Mwananchi akipita pembezoni mwa rundo la takataka, uchafu ni chanzo cha magonjwa mengi ikiwamo kipindupindu (picha na mtandao)
Na Veronica Romwald, Aliyekuwa Dodoma
UCHAFU wa mazingira ni chanzo kikuu cha magonjwa
mengi ya kuambukiza hasa ya kuhara, kila mwaka watu bilioni 1.7 huugua magonjwa
ya kuhara duniani.
Takwimu hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya
Duniani (WHO) ambalo linaeleza watu milioni 1.8 hufariki dunia kila mwaka
kutokana na magonjwa hayo.
Idadi hiyo ni sawa na wastani wa vifo vinne kila
dakika, kwamba hali hiyo huchangiwa zaidi na ukosefu wa vyoo bora.
Shirika hilo linaeleza watu bilioni 2.3 sawa na
theluthi ya watu wote duniani hawatumii vyoo bora na watu milioni 892 hawana
kabisa vyoo bora.
Kwa mujibu wa Shirika hilo asilimia 70 ya wakazi
waishio katika Bara la Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania
ikiwamo hawana kabisa vyoo bora.
Takwimu zinaeleza asilimia 40.5 ya kaya zote Tanzania
ndizo zenye vyoo bora huku Kaya 600,000 zenyewe hazina vyoo bora.
Aidha, kila mwaka watu 30,000 huugua magonjwa ya
kuhara nchini hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 83 ya wagonjwa wote wanaolazwa
kila siku hospitalini.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hasaan wakipiga makofi kushangilia baada ya uzinduzi wa awamu ya pili ya Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira hivi karibuni mjini Dodoma
Ni
idadi kubwa
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu anasema katika kila wagonjwa 100 wanaofika katika
vitengo vya wagonjwa wa nje hospitalini (OPD) kwa siku 60 huwa ni wale
wanaougua magonjwa yatokanayo na hali ya uchafu.
“Ni wengi lakini tunaweza kukabili jambo hili kwa kuhamasisha wananchi kubadili mtizamo waliona
nao juu ya ujenzi, matumizi ya vyoo bora na kuzingatia kunawa mikono baada ya
kutoka chooni,” anasema.
Anaongeza “Nasema hivi kwa sababu, ingawa Rais John
Magufuli ametuongezea bajeti ya dawa lakini ikiwa hatutaweza kukabili magonjwa
haya itakuwa ni sawa na bure.
“Uchambuzi wa Benki ya Dunia (WB) inatueleza kila
mwaka tunatumia zaidi ya Sh bilioni 400 kutokana na hali ya uchafu ni fedha
nyingi ambazo tutaweza kuziokoa ikiwa tutafanikiwa kuhamasisha wananchi katika
hili,” anasema.
Choo
bora ni kipi?
Anasema katika mazingira ya Tanzania ni kile
ambacho kimejengwa na kusakafiwa vema kuwezesha maji kupita kwa wepesi huku
shimo linalohifadhi kinyesi likiwa limejengwa kwa nje na kikiwa kimeezekwa.
“Watanzania wasidhani ni kile minachohitaji
kuwekewa masinki, tairizi… hapana, na si kwamba watanzania hawawezi kujenga
vyoo bora tatizo ni ule mtizamo waliona juu ya matumizi ya vyoo, tumekusudia
kuwafikishia elimu hii,” anabainisha.
Mwakilishi
wa DFID
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la DFID nchini Tanzania
Elizabeth Arthur, anasema uchafu ni chanzo kikuu cha udumavu kwa watoto nchini
Tanzania.
Anasema takwimu zinaonesha kila mwaka watoto 18.500
hufariki dunia sawa na watoto 50 kila siku kutokana na magonjwa ya kuhara
“Watoto wanaopata udumavu wapo katika hatari kubwa ya
kuugua magonjwa mbalimbali kama vile nimonia, surua na mengineyo mengi,”
anabainisha.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akishiriki kufanya usafi mapema mwaka huu (picha na mtandao)
Mama
Samia
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anasema takwimu
hizo zinaonesha kwamba hali ya maisha ya binadamu si nzuri hivyo juhudi
zinahitajika kufanyika kuboresha usafi wa mazingira.
“Zinaonesha pia watu wengi nchini hawana maeneo
maalum ya kunawia mikono na asilimia 12 pekee ya watanzania hunawa mikono kwa
maji safi na sabuni baada ya kutoka chooni,” anasema.
Akitolea mfano, anasema tangu mwaka 2015 ugonjwa wa
kipindupindu ulipogundulika hadi kufikia Novemba 12, mwaka huu tayari watu
27,554 wameripotiwa kuugua.
“Katika kipindi hicho vimeripotiwa vifo 432, hii ni
idadi kubwa na tungeweza kuepukana na hali hii ikiwa tungekuwa na mazingira
yaliyo safi, hivyo ni lazima tuchukue hatua,” anasema.
Hatua
zachukuliwa
Waziri Ummy anasema ili kukabili hali hiyo waliona
umuhimu wa kuendeleza kampeni ya ‘Mtu ni Afya’ iliyoanzishwa na kutekelezwa
kati ya mwaka 1973 hadi 1978 na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Kampeni hiyo ya ‘Mtu ni Afya’ ilituchagiza Wizara
pamoja na wadau wa maendeleo kuandaa kampeni inayofanana na hiyo ili tuweze
kupambana na changamoto za usafi zilizopo nchini.
Anasema mwaka 2012 hadi 2016 walizindua awamu ya
kwanza ya Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira ambayo ililenga katika kuhamasisha
ujenzi na matumizi ya vyoo bora.
Anasema awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, ilihusisha
Wilaya 196 nchini na kwamba mafanikio makubwa yamepatikana.
“Tumefanikiwa kuzifikia Kaya 516,444 ambazo
zimejenga vyoo bora kati ya Kaya 600,000 tulizokuwa tumezikusudia hii ni sawa
na asilimia 87 ya mafanikio,” anasema.
Anasema katika awamu hiyo ya kwanza ya mpango huo
walilenga Kaya 800,000 zinatengeneza sehemu maalumu za kunawa mikono ambapo
wamefanikiwa kuzifikia Kaya 701,788.
“Tulilenga kuboresha huduma za vyoo katika vituo
vya kutolea huduma za afya, tumeweza kujenga vyoo katika vituo 441 awali
tulilenga kufikia vituo 250 hivyo tumefanikiwa kwa kiwango cha asilimia 176 ya
lengo letu,” anabainisha.
Anaongeza “Walilenga pia kuzifikia Kaya milioni
moja ili kuzihamasisha kutibu maji ya kunywa kwa kutumia dawa ya fluoride au
kwa kuyachemsha.
“Tumefanikiwa kuzifikia Kaya 684,477 ambazo sasa
zimeanza kutibu na kuchemsha maji ya kunywa hii ni sawa na asilimia 93 ya lengo
letu tulilokusudia,” anasema.
Njombe
yatia fora
Waziri Ummy anasema Wilaya ya Njombe imefanya
vizuri zaidi ambapo Kaya zote 240200 zimejenga vyoo bora.
Anasema shule za msingi 44 kati ya 52 zilizopo
wilayani humo zina huduma ya vyoo bora kwa matumizi ya walimu, watumishi wasio
walimu na wanafunzi (bila kusahau wenye ulemavu).
“Wametenga pia vyumba maalum kwa usafi wa wasichana
waliopevuka, mafanikio haya yamepatikana katika awamu ya kwanza, tunaona wazi
inawezekana kabisa kila Kaya nchini kuwa na choo bora.
Mkakati
zaidi
Anaongeza “Ikiwa Njombe wameweza, tunajiuliza
kwanini zingine zishindwe na ndiyo maana tunazindua awamu ya pili ya Mpango wa
Taifa wa Usafi wa Mazingira.
Anasema awamu ya pili ya mpango huo utatekelezwa
kwa miaka mitano kuanzia sasa hadi kufikia Juni, 2021.
“Utaenda sambamba na program ya maendeleo ya sekta
ya maji wenye ‘component’ (vipengele) nne, ambapo ile ya nne inahusu masuala ya
usafi wa mazingira,” anabainisha.
Malengo
Anasema wamekusudia kutekeleza maeneo manne katika
awamu hii ikiwamo kuendelea kusimamia ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika ngazi ya kaya.
“Tumekusudia kuzifikia kaya milioni 5.6, kufikia
2021, tunataka kuimarisha huduma za unawaji mikono kwa maji na sabuni kwa kaya
hizo.
“Tunataka shule za msingi 3,555 ziwe na vyoo bora
na sehemu za kunawia mikono pamoja na shule za sekondari 700, aidha,
tumekusudia kujenga vyoo bora katika vituo 1,000 vya kutolea huduma za afya
nchini” anasema.
Anasema wamekusudia pia kujenga vyoo bora 540
katika vituo vya mabasi ili kukabiliana na changamoto ya watu kujisaidia
‘porini’ wakati wa safari.
“Awamu ya pili itahusisha Wilaya zote 185 zilizopo
nchini,” anabainisha Waziri Ummy
Kipimo
kwa wakurugenzi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Suleiman Jaffo anawataka wakurugenzi wa Wilaya zote nchini
kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kutekeleza Kampeni hiyo kwa vitendo.
“Katika awamu ya kwanza kuna mikoa ambayo
haikufanya vizuri, katika awamu hii nataka kila mmoja atimize wajibu wake,”
anatoa rai.
Anaongeza “Lengo letu tuwe na mazingira safi
tukabili magonjwa yatokanayo na hali ya uchafu, ni muhimu pia wataalamu wa afya
mtenge fedha za kutosha katika kusimamia jambo hili.
“Ningependa kuona kila mmoja anatimiza wajibu wake,
kuna Wilaya zimefanya vizuri zimakabidhiwa zawadi zao mbalimbali, natamani
ifike mahala kila tunayempima awe mshindi katika utekelezaji wa mpango huu,”
anasema.
Mikopo
ya vyoo
Mama Samia anazitaka taasisi za kifedha kuona
umuhimu wa jambo hilo na kuanza kutoa mikopo maalumu ya ujenzi wa choo kwa
wananchi.
“Waweke kipengele maalumu mwananchi akopeshwe fedha
zitakazotumika kujenga choo bora, hatua hiyo itasaidia mno kukabiliana na
changamoto hii.
“Tutaweza kukabiliana na magonjwa yatokanayo na
hali ya uchafu wa mazingira, lazima tushirikiane katika hili ili tuweze kufikia
malengo tuliyojiwekea,” anasisitiza.
Anaongeza “Kampeni hii imekuja wakati ambapo dunia
inaendelea kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s).
Anasema usafi wa mazingira ni mojawapo ya viashiria
196 vilivyomo kwenye malengo 17 ya SDG’s.
Anasema kati ya malengo hayo, lengo la tatu
linahusu uboreshaji wa afya na ustawi wa jamii na lengo la sita linahusu
upatikanaji wa huduma za maji safi na salama na usafi wa mazingira.
Anasema malengo hayo yanalipa Taifa msukumo wa
kuhakikisha yanafikiwa kabla ya kufikia mwaka 2030.
“Ndani ya malengo haya mawili tunatakiwa kupunguza
magonjwa ya kuambukiza kwa kuhakikisha tunaboresha usafi wa mazingira.
“Wachambuzi wa masuala ya mipango na maendeleo wameeleza
dunia haiwezi kufikia malengo ya SDG’s ikiwa lengo la sita linalohusu huduma
bora za maji na usafi wa mazingira halitafikiwa, maji ni uhai na ndiyo
yanayoleta usafi wa mazingira.
Anaongeza “Kwa kuzingatia ukweli huo, serikali
inatekeleza Program ya Maendeleo ya Maji ya mwaka 2006/2025 ambayo ndani yake
kuna program ya usafi wa mazingira ambayo pia inasimamia kampeni ya Taifa ya
Usafi wa Mazingira.
“Hivyo hatuna budi kuwekeza katika kusimamia usafi
wa mazingira ili kuhakikisha tunafikia malengo ya Taifa tuliyojiwekea na haya ya
Kimataifa yaliyowekwa,” anasema.
DFID
wapo tayari
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la DFID - Tanzania
Elizabeth Arthur, anaipongeza serikali ya awamu ya tano kuona umuhimu wa
kuendeleza mapambano dhidi ya uchafu wa mazingira ili kunusuru afya za wananchi
wake.
“DFID tupo tayari kuendelea kushirikiana na
serikali ya Tanzania kuiwezesha kwa kila namna ili iweze kufikia lengo
iliyojiwekea kwamba kufikia mwaka 2025 kila Mtanzania awe na choo bora nyumbani
kwake.
“Ni muhimu pia mashirika mengine ya kimataifa na
wadau wa maendeleo wakaunga mkono jitihada hizi na wananchi kwa ujumla
wakashiriki katika kampeni, usafi unahitaji nidhamu na utayari,” anashauri.
Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia Desemba 14, 2017.
Chapisha Maoni