Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Image result for moyo wa binadamu\
Katika awamu ya kwanza makala haya yaliishia hapa kwa Dk. Pallangyo ikieleza utafiti alioufanya kwa wagonjwa wa moyo. Sasa endelelea...

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

Pedro Pallangyo ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye hivi karibuni amefanya utafiti kujua hali halisi na changamoto zinazowakabili wagonjwa wa moyo nchini.

Akizungumza Pedro anasema  magonjwa ya moyo nayo ni miongoni mwa magonjwa yaliyopo katika kundi la magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Anasema utafiti alioufanya ulihusisha wagonjwa 459 waliokuwa na umri wa kati ya miaka 46 na kuendelea na kwamba asilimia 57 walikuwa wanawake huku asilimia 43 ni wanaume.

“Kati ya wagonjwa hao asilimia 68 walikuwa wakiishi katika maeneo ya mijini, nilibaini asilimia 80 ya wagonjwa walikuwa na matumizi mabaya ya dawa, asilimia 22 tu ndiyo walikuwa na bima ya afya,” anasema.

Dk. Pallangyo anasema kwa kawaida wagonjwa wanaotibiwa  hospitalini hapo hupatiwa dawa zinazostahili kutibu magonjwa ya moyo yanayowakabili.

“Nilibaini tunapowalaza wodini huzingatia matumizi mazuri ya dawa na hali zao huimarika lakini baadhi yao tunapowapa rufaa kurejea nyumbani huwa wana matumizi mabaya ya dawa hali inayosababisha wengi kurejeshwa hospitalini wakiwa na hali mbaya.

“Matokeo yake, kama wana tatizo la moyo kushindwa kufanya kazi, wakilazwa hospitalini huwa na hali nzuri lakini wakirudi nyumbani hali hubadilika na kuwa mbaya kuliko awali kwa sababu hawatumii dawa ipasavyo,” anasema.

Chanzo gharama

Dk. Pedro anasema matokeo ya utafiti huo yalibainisha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa waliohojiwa walieleza sababu kubwa iliyowapelekea kuacha kuzingatia matumizi ya dawa ni kukosa fedha za kununulia dawa hizo.

“Walisema dawa ni ghali kuzinunua, ingawa zipo pia sababu nyinginezo tulizobaini ikiwamo usahaulifu ambapo ilikuwa ni asilimia 53.9, asilimia 34.4 waliacha matumizi ya dawa kutokana na ule wingi wa dawa walizopewa waliamua kuzipungua na asilimia 26 waliacha matumizi kutokana na uzembe,” anasema.

Anasema kutokana na matokeo ya utafiti huo inaonesha wazi kiujumla hayawezi kuleta matokeo chanya kwa asilimia 100 katika kumtibu mgonjwa wa moyo.

“Tulijaribu kuangalia kigezo cha umri kwamba labda ilikuwa ni miongoni mwa mambo yaliyochangia hali hiyo, tulibaini haukuwa tatizo.

“Lakini kwa upande wa elimu tulibaini kulikuwa na tatizo, wagonjwa waliokuwa na kiwango kidogo cha elimu (Msingi kushuka chini) walikuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa ikilinganishwa na wale waliokuwa na kiwango cha Elimu ya Msingi na kuendelea,” anabainisha.

Ukosefu wa ajira

Anaongeza “Tuliangalia kigezo cha ajira tulibaini wale ambao hawakuwa na ajira ya kuwaingizia kipato walikuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa kuliko wale waliokuwa na ajira za kueleweka.

“Matokeo yalionesha pia waliokuwa wanaishi maeneo ya vijijini walikuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa ikilinganishwa na wale wanaoishi maeneo ya mijini.

Anasema wagonjwa ambao hawakuwa na bima ya afya walikuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa mara nne zaidi ya wale ambao walikuwa na bima ya afya.

“Kwa hiyo, tukaainisha vigezo vya msingi katika utafiti huo ambavyo vilichangia hali hiyo ni elimu duni, tatizo la ajira, hali ya kijiografia na suala la bima ya afya,” anasema Daktari huyo ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya watafiti vijana Barani Afrika, mwaka 2017.

‘Ni sawa na kuchungulia kaburi’

Dk. Pallangyo anasema katika utafiti huo walienda mbali zaidi na kuangalia maendeleo ya wagonjwa waliolazwa mara kadhaa baada ya mahojiano ya awali.

“Tulibaini baada ya mahojiano ya awali, wagonjwa ambao  hawazingatii matumizi ya dawa kama walivyotakiwa wana uwezekano wa kulazwa mara kwa mara huwa ni asilimia 70 kuliko wale ambao huzingatia,” anasema.

Anaongeza “Matokeo yanaonesha pia wagonjwa ambao huwa na uzingatiaji mbaya wa matumizi ya dawa hali inayopelekea kulazwa mara kwa mara hospitalini wapo kwenye hatari ya kufariki dunia mara tatu zaidi ya
wale wanaozingatia matumizi sahihi ya dawa.

“Hii tuliibaini baada ya kuwafuatilia kwa ukaribu wagonjwa hao ambapo kati yao walikuwapo ambao walipoteza maisha ndani ya miezi sita ya utafiti huu,” anasema.

Dk. Pallangyo anasema kutokana na matokeo ya utafiti huo inawezekana kutokuzingatia matumizi sahihi ya dawa huenda ni sababu inayochangia vifo vya wagonjwa wengi hadi wale wanaokabiliwa na magonjwa mengineyo.

Umasikini

Daktari huyo anasema jamii nyingi bado ni masikini huenda hali hiyo inachangia pia kuwapo uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa.

“Kusema ule ukweli bado wananchi hawawezi kumudu gharama  za kutibu magonjwa yasiyo kuwa ya kuambukiza,” anabainisha..

Anasema walitumia ‘tool’ ya Morsw (kipimo cha kitaalamu) kinachoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kufanya tafiti za namna hiyo.
Image result for figo ya binadamu\

Figo ‘hutafuna’ mamilioni

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile anasema gharama za kutibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni kubwa.

“Kila mwaka serikali imekuwa ikipelekea nje ya nchi wagonjwa 35 wanaohitaji huduma ya kupandikizwa figo pekee ambapo hutumia kati ya Sh. milioni 70 hadi 75 kwa kila mgonjwa mmoja,” anabainisha.

Anasema hapa nchini, mgonjwa mmoja wa figo huhitaji wastani wa Sh. milioni 37 kwa ajili ya kulipia huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na kwamba hulazimika kusafiri wastani wa safari 126 kwa mwaka sawa na safari tatu hadi nne kila wiki kufuata huduma hiyo hospitalini.

“Kutokana na hali hiyo, sasa serikali imeona vema kuimarisha Idara ya Magonjwa ya Figo Muhimbili kwani kwa kupandikiza mgonjwa mmoja wa figo nchini tunagharamia kiasi cha wastani wa Sh. milioni 20.

“Huwa wanahitaji ‘section’ tatu hadi nne kwa wiki, NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya)  wamepiga hesabu tunatumia kati ya Sh milioni 37 kwa mtu mmoja kwa mwaka na wagonjwa wanafikia kiasi cha 1000 hivyo kwa mwaka inatumika kama zaidi ya Sh  bilioni 3.7 na hapo bado hatujagusa magonjwa mengine,” anabainisha.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa MNH, Jaqueline Shoo anasema takwimu zinaonesha tatizo linaendelea kuwa kubwa duniani.

Anasema takwimu zinaonesha asilimia 10 ya watu duniani tayari wanaugua ugonjwa sugu wa figo na kwamba inakadiriwa ifikapo 2025 asilimia 70 ya wagonjwa watakuwa wanatokea katika nchi zilizopo katika ukanda wa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.

Anasema katika kliniki yao wanaona wagonjwa wengi kila mwezi wakiwamo watoto ambao huwa ni kati ya asilimia30 hadi 40.

Anasema kati ya wagonjwa wanaowapokea kila mwezi watu wazima huwa ni kati ya 120 hadi 150.

“Tangu mwaka 2006 hadi 2017 zaidi ya wagonjwa 220 wamepandikizwa figo na hali zao zinaendelea vizuri, wagonjwa wapatao 132 tunawafanyia  ‘dialysis’.

“Asilimia 50 kati ya hawa wapo kwenye mchakato wa kupandikiza figo, wanatafuta watu watakaowasaidia kupata figo ya kupandikizwa,” anasema.

Anaongeza “mwaka 2011 WHO ilieleza kwamba watanzania wapatao 4,300 hugundulika kuwa wanaugua magonjwa ya figo kila mwaka.

“Na kati yao wengi wanafariki kwa sababu ya magonjwa ya moyo (yanahusiana na magonjwa ya figo), ndiyo maana tunaona kuna umuhimu wa kuelimisha jamii kupambana kupunguza visababishi vinavyochangia mtu kupata magonjwa haya hasa unene uliokithiri,” anasema.

Anaongeza “Takwimu za WHO zinaonesha watu wapatao milioni 600 duniani wameathirika na unene uliokithiri (wengi wana vitambi au viriba-tumbo).

Denis Mbinga ni Mtaalamu wa Lishe wa Muhimbili anasema utafiti uliofanyika hospitalini hapo, mwaka 2017 katika Maadhimisho ya Wiki ya Lishe unaonesha asilimia 39.9 ya watu ambao walijitokeza kupima afya zao walikutwa na uzito uliokithiri (obesity) na asilimia 29.5 walikutwa na uzito mkubwa (over weight).

Anasema uzito mkubwa ni miongoni mwa mambo yanayochochea watu kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo hayo ya figo, moyo, saratani na mengineyo.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa Muhimbili, Onesmo Kissanga anasema zaidi ya wagonjwa 50 hivi sasa wanasubiri huduma ya kupandikizwa figo.

“Takwimu zinaonesha idadi ya watu wanaougua magonjwa ya figo nchini inaongezeka, katika kitengo chetu tunahudumia wagonjwa wapatao 200 ambao  wanafanyiwa dialysis,” anasema.

Anasema asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa hao wanahitaji huduma ya kupandikiza figo ambayo ni bora zaidi kuliko ile ya kuchuja damu katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement