Picha na mtandao
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
KATI ya Novemba 25 hadi Desemba mosi, 2017 Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) ilifanya upasuaji mkubwa wa moyo wa kihistoria nchini.
Madaktari Bingwa wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi
ya Open Heart International kutoka nchini Austraria waliwafanyia upasuaji
wagonjwa 16 wenye matatizo mbalimbali ya moyo.
Kati ya wagonjwa hao tisa walikuwa watoto na saba walikuwa
watu wazima ambao walifanyiwa upasuaji wa kubadilisha milango ya moyo iliyokuwa
imeharibika na kuwekewa milango ya chuma.
Miongoni mwa watu wazima waliofanyiwa upasuaji wapo ambao
walipandikizwa mishipa ya damu iliyovunwa kutoka miguuni na kwenda kuzibua ile
iliyokuwa imeziba.
“Upasuaji huo kitaalamu unaitwa bi-pass surgery, hii si mara
ya kwanza kwa taasisi yetu kufanya kwani tayari wagonjwa wapatao 30 wamefanyiwa
kwa mwaka huu pekee,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed
Janabi.
Profesa Janabi (pichani) Anasema kati ya wagonjwa hao 16 waliofanyiwa upasuaji katika
kambi hiyo ya matibabu, tisa walikuwa ni watoto.
“Walikuwa na umri wa kuanzia miezi minne wakiwa na uzito wa
kuanzia kilo nne hadi 12, kati ya watoto hao, mmoja (jina linahifadhiwa) alikuwa
amezaliwa akiwa na moyo upande wa kulia,” anabainisha.
Ipoje?
Kibaiolojia moyo wa binadamu upo upande wa kushoto hata
hivyo, Profesa Janabi anasema hutokea mara chache mtoto kuzaliwa moyo ukiwa
upande wa kulia.
Chanzo
ni nini?
Anasema bado haijajulikana wazi nini hasa husababisha mtoto
kuzaliwa moyo wake ukiwa katika upande wa kulia.
“Duniani tafiti zinaonesha kati ya watoto 2000 wanaozaliwa
basi mmoja huwa katika uwezekano wa kuzaliwa moyo wake ukiwa upande wa kulia,”
anasema.
Anasema hata hivyo hakuna madhara yoyote yanayoweza kumpata
mtoto ambaye moyo wake umeumbwa ukiwa upande wa kulia.
“Anaweza kuishi vema kabisa kama binadamu wengine ambao
wameumbwa wakiwa na moyo katika upande wa kushoto,” anabainisha.
Kwanini
walimpasua?
Profesa Janabi anasema walilazimika kumfanyia upasuaji mtoto
huyo kwani alikuwa na matatizo makubwa mawili ya moyo.
“Moyo kuumbwa upande wa kulia haikuwa tatizo kubwa, isipokuwa
tulibaini mishipa yake ya damu ilikuwa haifanyi kazi inavyopaswa.
“Katika moyo kuna mishipa inayoingia upande wa kulia ambayo
kazi yake kuu ni kubeba damu chafu yenye hewa ya Kabonidaioksaidi na kuna
inayoingia upande wa kushoto yenyewe hubeba damu safi yenye oksijeni,”
anabainisha.
Anaongeza “Huyu mishipa yake ilikuwa inachanganya damu safi
na chafu kwa pamoja jambo ambalo lilikuwa ni hatari kwa maisha yake.
Jengo la JKCI
Kivipi?
Anafafanua “Ni kama vile uchukue maji safi na taka halafu
uyachanganye kwa pamoja kisha unywe, kamwe mwili hauwezi kuhimili mchanganyiko
huo.
“Sasa yeye badala ya damu chafu kupita katika upande
unaostahili ili ikasafishwe huchanganyika pamoja na damu safi iliyokwisha
safishwa kisha iende mwilini kutumika, ni tatizo,” anasema.
Anasema pamoja na tatizo hilo, tatizo jingine lilikuwa kwamba
mapigo yake ya moyo yalikuwa chini mno kutokana na kiwango kidogo cha umeme
kwenye moyo wake.
“Kutokana na hali hiyo, ilibidi tumpandikize betri ndani ya
moyo wake, hii ni oparesheni ya tatu kwa watoto na sasa mapigo yake yanakwenda
vema,” anasema.
Anasema ilichukua takriban saa tisa kumfanyia na kukamilisha
upasuaji huo.
“Kwa sababu kwa case kubwa namna hili hutulazimu
‘kuusimamisha’ moyo wake kwa saa kadhaa,” anabainisha.
Kisa cha
kuwa bluu
Anasema ni kutokana na mchanganyiko huo wa damu safi na chafu
ndipo hupelekea mtoto kugeuka kuwa na rangi ya bluu.
“Kitendo cha kugeuka kuwa na rangi ya bluu maana yake ni
kwamba kile kiwango cha oksjeni kinachohitajika mwilini huwa hakitoshelezi,”
anabainisha.
Dalili
zake
Anasema dalili za awali kwa mtoto aliyezaliwa na tatizo la
moyo ambazo mzazi anaweza kuziona ni pamoja na kushindwa kunyonya vizuri.
“Hii huwa zaidi kwa wale ambao wapo katika umri wa kunyonya
lakini kwa wale ambao wapo katika umri wa kwenda shule wengi huchoka mara kwa
mara,” anabainisha.
Makuzi
yake
Anasema yataendeelea vizuri baada ya upasuaji huo na kwamba
ataishi na kulelewa kama ilivyo kwa watoto wengine wasio na tatizo.
“Kila mshipa wa damu sasa unafanya kazi yake kama
inavyotakiwa na mfumo wa umeme upo sawa sawa baada ya kumpandikiza betri hiyo,”
anasema.
Anaongeza “Lakini kama asingetibiwa mapema basi kidaktari
naweza kusema wazi kwamba asingefika na kusherehekea sikukuu yake ya kuzaliwa
ya mwaka mmoja.
“Ila kwa kuwa tumewahi kumfanyia upasuaji tunaamini Mungu
akimjalia basi atasherehekea sikukuu yake ya mwaka wa kwanza na kuendelea,”
anasema.
Masharti
Anasema mtoto huyo ataishi na kula kila kitu isipokuwa
amepewa masharti kadhaa.
“Tumempatia kadi maalumu ya utambuzi, hatatakiwa kupita
kwenye maeneo ambayo yana sumaku kubwa kama vile uwanja wa ndege kwa sababu ile
nguvu inaweza kukiwasha na kupelekea mapigo ya moyo kubadilika na kwenda kasi,”
anasema.
Ushirikiano
zaidi
Mkufunzi wa Wagonjwa Mahututi na daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo wa OHI, Russel Lee anasema wataendelea kushirikiana kwa ukaribu na JKIC
katika kutoa matibabu.
“Kila ninapokuja Tanzania naona JKCI inazidi kufanya
matibabu kwa kiwango cha juu zaidi ya awali, hili ni jambo linalotia faraja
kubwa, OHI tutaendelea kushirikiana nao pia kwa kuwapatia mafunzo wataalamu
wake ili wazidi kufanya vizuri zaidi,” anasema.
Faida
zake ni zipi?
Daktari Bingwa wa Upasuaji Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa
JKCI, Godwin Sharau (Pichani) anasema faida kubwa wanayopata katika kambi hizo za
matibabu ni kubadilisha ujuzi.
“Kuna baadhi ya magonjwa ya moyo ambayo ni magumu sana na
JKCI tunahitaji kupanda hatua kwa hatua ili tuweze kuwa- manage watoto na watu
wazima ambao wana matatizo haya.
“Hivyo tunataka twende sambamba na wenzetu katika teknolojia
ya kutibu magonjwa ya moyo ili kufikia adhma ya serikali kupunguza idadi ya
wagonjwa wanaoenda kutibiwa nje ya nchi,” anasema.
Anaongeza “Ndiyo maana tunahitaji kukutana mara kwa mara na
wenzetu ambao wamefika mbali katika utoaji matibabu ya magonjwa ya moyo kusudi
tupate ule ujuzi walionao.
Wito
Anawasihi wazazi wanapoona dalili hizo wawahi kuwapeleka
watoto wao hospitalini kwa uchunguzi zaidi.
“Ukimpeleka hospitalini watabaini tatizo na kama anastahili
kuletwa JKCI watampa rufaa kuja huku, kuendelea kukaa naye nyumbani
kutahatarisha zaidi maisha yake na kupelekea kufariki dunia.
“Lakini akiletwa hospitalini tukamfanyia uchunguzi kama
atahitaji upasuaji tutamfanyia na anakuwa na uwezekano mkubwa wa kuishi maisha
marefu kuliko akiendelea kukaa nyumbani,” anasema.
Anaongeza “Katika mwaka huu pekee tumeweza kuwafanyia
upasuaji watoto wapatao 300 wenye matatizo ya moyo, ukijumlisha na watu wazima
idadi yao inazidi 600.
“Lakini katika mwaka huu pekee watoto waliopoteza maisha ni
wanne tu, hivyo wasiogope kuja kuwafanyia uchunguzi na upasuaji watoto wao,”
anawasihi.
Profesa Janabi anawahimiza pia wataalamu wa afya kuhakikisha
wanawapa rufaa mapema kwenda JKCI watoto wanaowapokea wakiwa na dalili hizo.
“Wawalete kwetu mapema, wasikae nao na kujaribu ‘diagnosis’
mbalimbali kwamba labda ni malaria, uti wa mgongo, nimonia au magonjwa
mengineyo,” anawahimiza.
Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka kwenye gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia Desemba 21, 2017
Chapisha Maoni