Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema - Dar es Salaam

“Si mchezo kuishi na saratani, inahitaji kujifariji mwenyewe, usitarajie kuna mtu atakuja kukufariji, unapaswa kumuomba Mungu akusaidie na lazima uwasikilize wataalamu wa afya kile wanachokuelekeza ili uweze kuishinda,” anasema Halima Mwaipopo, Mkazi wa Masasi, Mkoani Mtwara.

Halima, mama wa watoto watatu ni miongoni mwa wagonjwa waliotibiwa na kupona saratani ya matiti katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

“Ni miaka 18 sasa tangu nilipogundulika nina saratani hii mnamo 2002, nimepambana nayo, nimepona, lakini kwa kuwa wataalamu wanasema saratani ina tabia ya kurudi, ndiyo maana bado naendelea kukuhudhuria kliniki Ocean Road,” anasema.

Anaongeza “Mimi ni shujaa wa saratani, nimeishinda, mimi ni malkia wa nguvu, najiamini, ukiwa na saratani unyanyapaa ni mkubwa mno, kwa ndugu, jamaa, marafiki na wakati mwingine hata wauguzi wapo baadhi wanaweza kukupita tu, ukihangaika mwenyewe kitandani, sielewi ni kubana na majukumu ya kazi au vipi!.

“Tunashukuru Mungu Ocean Road ya sasa si kama ile ya zamani, tulikuwa tunapiga kwata hapa, asubuhi hadi jioni bado mtu hujapata matibabu, nilivumilia.

“Nashukuru watoto wangu sasa wamekua wakubwa, mwanangu aliyekuwa na miaka minne niliyembeba na kwenda naye  hospitalini kuchukua majibu ya kipimo changu, kule Masasi, sasa amemaliza chuo, amejiajiri na mimi bado napambana na saratani (isinirudie tena).

“Kikubwa ni kupokea tatizo ukikutwa nalo, likubali, usiseme kwanini mimi sema asante Mungu, jifariji mwenyewe, usitarajie kuna mtu atakufariji, hapana.

“Endelea kufanya kile unachokipenda, jichanganye, ukihisi tofauti mwilini mwako rudi hospitalini, mueleze daktari wako, atakusaidia.

“Watanzania tusidanganyane, dawa za kienyeji, tusipotezane kwa waganga wala kwenye maombezi, tufuate masharti tunayoelekezwa na madaktari, tule nini, tufanye mazoezi, tusisikilize watu ambao hawajui kinachoendelea kuhusu ugonjwa wa saratani,” anasisitiza.

“Nilipokatwa ziwa mwanangu wa mwisho alikuwa ameshaacha kunyonya, mume wangu tulishatengana japo alikuwa bado anakuja kutusalimia.

“Jamii haikunielewa, nilipopita njiani, walinisema mwanamke yule hana ziwa moja, wapo walioniuliza kwanini nilikubali kukatwa, nilijibu ni mapenzi ya Mungu, ndiye aliyenichagulia.

Anaongeza “Nimeishinda saratani, sasa situmii tena dawa, nimepangiwa kurudi kliniki kila baada ya miaka miwili, wanaangalia maendeleo yangu.

ALIPAPASA ZIWA

Anasimulia jinsi alivyotilia shaka ziwa lake baada ya kulipapasa siku moja, mwaka 2002 saa chache zikiwa zimepita tangu aliposikiliza kipindi maalum kilichorushwa katika redio moja, kiliitwa Ocean Road Leo.

“Nilikuwa nimetoka kazini siku hiyo, nilipofika tu nyumbani, nilifungua redio, katika kipindi hicho, alikuwa anazungumza Dk. Ngoma.

“Nilikaa, nilimsikiliza kwa umakini mno, nilikuta kipindi kipo katikati, alianza kufundisha jinsi mwanamke anavyoweza kujigundua kama ana saratani ya matiti.

“Alituelekeza jinsi ya kujikagua, siku ile baada ya kusikiliza, ilibidi nikafanye vile vile alivyotuelekeza, nililala chali, niliweka mkono wa kulia nyuma ya kichwa, nikalipapasa ziwa langu la kushoto, nilipomaliza nilihamia ziwa la kulia vivyo hivyo,” anasimulia.

Halima anaongeza “Katika ziwa la kushoto hakukuwa na kitu nilichotilia shaka, lakini nilipohamia katika ziwa la kulia, nilipolipapasa nilihisi lilikuwa na kiuvimbe.

“Sikuwa nahisi maumivu yoyote, nilipokwenda kulala usiku, nilijikagua tena, ziwa la kushoto lilikuwa sawa, la kulia nilikuta kile kiuvimbe bado kipo.

“Nilianza kujiuliza ni kiuvimbe cha kawaida au ndiyo saratani kama Dk. Ngoma alivyosema!?, nililala… kulipokucha, nilijiandaa na kwenda ofisini, niliomba ruhusa, nilijieleza ni mgonjwa nahitaji kwenda hospitalini, niliruhusiwa.

“Nilikwenda Hospitali ya Wilaya, walinikagua na kusema ni uvimbe wa kawaida, sikukubaliana nao. Nilipotoka hapo nilienda tena Hospitali ya Ndanda, nilikutana na Daktari (anamtaja/ sasa ni marehemu), aliniuliza swali, kwanini nafikiri kauvimbe kale ni saratani, nilimueleza kwa sababu nilimsikiliza daktari kwenye redio.

“Kwa hiyo, nataka nihakikishe afya yangu, kama ni ka kawaida au saratani, ikigundulika ni saratani basi katolewe mapema,” anasema.

Halima (Pichani chini) anasema Daktari alikubaliana naye, alimchukua sampuli ya kinyama, ilisafirishwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na katika hospitali moja huko Ujerumani.

LILIZIDI KUVIMBA

“Nilipokatwa kile kinyama, ziwa lilizidi kuvimba, nilikumbuka Dk. Ngoma alivyokuwa akieleza redioni kwamba hii nayo ni miongoni mwa dalili kwamba si kaumvimbe ka kawaida bali saratani, nikaanza kuhisi … ahaaa… itakuwa saratani.

“Majibu ya sampuli iliyopelekwa Muhimbili na Ujerumani yaliwahi kurudi, nilipigiwa simu niende kuyachukua, nilijipa moyo, maana nilikuwa na watoto wadogo, nawalea mwenyewe, nilitengana na mume wangu. 

“Kwa hiyo, sikutaka kukata tamaa, kila nilipowaangalia wanangu kama mama nilihisi roho inaniuma, nilienda hospitali nikiwa nimembeba mwanangu wa mwisho, wakati ule alikuwa na miaka minne.

Anasema Daktari alipomuona alisita kumpatia majibu ya vipimo vyake, wakati ule walikuwa wanataka ndugu wa karibu wa mgonjwa aende apatiwe majibu.

“Mimi nilikwenda mwenyewe, walipata wasiwasi watanielezaje, nilivaa ujasiri, niliwaambia pale hospitalini, mimi ndiye mgonjwa, wanieleze maana hata kama atakwenda ndugu yangu, hataweza kunisaidia kwa lolote.

“Nilipewa majibu yangu kwamba nina saratani, natakiwa kwenda Ocean Road, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, kwa kweli binadamu kupokea tatizo ni changamoto, lakini binafsi nililipokea.

“Nilisafiri hadi Ocean Road, bahati nzuri nilikutana na Dk. Ngoma mwenyewe, aliniambia nilipaswa kupata matibabu ya aina mbili, mionzi na kukatwa ziwa lililoathiriwa na saratani.

“Aliniambia Ocean Road wanatoa huduma ya tiba mionzi lakini kukatwa ziwa nilipaswa kwenda kwanza Muhimbili, alinishauri nikate ziwa ili niwe huru,” anasimulia.

Anaongeza “Ofisini walinifanyia mpango, nashukuru uongozi ulinielewa na kunisaidia fedha za matibabu yangu, nilikuwa 'customer care' katika Benki ya NMB, nilisafiri hadi Dar es Salaam, Hospitali ya Taifa Muhimbili.

HOFU ILIMUANDAMA

“Nilipofika Muhimbili, changamoto niliyoipata nilipolazwa wodini, nilikuta wanawake wawili waliofanyiwa upasuaji wa saratani ya titi, walifariki dunia, kwa kweli nilishtushwa na taarifa ile.

“Ndugu zangu nilioambatana nao siku ile nao walishtuka, wakaniuliza itakuwaje?... siku ya upasuaji ilipowadia, waligoma kuondoka, walikuwa wanalia,” anasimulia.

Halima anasema ilibidi daktari atumie mbinu kuwaondoa, aliwaeleza upasuaji utafanyika saa tisa jioni, lakini ukweli ilikuwa mbinu tu ya kuwaondoa, walipokubali kuondoka, nilichukuliwa na kupelekwa chumba cha upasuaji.

“Ilikuwa Desemba 2002, kulikuwa na mgomo wa madaktari kipindi hicho, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu nilifanyiwa upasuaji kwa mafanikio.

Anasema ndugu zake waliporudi mchana, walidhani bado hajaingizwa chumba cha upasuaji, kumbe la hasha! Tayari alikuwa ameshafanyiwa na kurudishwa wodini.

“Fahamu zilikuwa zimeshanirudia, nilikuwa nawaita majina waliita, walipoambiwa nimshafanyiwa upasuaji kuondoa titi lile, ghafla walianza tena kulia.

“Walilia mno, niliwauliza kuna msiba!!?, basi manesi ilibidi wawatoe, wasinisumbue, niliwasihi wasilie tena, nimeshafanyiwa upasuaji, niko salama kabisa,” anasimulia akitabasamu.


IMANI POTOFU

Halima anasema hatimaye aliruhusiwa kutoka Muhimbili na kurudi Ocean Road kwenda kuanza tiba ya mionzi (radiotherapy) na ile ya kemia (chemotherapy), mwaka 2003.

“Wakati ule dawa za saratani ilikuwa mtihani, tulitakiwa kuzinunua wenyewe, si kama sasa hivi zinapatikana hospitalini, Serikali imefanya kazi kubwa, basi ilibidi niwasiliane na ofisi, walinisaidia kulipia gharama za dawa.

Anasema wakati yupo kwenye matibabu, ndugu na jamaa walikuwa wanasema hataweza kupona, kwa sababu watu husema yeyote anayeugua saratani huishia kupoteza maisha.

“Wengine walinishawishi niachane na matibabu ya hospitali, niende kwa waganga wa kienyeji kwamba nimerogwa, sikukubaliana nao.

“Niliendelea kufuatilia maelekezo ya daktari, nile nini, nifanye nini, mwenyewe niliamua kupunguza kula nyama nyekundu maana nilishasikia nyama nyekundu, zenye mafuta mafuta, niliamua kula samaki, kunde, mboga za majani, nilikuwa nalia sana, nikimuomba Mungu anisaidie watoto wangu wakue, maana najua kifo tumeumbiwa binadamu,” anasimulia Halima ambaye kwa sasa ni mstaafu na ameajiajiri, mkulima wa zao la korosho na mjasiriamali wa bidhaa hiyo.

HALI HALISI TANZANIA

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa anasema kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Globalcan za 2018, inakadiriwa zaidi ya wagonjwa 42,060 wa saratani wanaogundulika kila mwaka Tanzania, asilimia 7.2 kati ya hao ni wa saratani ya matiti.

“Katika uhalisia, takwimu zetu nchini zinaonesha mwaka 2018 wagonjwa wa saratani walioweza kuhudhuria hospitalini ni zaidi ya 12,215 kati ya hao 42,060 wanaokadiriwa.

“Kati ya hao 12,215 walioweza kuhudhuria wanawake waliopata saratani ya matiti walichukua wastani wa asilimia 16 ya wagonjwa wote.

Dk. Kahesa anasema takwimu zao zinaonesha saratani ya matiti ni tatizo kubwa ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa, baada ya saratani ya kizazi na saratani ya tezidume.

“Wastani wa umri wa wanawake wanaogundulika kuugua hii ORCI umeshuka, takwimu zetu zinaonesha mwaka 2008/09 wanawake waliokutwa wakiugua walianzia miaka 64 lakini mwaka 2019 walianzia miaka 56 na wapo hadi wenye umri wa miaka 25 wamegundulika.

Anasema takwimu hizo zinaonesha wazi hali hiyo ni kiashiria cha hatari kwamba saratani hiyo sasa imeanza kushambulia hadi wanawake wenye umri mdogo tofauti na miaka ya nyuma.

Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage anasema “Ni saratani inayoongezeka kwa kasi nchini. Miaka 10 iliyopita ilikuwa inashika nafasi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa hapa ORCI sasa hivi inashika nafasi ya pili.

“Changamoto tunayoiona hivi sasa kwenye jamii ni wimbi la taarifa potofu zilizopo kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wagonjwa hushawishiwa kwenda kupata dawa za kienyeji ambazo hata hazijafanyiwa utafiti na hivyo huacha tiba za hospitalini.

“Hatujafanya utafiti kamili ila tunakadiria asilimia 10 ya wagonjwa wa saratani zote tunaowatibu hukacha matibabu, huondoka wodini na kwenda kwa waganga wa kienyeji au kwenye maombezi.

“Wengine hupoteza maisha huko na wale wachache wanaorudi ugonjwa huwa upo hatua za juu, tiba huwa ngumu, wanapoteza maisha,” anabainisha.

Anaongeza “Tunasisitiza wazingatie matibabu, hata wakienda huko, wasiache matibabu, Serikali inazidi kuboresha huduma, sasa tunao uwezo wa kuigundua mapema na kuitibu pasipo kuondoa titi lote, ikiwa mtu atagundulika mapema.

“Kila mwaka tunatibu kwa njia hii ya upasuaji pasipo kuondoa titi lote, wanawake 100 ikiwa ni sawa na asilimia 30 ya wagonjwa wote tunaowatibu, tunayo.

“Hata wale waliofanyiwa upasuaji na kuondolewa katika titi lote jitihada zinafanyika, wataalamu wetu wapo China wakijifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kupandikiza matiti, walikuwa wawe wameshamaliza masomo yao na kurejea nchini tayari kuanzisha huduma hii, Corona imetuchelewesha,” anasisitiza.

SHUJAA MWINGINE

Anna Migila naye ni miongoni mwa mashujaa walioishinda saratani ya matiti, anayeendelea kuhudhuria kliniki Ocean Road kufuatiliwa maendeleo ya hali yake.

“Kweli unyanyapaa upo kwa kiwango kikubwa kwenye jamii dhidi ya watu wanaokabiliwa na ugonjwa wa saratani, niwasisitize tu wenzangu ambao wanapitia changamoto hii, wasikate tamaa, wazingatie yote wanayoelekezwa na wataalamu, ipo siku wataishinda, kama sisi tulivyoishinda,” anasisitiza.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement