiyo haikuondoka na kwamba jirani yao mmoja alimshauri apande juu ya mti mkubwa kisha ajisaidie haja ndogo akiwa juu ya mti huo kwamba ni dawa nzuri ya kuacha tabia hiyo.

“Nilifanya jambo hilo, nilisubiri usiku ukafika, nje ya nyumba yetu kulikuwa na mti mkubwa wa mwembe, ndugu zangu walinisaidia kunipandisha juu ili nijisaidie.

“Nikiwa kule juu ya mti nilihisi wakati wowote nitadondoka chini, nilipolala mawazo yale yaliendelea kujirudia, kwa muda wa wiki moja sikuweza kukojoa kitandani,” anasema.

Anasema hata hivyo hali hiyo ilianza tena kujirudia kitendo kilichofanya mama yake kumnunulia godoro dogo ambalo alikuwa akilazimika kulitandika chini kila ilipofika usiku na kulala hapo.

“Si unavijua hivi vigodoro wanavyoenda ‘boarding’ mama alininunulia, ikifika usiku natandika chini nachomekea neti nalala kwa sababu wenzangu walikuwa wanalalamika mno na kila asubuhi nililazimika kutoa godoro nje kulianika na kufua shuka zangu,” anasema.

Anasema mama yake alijitahidi kutafuta dawa za kumsaidia hadi kwa waganga wa kienyeji lakini bado hali iliendelea kujirudia.
http://www.yasu8407.sakura.ne.jp/prime/Archives/gallery/Bedwet/01/06d.jpg
“Lakini ilikoma nilipofikisha umri wa miaka 15, nilifurahi mno niliona kama vile nimetua mzigo mzito uliokuwa umenielemea, ilianza kuondoka kidogo kidogo nadhani ni kwa sababu mama yangu alikuwa akinishauri kwa upendo.

“Jambo lililokuwa likiniumiza na kuniacha na maswali mengi yaliyonifanya nichukie hali ile ni pale aliponiuliza swali kwamba itakuwaje kama nitaendelea kutokwa haja ndogo kitandani, nikiwa mkubwa na kuolewa, nitaenda kutia aibu kwa mume wangu.

“Kauli hiyo nilikuwa naitafakari mno na nikaanza kuchukua hatua ili nisiiabishe familia yangu ingawa ilikuwa ni kipindi kigumu,” anasema Miriam ambaye kwa sasa ameolewa na ni mama wa mtoto mmoja.

Kwanini hali hiyo hutokea

Doroth Mushi ni Daktari Bingwa wa Afya ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) anasema kutokwa na haja ndogo kitandani si hali ya kawaida bali ni tatizo la lililopo katika kundi la magonjwa ya akili.

“Wengi hawajui kwamba hadi mtu anafikia hatua hiyo maana yake kuna tatizo kwenye mfumo wake wa fahamu, hakuna mawasiliano vizuri, hali inayopelekea mtu kushindwa kuhimili hali ya kujizuia haja ndogo akiwa usingizi na wapo wengine ambao hushindwa kuhimili hata haja kubwa pia,” anasema.

Anasema kwa kuwa wengi hawajui jambo hilo huishia kuwaadhibu watoto na vijana wao wakidhani kuwa huenda wanafanya makusudi kumbe ni wagonjwa.

“Wazazi na walezi wengi kwa kuwa hawajui ni ugonjwa wanaishia kuwapa adhabu, wanawatembeza mtaani kumbe hawamsaidia bali wanamuongezea tatizo juu ya tatizo,” anasema Dk. Doroth (pichani juu).
Kikwazo kwa wana-ndoa

Tumeshuhudia baadhi ya ndoa zikivunjika na nyingine zikiwa hazina maelewano kutokana na mmoja wao kupatwa na adha hiyo.

Vijana wasaka tiba

Daktari huyo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Muhimbili (MUHAS) Idara ya Magonjwa ya Akili kwa Watoto na Vijana anasema wamekuwa wakipokea vijana wengi wanaokabiliwa na tatizo hilo.

“Kwa kuwa kuna ambao tayari tulishawasaidia na wameondokana na tatizo hilo, wanapokwenda na kuwaeleza wenzao nao wanajua sasa kwamba kuna msaada.

“Kwa hiyo hapa Muhimbili katika Idara yetu tunao vijana tunaowahudumia, kati ya vijana hao wapo wanaotueleza wanapata shida mno kwani wanataka kuingia katika maisha ya ndoa lakini wanashindwa kutokana na hali hiyo, ni changamoto inayoikabili pia jamii yetu,” anasema.

Tatizo hutokeaje

Dk. Doroth anasema zipo sababu nyingi zinazochangia mtoto kupata tatizo la afya ya akili maishani mwake, ni hizi zifuatazo.

Uchungu wa muda mrefu

“Mama akipata uzazi pingamizi (uchungu muda mrefu) ni hatari kwa mtoto kwani husababisha baadae kupata magonjwa ya akili, mama anapokaa na uchungu muda mrefu husababisha mtoto kukosa hewa ya kutosha ya oxijeni kwenye ubongo wake,” anasema.
https://globalpublishers.co.tz/wp-content/uploads/2015/10/PainDuringpregnancy2.jpg
Anasema ubongo wa mtoto unapokosa oxijeni katika kipindi hicho husababisha madhara makubwa kwenye ubongo wake ambapo hata akizaliwa hauwezi kujitengeneza tena.

“Sasa kulingana na ubongo ulivyoathirika huwa tunaona madhara hayo yakitokeza nje baadae wakati wa ukuaji wa mtoto husika,” anasema.

Anasema yapo pia baadhi ya magonjwa ambayo mama akiugua wakati wa ujauzito humsababishia matatizo mtoto wake pindi atakapozaliwa.

“Ndiyo maana wataalamu wa afya tunasisitiza ni vema mwanamke anapojihisi ni mjamzito awahi hospitalini kuanza kliniki ili afya yake iwe inafuatiliwa na ajitunze kumlinda mtoto wake aliyembeba tumboni,” anasema.

Sababu za kibaiolojia

Dk. Doroth anasema magonjwa ya kiakili nayo katika kundi la magonjwa ya kurithi na hukumba kizazi kimoja hadi kingine.

“Magonjwa haya yapo kwenye vina saba pia, ndiyo maana unaweza kukuta katika baadhi ya familia baba anaugua ugonjwa wa akili, baadhi ya watoto wake na hadi wajukuu kama amebahatika kuwa nao wanaugua magonjwa ya akili,” anasema.

Vitendo vya ukatili

“Leo hii tunashuhudia kuna vitendo vingi vya ukatili wanavyofanyiwa watoto majumbani, wengine wanatelekezwa na wazazi wao si jambo zuri kwani vitendo hivyo vinawaathiri kisailikolojia,” anasema.

Ugonjwa wa usonji

Dk. Doroth anasema yapo pia baadhi ya magonjwa ambayo mtoto akiugua yanaweza kumsababishia kupata magonjwa ya kiakili hapo baadae ukiwamo usonji.
http://www.askdrmakkar.com/images/bed%20wet%20or%20enuresis.jpg
“Ugonjwa huu huathiri uwezo wa mtoto kuwasiliana na jamii yake kwa lugha inayotakiwa. Unakuta mtoto anakosa utulivu, tabia zake zinakuwa haziendani na jamii yake, hawezi kukaa hata sekunde kila wakati anakuwa kama saa zote yupo kwenye mwendo, hana subira,” anasema.

Ugonjwa wa sonona

“Huu ni ugonjwa ambao huathiri hisia, mtu hukosa raha, kwa mfano mtoto akikosa vitu muhimu anavyohitaji wakati mwingine hupatwa na hali ya wasiwasi uliopitiliza kwa mfano akiachwa na wazazi wake. Hali hiyo ikiendelea bila kupata msaada ni hatari,” anasema.

Malezi

Anasema kipindi cha ukuaji wa mtoto ni cha muhimu kuzingatia kwani ndiyo wakati ambao huhitaji kujifunza vitu vingi kutoka kwa watu waliomzunguka.

“Lakini jamii yetu ya leo hali ni tofauti, watoto hawalelewi vizuri, unakuta leo yupo kwa mjomba kesho kwa bibi kesho kutwa kwa shangazi, halelewi mahala pamoja ni vigumu kwa mtoto huyu akili yake kujifunza inavyotakiwa.

“Kule kubadilika badilika kwa walezi humfanya ubongo wake kushindwa kukua na hivyo kuchochea kupata magonjwa ya kiakili katika ukuaji wake kwa sababu anashindwa kuelewa kipi ni sahihi kipi si sahihi,” anasema.

Utamgunduaje mtoto mwenye tatizo

Daktari huyo anasema ni rahisi kumgundua mtoto mwenye tatizo kwani hufanya mambo ambayo hayaendani na tabia za jamii husika inayomzunguka.

“Dalili hujitokeza kulingana na mfumo wa ukuaji wa neva zake za fahamu, mara nyingi hutamgundua akifikisha umri wa kwenda shuleni. Hali yake ya kujifunza huwa hailingani na watoto wa umri wake,” anasema.

Anasema uwezo wake wa kitaaluma huwa ni mdogo kulinganisha na watoto wa umri wake na kwamba uwezo wake wa kujifunza kutokana na mazingira yanayomzunguka nao huwa ni mdogo.

Anasema wakati mwingine hata uwezo wake wa kuzungumza nao huwa ni mdogo ikilinganishwa na watoto wenzake wa umri wake.

Utukutu

“Unakuta mtoto ni mtukutu mno, si rafiki kwa wenzake hata wanyama, yaani anashindwa kabisa kuendana na tabia za jamii yake anayoishi nayo na huwa hafuati taratibu hata za shuleni, unakuta anapinga kila anachoelekezwa, huu nao ni ugonjwa wa akili,” anasema.

Majanga ya kijiografia

Dk. Doroth anasema yapo pia majanga mbalimbali ya kijiografia ambayo mtoto akiyashuhudia humsababishia baadae kupata magonjwa ya kiakili.

“Kwa mfano tetemeko la ardhi, linapotokea na mtoto akashuhudia jinsi inavyokuwa hali hiyo humuathiri kisaikolojia na hivyo anahitaji kupatiwa msaada mapema,” anasema.

Sababu nyinginezo

Daktari huyo anazitaja kuwa ni pamoja na majanga ya vita na hata ugonjwa wa kifafa.

“Kwa kundi la vijana tunaowapokea tumebaini sababu kubwa inayochangia wao kupata magonjwa ya kiakili ni utumiaji wa dawa za kulevya na pombe,” anasema.

Athari

Anasema mtoto au kijana mwenye tatizo la akili asipopatiwa matibabu mapema hupelekea baadae kuwa tegemezi kwa jamii na nchi kwa ujumla.

“Kwa sababu anakuwa hana uwezo wa kushiriki vema katika shughuli za kijamii na kiuchumi hivyo familia yake inakuwa na mzigo mkubwa wa kumsaidia kwani matatizo haya kama hatibiwa mapema huweza hata kumsababishia ulemavu wa kudumu katika maisha yake,” anasema.

Hatua za kuchukua

“Mzazi au mlezi akiona mwanawe ana dalili hizo nilizotaja hapo juu ni vema amuwahishe mtoto wake hospitalini afanyiwe uchunguzi na apatiwe tiba mapema iwapo atagundulika kuwa na tatizo,” anasema.

Anasema huwa wanatumia dawa maalumu katika kutoa tiba pamoja na ushauri wa kumjenga kisaikolojia.

“Lakini tiba hutolewa kulingana na hatua aliyofikia mgonjwa wakati mwingine hulazimika hadi kumpeleka katika shule maalumu zilizotengwa kwa ajili yao,” anasema.

Ushauri

Daktari huyo anashauri wazazi na walezi wanaolea watoto na vijana wanaokabiliwa na matatizo ya kiakili kuacha kuwaficha ndani badala yake wawapeleke hospitalini watibiwe.

“Lakini pia jamii ihusike katika kuwasaidia watoto kujifunza mambo yaliyo mema ili tuweze kuwa na kizazi bora baadae kitakachosaijia ujenzi wa Taifa letu,” anasema.

Makala haya kwa mara ya kwanza yalichapishwa katika gazeti la MTANZANIA Januari 26, mwaka huu.