>Wanawake waathirika zaidi kuliko wanaume
NA
VERONICA ROMWALD - DAR ES SALAAM
DUNIANI
kuna watu wa jinsia mbili yaani ya kike na ya kiume, hata hivyo wakati mwingine
huweza kutokea mtu akazaliwa na jinsia zote mbili.
Hali
hiyo inaelezwa kibaiolojia si jambo la kawaida na hutambulika kuwa ni tatizo la
jinsia tata kitaalamu linaitwa ‘Ambigious Genitalia’.
Ni
neno linalotumika kueleza viungo vya siri vya mtoto aliyezaliwa ambavyo ni
vigumu kujua ni wa jinsia ya kike au ya kiume.
Inaelezwa,
mtoto wa kike mwenye tatizo hilo huzaliwa na kiungo kinachofanana na uume,
mfuko wa korodani na kwamba tundu la njia ya uzazi huwa halionekani kabisa.
Aidha,
mtoto wa kiume mwenye tatizo hilo, huzaliwa na tatizo la kutokufunguka kwa njia
ya mkojo mwishoni mwa uume, uume kuwa mfupi sana, kutokuwepi kwa korodani ndani
ya vifuko vyake au kuwa na uwazi katikati ya korodani.
Daktari
Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaitun
Bokhari anasema tatizo hilo huwaathiri zaidi watoto wa kike kuliko wa kiume.
Anasema
kitaaluma punde tu baada ya mama kujifungua daktari au mkunga huwajibika
kumnyanyua mtoto na kumuonesha ili atambue jinsia ya mtoto wake.
“Moja
kwa moja mama hupeleka macho yake eneo la sehemu ya siri ya mwanawe na anapoona
anataja jinsia aliyoiona kama ni wa kike au wa kiume,” anasema.
Anasema
katika hatua hiyo ni vigumu mno mama kubaini kasoro ikiwa mtoto wake amezaliwa
na tatizo la jinsia tata.
“Nimesema
awali kwamba tatizo hili linawalabili zaidi watoto wa kike kuliko wa kiume, kwa
sababu mama anapomuangalia mtoto pale anapooneshwa akiona uume umechomoza moja
kwa moja anasema ni wa kiume na asipouona anasema ni wa kike.
“Si
rahisi kugundua kwa sababu unaweza kukuta mtoto wa kike anazaliwa akiwa na
kinena kikubwa kuliko kawaida kiasi kwamba mtu anaweza kukifananisha na uume wa
mtoto aliyezaliwa.
“Mtoto
wa aina hiyo, anakuwa na mashavu ya uke kama kawaida na yale matundu muhimu
kwenye uke au wakati mwingine unakuta yale mashavu yameungana.
“Lakini
ukimwangalia kule chini unakuta ana njia ya haja ndogo kama kawaida,
ni maumbile yenye utata hivyo kutokana na hali hiyo ndiyo maana ni vigumu mama
kutambua kasoro pale anapooneshwa mtoto wake punde tu baada ya kujifungua,”
anasema.
Wakati
wa ukuaji
Dk.
Bokhari anasema kwa kuwa wazazi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu
tatizo hilo, huendelea kulea watoto wao wakidhani ni hali ya kawaida kumbe la.
“Hushindwa
kutambua mapema kwamba ni tatizo linalohitaji kutafutiwa ufumbuzi mapema,
hudhani ni hali ya kawaida na wengine hudhani watoto wao wapo katika hali hiyo
kutokana na unene, kumbe ni tatizo,” anasema.
Anaongeza
“Kwa hiyo unakuta mtoto analelewa kama vile wa kiume kumbe ni wa kike au
analelewa kama wa kike kumbe ni wa kiume.
Chanzo
chake
Tatizo
hilo inaelezwa huweza kusababishwa na ongezeko la homoni za kiume kwa mtoto wa
kike au za kike kwa mtoto wa kiume wakati akiwa tumboni mwa mama yake.
Hali hiyo husababisha
muonekano wa viungo vya nje na tabia visiendane na viungo vya uzazi vya ndani
na aina ya jinsia kwenye vinasaba.
“Kwa kawaida jinsia ya
mtoto hutegemea ile mbegu ya baba imebeba vinasaba vya kike au vya kiume,”
anasema Profesa Sten Drop wa Netherlands.
Anasema jinsia ya mtu
hutokea mara tu baada ya mimba kutungwa, hata hivyo viungo vya ndani na vya nje
vya uzazi hutegemea homoni ambazo zimebebwa kwenye vinasaba.
Prof. Drop anasema ikiwa
itatokea hitilafu yoyote katika vinasaba hupelekea homoni hizo kushindwa
kufanya kazi yake vizuri.
“Hali hiyo husababisha
kutotengenezwa au kutengenezwa jinsia zote mbili kwa mtoto aliyepo tumboni mwa
mama,” anasema.
Visababishi
Dk.
Bokhari anasema hadi sasa bado haijulikani nini hasa husababisha kutokea kwa
hitilafu katika vinasaba na hivyo kupelekea mtoto kuzaliwa na tatizo hilo.
“Lakini
kuna visababishi ambavyo huweza kuchangia mtoto kuzaliwa na tatizo hili, hasa
magonjwa ambayo mama huugua kipindi cha ujauzito na anapokosa virutubisho
muhimu kipindi cha ujauzito,
“Kiujumla
afya ya mama ni jambo la msingi mno ili kumuepusha mtoto kuzaliwa na tatizo
hili, mama akiwa na afya duni huchangia kwa kiwango kikubwa uwezekano wa mtoto
kuzaliwa na tatizo tata,” anabainisha.
Hali
ilivyo MNH
Dk.
Bokhari anasema kila mwezi hupokea watu watano hadi sita wanaokabiliwa na
tatizo hilo katika kliniki yake.
“Muhimbili
ni hospitali kubwa ya rufaa hivyo wagonjwa hao hutoka katika mikoa mbalimbali
nchi nzima lakini changamoto ni kwamba huja wakiwa wamechelewa mno,” anasema.
“Tumeshapokea
watoto wenye umri wa miaka mitatu, saba, nane na hivi karibuni tumepokea kijana
mwenye miaka 29 ambaye amelelewa miaka yote hiyo kama mtoto wa kiume na tayari
ana mpenzi wake na wanatarajia kufunga ndoa.
“Lakini
mpaka amechukua hatua kuja hospitalini ni baada ya kuona anapatwa na hali
tofauti na wavulana wengine, alishangaa kuona anapata hedhi hali ambayo
kwa kawaida huwapata wanawake,” anasema.
Anasema
walimfanyia uchunguzi kwa vipimo vya kibingwa ambavyo vilionesha ndani ya mwili
wake kuna mfumo wa uzazi wa mwanamke na hana kabisa mfumo wa uzazi wa mwanaume.
“Kijana
huyo ana uterasi (tumbo la uzazi), mirija yote miwili na vifuko vya mayai
anavyo na tuliona kuna yai lilikuwa limeshapevuka tayari kupata hedhi,” anasema.
Athari
zinazowakabili
Prof. Drop anasema watu
waliozaliwa na tatizo hilo wanapokuja kugundulika ukubwani wengi hupatwa na
matatizo ya kisaikolojia.
“Hukosa raha, wengi
hutafakari namna ambavyo jamii itawanyanyapaa pindi itakapojua kuhusu tatizo
lao, huwa na mawazo mengine mno, huhitaji ushauri nasaha kila wakati,” anasema.
Anasema hata wazazi
waliopata mtoto mwenye tatizo la jinsia mbili huwa katika wakati mgumu.
“Kwa sababu wanakuwa
wanajua mtoto wao labda ni wa kiume lakini vipimo vinaonesha ni wa kike, au wa
kike lakini vipimo vinaonesha ni wa kiume.
“Hivyo hujiuliza maswali
mengi hasa namna gani watamtuza mtoto wao kulingana na majibu ya vipimo huku
jamii inayomzunguka ikifahamu kinyume chake,” anasema.
Anasema hata hivyo ni
muhimu mno kwa wazazi kuwahi kumpeleka mtoto hospitalini kwa uchunguzi pindi tu
wanapobaini kasoro.
“Katika nchi zilizoendelea
tatizo hili hugundulika mapema na watoto wa aina hii hupewa matibabu mapema
lakini naona hali ni tofauti katika nchi zinazoendelea,” anasema.
Dk. Bokhari anasema
kutokana na uelewa mdogo juu ya tatizo hilo ni kweli kwamba watoto wengi
hufikishwa hospitalini wakati umri ukiwa umekwenda.
“Ni changamoto ambayo
tunaiona tofauti na wenzetu wa nchi zilizoendelea wao wanawahi kugundua na
wanatibiwa mapema,” anasema.
Kutokukubali
matokeo
Anasema zipo jamii zingine
ambazo hukataa kukubali matokeo ya vipimo vya kitaalamu kuhusu watoto wao.
“Kwa mfanao yupo mama
mmoja, mtoto wake alichunguzwa hospitalini tangu siku alipozaliwa na madaktari
walimueleza ana tatizo hili.
“Kadiri alivyokua yule mtoto
alionekana kuwa na mwonekano wa mtoto wa kiume lakini jinsia ya kike, yule mama
alikuwa akimlea kama mtoto wa kike.
“Lakini kipindi fulani
ikabidi aende kijijini kuwasalimia wazee alipofika huko wale wazee walihoji
kwanini anamlea mtoto kama wa kike wakati ni wa kiume.
“Wakamshinikiza amlee
kulingana na malezi ya mtoto wa kiume na si wa kike, ikabidi afanye hivyo hadi
aliporejea mjini na akaja hapa Muhimbili.
“Tukamchunguza tena mtoto
vipimo vikaonesha ni wa kike ila mwonekano wake ni wa kiume, kwa hali ya namna
hiyo moja kwa moja wazazi huathirika kisaikolojia.
“Yupo pia mama mwingine
ambaye nimempa ushauri nasaha na kumfanya kuwa rafiki yangu ili niwe naye
karibu zaidi, nikimshauri asijisikie vibaya kuwa na mtoto wa aina hiyo,”
anasema.
Je
tiba ipo?
Prof.
Drop anasema tatizo hilo linatibika kwa njia ya upasuaji na kwamba matibabu
hayo huhusisha jopo la madaktari pamoja na wataalamu wa saikolojia.
“Lakini
hutegemea hatua za tatizo ila ni muhimu wazazi kupatiwa ushauri wa kisaikolojia
ili waweze kukabiliana na hali ya wasiwasi wanaoweza kuwa nao na kuwasihi kuwa
wavumilivu kipindi cha kusubiri majibu ya vipimo,” anasema.
Anaongeza “Madhara makubwa
yanawapata hasa pale ambapo inabidi kubadili utambulisho wa jinsia ili kuendana
na muonekano wao.
Dk. Bokhari anasema sheria
inawapa ruhusa madaktari nchini kufanya upasuaji dhidi ya tatizo hilo.
“Hairuhusiwi kubadili
jinsia kama vipimo vya uchunguzi havijaonesha muhusika ana tatizo, lakini hata
kama mtu ana tatizo inabidi familia iliridhie kama ni mtoto.
“Na ikiwa ni mtu mzima japo
tutamshauri lakini anaweza mwenyewe kuamua anataka kufanyiwa au la,”
anabainisha.
Anasema
hata hivyo wengi hushindwa kufanya maamuzi kwa kuhofia unyanyapaa
watakaofanyiwa kwenye jamii pale itakapogundulika kuwa walizaliwa na jinsia
tata.
Kuhama
mazingira
Anasema wakati mwingine
hasa baada ya upasuaji hushauri wahusika kuhama au kuhamishiwa kwenda kuishi
katika mazingira mengine tofauti na aliyokulia.
“Hii ni sehemu ya matibabu,
kwa mfano kuna watoto wawili ambao tuliwagundua kuwa na jinsia tata, tukawatibu
sasa ili kuwaepusha na ule unyanyapaa kutoka kwa jamii na wanafunzi wenzao
tuliwashauri wazazi wao wawahamishe katika mazingira mengine.
“Hivyo waliwahamisha shule
na hata makazi walihama,” anabainisha.
Anatoa
rai kwa wataalamu wenzake wa afya hasa wauguzi, wakunga na madaktari kuwakagua
kwa makini watoto baada ya kuzaliwa.
“Kiutaratibu
baada ya mama kuoneshwa, wanatakiwa kumkagua mtoto kuanzia utosi hadi unyayo
wake kujiridhisha amezaliwa salama au la, na wanapoona kasoro wampe mama rufaa
ili akasaidiwe na wataalamu waliobobea zaidi,” anasema.
Anasema
ni rahisi pia kwa mama kumkagua mtoto wake kwa kulinganisha maumbile yake ya
kwake ikiwa ni wa kike au ya baba yake ikiwa ni wa kiume.
“Hata
kama yatatofautiana ukubwa lakini ikiwa kuna kasoro atabaini tu, ni vema
akibaini amuwahishe hospitalini,” anatoa rai.
Muhimu
Tatizo hilo huweza
kurithiwa kwenye familia kwa sababu hutokana na hitilafu kwenye vinasaba.
Hivyo ni vizuri kujua kama
kwenye familia kuna historia ya tatizo la jinsia tata au la.
Jambo jingine muhimu ni
kujua iwapo mzazi mmojawapo ana tatizo la kimaumbile kwenye viungo vya uzazi.
Ni muhimu kujua iwapo
mmojawapo ana historia ya kuchelewa kubalehe au kutopata hedhi mara kwa mara na
mambo mengineyo.
Chapisha Maoni