Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Miaka 10 iliyopita ilikuwa nadra wataalamu mabingwa wa magonjwa ya saratani nchini kubaini wagonjwa wenye umri mdogo wanaokabiliwa na saratani ya matiti, wengi waliogundulika ni wale wenye umri mkubwa zaidi.

Lakini sasa ‘shilingi’ imepinduka, baadhi ya wasichana wenye umri mdogo waliofanyiwa uchunguzi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), wamekutwa wanaugua saratani hiyo.

Takwimu halisi za ORCI zinaeleza wastani wa umri umeshuka kutoka miaka 64 ilivyokuwa mwaka 2008/09 hadi miaka 56 mwaka 2019, ikielezwa wapo pia wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 25 waliobainika.

Katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG hivi karibuni, Daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Kandali Samwel, anasema miongoni mwa wasichana waliobainika walipowahoji walieleza kwamba wamekuwa wakitumia vidonge vya P2 kama vile ‘karanga’.

Dk. Kandali anasema tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani zinaonesha watu wanaotumia holela dawa hizo, zenye vichocheo vya kuharibu mimba, wapo kwenye uwezekano mkubwa kuishia kupata saratani hiyo.

“Pale Ocean Road wapo wasichana wanatueleza wametumia dawa hizo bila ushauri wa daktari, kwa wingi na kwa muda mrefu, tumewakuta na saratani.

“Hivyo, tunapata hizo taarifa, tunatilia maanani na tunaendelea kutoa elimu sahihi ili mbeleni tusije tukapata shida, hii inatufumbua macho na huu ni wito kwa kwa upande wa tafiti tuangalie shida hii ipo kwa kiwango gani kwenye jamii.

“Sisi tunaona tu kama wahudumu watu wanatoa hizi shuhuda, lakini hatuwezi kujua kwa kiwango gani pengine tatizo ni kubwa zaidi, hili linaweza kuletewa majibu na tafiti za kisayansi zaidi.

WASICHANA WAFUNGUKA

MATUKIO NA MAISHA BLOG limefanya mahojiano maalum na baadhi ya vijana hasa wasichana kudadisi kile kilichopo ‘nyuma ya pazia’ ambapo wasichana waliweka wazi siri ya ‘kijiwe’ kinachotumika kuchochea matumizi holela vidonge vya P2 kwa kundi hilo.

“Vijana tunatamani mno kupata elimu kuhusu afya ya uzazi, lakini bado hatujapa fursa hii kwa undani, mimi nimehitimu elimu ya juu hivi karibuni katika chuo kimoja hapa Dar es Salaam, hata kule chuo wengi wetu tulikuwa hatujui.

“Tunaambiana-ambiana tu, basi unachukua ushauri wa huyu na yule unautumia, hatuna ule ujasiri wa kwenda moja kwa moja kuzungumza na daktari, kwa sababu mazingira bado si rafiki kwetu, ndiyo maana tunapotoka,” anasema Selina Ibrahim (22) mhitimu wa elimu ya juu katika chuo kimoja Dar es Salaam (hakupenda kiandikwe).

Selina anasema hata yeye amewahi kutumia dawa za uzazi wa mpango lakini hakwenda kuonana na daktari kupata ushauri wa kina.

“Nilishauriana kwanza na marafiki yangu, sikuwa najua kuhusu hivyo vitu, rafiki yangu mmoja aliniambia nikanunue P2 famasi, nilipokwenda mfamasia pale dukani alinishauri, aliniuzia, nilizitumia, nakumbuka nimeshazitumia mara mbili ndani ya mwaka mmoja,” anasimulia.

USIPOTUMIA MSHAMBA!

Esma Mustafa (25) anasema yupo kwenye mahusiano, miezi sita sasa, yeye na mpenzi wangu waliamua kutumia kondomu kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya ngono, VVU (Virusi Vya Ukimwi) na kuepuka mimba zisizotarajiwa.

“Hatujawahi kutumia njia nyingine za uzazi wa mpango zaidi ya Kondomu, japokuwa nimewahi kushawishiwa na marafiki zangu kwenye ‘grupu’ letu la watsup, hivi karibuni nitumie P2,” anasimulia Esma.

Anaongeza “Si unajua tena mambo ya ‘watsup’ kuna msichana alikuwa anaomba ushauri atumie njia gani na mwenza wake, mimi ‘nika-type’ kondomu inafaa.

“Nilichekwa, wengi ‘wali-type’ kuhusu vidonge vya P2 kwamba ndiyo njia inayofaa, walihoji eti kwanini kula pipi na ganda lake!,” anasimulia Esma na kusisitiza msimamo wake na mwenza wake bado ni kutumia kondomu.

USHAWISHI NI MKUBWA

Christina Steven ni mwana-chuo katika chuo cha Veta – ICT Kipawa, Dar es Salaam anasema ushawishi ni mkubwa hasa katika zama hizi za kukua kwa kasi ya maendeleo ya kiteknolojia tofauti na miaka ya nyuma.

“’Magrupu’ ya watsup yanatuleta vijana wengi kwa pamoja, ni mada ambayo huletwa na kujadiliwa mara kwa mara kwenye ‘grupu’ moja nililopo, kuhusu hizo P2.

“Wengi huwa wanaandika kwamba wanazitumia kujikinga wasipate mimba zisizotarajiwa, si kazi ngumu kuzipata, zipo maduka ya dawa muhimu, zinauzwa,” anasema.

Katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), baadhi ya wasichana wenye umri Kati ya miaka 20 hadi 25 wamekutwa na saratani ya matiti baada ya kufanyiwa uchunguzi, Dk. Kandali (pichani) anasema miongoni mwao walipohojiwa walieleza kwamba huwa wanatumia P2 mithili ya karanga jambo ambalo ni hatari.

Mwandishi wa makala haya, alikwenda hadi huko Mbezi Luis kufanya uchunguzi, katika duka moja la dawa (jina linahifadhiwa), muuzaji ambaye hakupenda jina lake liandikwe katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG, anasema ni kweli baadhi ya wasichana wanashawishiwa kutumia dawa hizo mitandaoni.

“Nimewahi kupokea mteja mmoja hapa, msichana alikuja akaniambia anahitaji P2 kwamba ameelezwa kwenye ‘grupu’ la ‘watsup’ kwamba ndiyo njia inayofaa kwa uzazi wa mpango.

“Ikabidi nianze kumuelewesha, ni muhimu kushauriwa na daktari njia ya kutumia na si tu kujiamulia kutumia, kwa sababu hivi ni vichocheo vinavyoweza kuleta athari endapo vinatumika kiholela,” anasema.

Steven Danford ni kijana anasema hawajawahi kumuona mwenza wake akitumia vidonge hivyo lakini amewahi kusikia ‘washikaji’ zake wakijadili juu ya vidonge hivyo ‘maskani’.

“Mimi nashauri vijana tuwe tunafikishiwa elimu mara kwa mara ikiwezekana wataalamu wawe wanakwenda moja kwa moja vijiweni na kuibua mijadala, mengi yataibuliwa na kutusaidia,” anasema.

Christina anashauri kwamba kwa kuwa tatizo limeanza kuonekana kwa wasichana wenye umri mdogo ni vema kundi hilo likafikiriwa kwa ‘jicho la tatu’ jinsi gani litasaidiwa.

Dk. Kandali anasema kimsingi dawa hizo zinapaswa kutumiwa pale tu dharura inapotokea ndiyo maana zinaitwa kwa kitaalamu ‘emergency contraceptive’, ni kwa ajili ya dharura.

"Tunajua dharura kutokea labda ni mara moja, kwa mfano kwa mtu ambaye anaweza kujamiiana pasipo kutarajia kile kitendo labda amebakwa na sisi wataalamu tunatarajia kitendo hicho si cha mara kwa mara.

“Njia za uzazi wa mpango zina kiwango cha homoni ambazo zinakuwa zimepimwa kwa wakati huo, lakini kumbe jamii wanafanya kuwa matumizi ya mara kwa mara, kwa wingi bila ushauri wa wataalamu, lakini si kuzimeza kama karanga,” anasisitiza.

ASILIMIA 99 WANAWAKE

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa ORCI, Maguha Stephano anasema ingawa jinsi zote wana matiti lakini kwa asilimia 99 huathiri wanawake na wanaume asilimia moja.

“Kuna visababishi mbalimbali vinaweza kuchangia, naweza kuviweka katika makundi mawili, vinavyozuilika na visivyozuilika,” anasema.

Anaongeza “Visivyozuilika ni vile tumezaliwa navyo, ukiwa jinsi ya kike upo kwenye hatari zaidi kuliko jinsi ya kiume. Kurithi pia ni kisababishi kingine ambacho hakizuiliki, kama ndugu wa karibu (wa damu) shangazi, hibi, mama aliwahi kuugua nawe upo hatarini.

Dk. Maguha anasema inashauriwa mwanamke anyonyeshe angalau miaka miwili lakini ikiwa hatanyonyesha kabisa au atanyonyesha kwa kipindi kifupi anakuwa kwenye hatari ya kupata saratani ya matiti.

“Mwili wa mwanamke una homoni iitwayo ‘oestrogen’. Anaponyonyesha kile kiwango cha homoni hii hushuka na hali hiyo humsaidia kumkinga dhidi ya saratani ya matiti kuliko yule asiyenyonyesha,” anafafanua.

Anaongeza “Mwanamke anaponyonyesha kuna faida nyingine pia kwa mtoto kupata virutubisho muhimu kwa ukuaji wa afya ya mwili na akili na ‘kujenga’ ukaribu na mama yake.

Dk. Maguha anasema licha ya kichocheo hicho cha ‘oestrogen’vipo pia visababishi vingine vinavyoweza kuchangia mwanamke kupata saratani hiyo.

“Suala la mtindo mbovu wa maisha, unene uliopitiliza, uzito mkubwa, kutokufanya mazoezi mara kwa mara, kujifungua katika umri mkubwa.

Siku hizi wapo wanaopata hedhi mapema na wengine wanachelewa kukoma, maana yake ni kwamba kiwango kile cha homoni ya eoestrogen huwa kingi kwa wanati mwingi na hivyo kuwa kwenye hatari ya kupata saratani hii,” anabainisha.

Anaongeza “Ndiyo maana tunashauri kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kama mtu ana saratani hii aweze kugundulika na kutibiwa mapema, kwani ikigundulika mapema ni rahisi kutibika na kupona kuliko anapochelewa.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement