Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
Na Veronica Romwald,  Dar es Salaam

ASILIMIA 40 ya watoto wenye saratani ya jicho (Retinoblastoma) hupona kabisa baada ya kupatiwa matibabu. 

Hata hivyo changamoto ni kwamba asilimia 85 hufikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa na ugonjwa ukiwa umeshaanza kusambaa. 

Hayo yameelezwa Dar es Salaam leo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kwa Watoto wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Anna Sanyiwa.

"Kutokana na hali hiyo vifo hutokea kwa kiwango cha asilimia 50 tofauti na nchi zilizoendelea ambako kwa kuwa hugundulika mapema uwezekano wa kupona ni zaidi ya asilimia 90, amesema. 

Awali akitoa tamko  kuhusu wiki ya maadhimisho ya saratani ya macho kwa watoto kwa niaba ya Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi amesema jumla ya watoto137 wenye saratani ya jicho (Retinoblastoma) wameonwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa mwaka 2017.

Amesema kati ya watoto hao 80 hadi 100 hupewa rufaa na kufika kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wengine hutibiwa KCMC Moshi.

Amewataka watumishi wa afya wa ngazi ya jamii, zahanati , vituo vya afya vya na hospitali za kliniki za mama na mtoto za wilaya kuhakikisha wanawachunguza watoto uakisi wa mwanga kwenye mboni zao kila wanapopelekwa kliniki kufuatiliwa maendeleo ya ukuaji wao ili kupunguza uwepo wa saratani ya macho kwa watoto.

“Iwapo mtoa huduma za afya unahisi kuwa mtoto ana tatizo kwenye jicho usimrudishe nyumbani hadi uhakikishe mtoto huyo ameonwa na mtaalamu wa macho ili kugundua kama ana tatizo kwenye macho yake” amesema Prof. Kambi.

Prof. Kambi amesema katika kuboresha huduma hizo Wizara imeandaa mwongozo ambao utasaidia kuinua uelewa wa wataalamu wa afya ili waweze kuwatambua watoto wenye tatizo hilo na kuwapa rufaa mapema.

Naye  Kaimu Mkurugenzi  wa mpango wa Macho wizara ya Afya Dk. Benadertha Shilio amewashukuru wadau wote wa macho ambao wamekuwa bega kwa bega na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha kuboresha huduma za macho kwa watoto.

“Tunawashukuru Rotary Club ya Dar es salaam Oysterbay wakishirikiana na Rotary Club ya Chelsea nchini Uingereza ambao wametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya kutibu Saratani ya macho vinavyogharimu kiasi cha Dola za Kimarekani 65,000 na Kampuni ya Pricewaterhouse ya Tanzania ambayo imetoa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 25 ambavyo vimesambazwa Muhimbili na Mloganzila” amesema Dk.
Shilio.

Maadhimisho ya Wiki ya Saratani ya Macho kwa watoto kwa mwaka 2018 imebeba kauli mbiu isemayo “MBONI NYEUPE KWENYE JICHO LA MTOTO INAWEZA KUWA SARATANI YA MACHO”.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement