moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

MFUMO wa chakula wa binadamu huanzia mdomoni ambako hutafuna chakula husika, hukimeza kupitia kooni na huendelea na ‘safari’ kuelekea katika tumbo la chakula. 

Hapo huchanganywa na kuwa chepesi baada ya hapo huingia kwenye utumbo mdogo ambao huchukua virutubisho vinavyohitajika mwilini kisha kwenda kwenye utumbo mkubwa ambako hukaushwa maji.

Baada ya kukaushwa maji hugeuka kuwa kigumu na hapo kile ambacho mwili hukihitaji hutolewa nje ya mwili kupitia njia ya haja kubwa.

Ili mfumo huo ukamilike ipasavyo inapaswa uanzie mdomoni, tumboni na kuungana na mfumo wa utumbo mdogo na mkubwa na lazima kuwe na uwazi katika eneo la kutolea haja kubwa.

Katika uwazi huo lazima kuwe na ‘valve’ ambazo humzuia mtu kujamba na huwa kuna mishipa ya fahamu ambayo humsaidia mtu kupata hisia za kupata haja kubwa au kutoa ushuzi (upepo) au uharo na hivyo kujizuia au kujisaidia.

Binadamu anahitaji kuwa na mfumo huo ikiwamo njia hiyo na valve hizo pamoja na mishipa hiyo ya fahamu, lakini kunapokuwa na hitilafu hupelekea watoto kuzaliwa na tatizo.

Kila binadamu anatakiwa kuwa na mfumo huo wa chakula uliokamilika hata hivyo wapo watoto ambao huzaliwa wakiwa na tatizo la njia ya haja kubwa.

Hadija ally Abdulah, Mkazi wa Zanzibar anasema awali hakugundua kwamba mwanawe amezaliwa na tatizo la kutokuwa na njia ya haja kubwa na kwamba alibaini hivyo miezi miwili baadaye tangu alipojifungua.

“Labda sikubaini mapema kwa sababu nilijifungua kwa upasuaji na siku tatu nilikuwa na hali mbaya, sikuweza kumuona mwanangu, hata hivyo nilijua wameshamkagua kuhakikisha kwamba alizaliwa salama, kumbe hawakubaini.

“Siku moja jioni wakati namuogesha ndipo nilishtuka kuona pempasi ilikuwa imejaa kinyesi lakini nilipoikagua vizuri ilinishangaza.

“Niliona ilikuwa na kinyesi lakini kinyesi kile kilionekana kimetoka katika njia isiyo ya kawaida kama ilivyo kwa watoto wengine, nilipoona ile hali, nilihisi vibaya mno, nilishtuka kwa sababu si hali ya kawaida.

“Huyu ni mwanangu wa nne niliojaliwa na Mwenyezi Mungu na ndiye mtoto wa pekee wa kike,  nililazimika kwenda kumshirikisha jirani yangu kuhusu kile nilichokiona,” anasema.

Anasema jirani yake huyo akampigia muuguzi anayehudumia watoto wake ambapo alimsihi kesho yake kuwahi hospitalini ili mwanawe achunguzwe.

 “Muuguzi yule alimchunguza (alimkagua) mwanagu kisha akanieleza  kinyesi kile kilikuwa kinatoka katika njia ya uke, niliogopa mno,” anasema.

Anasema ilibidi pale hospitalini wamfanyie upasuaji mdogo  eneo la ubavuni mwa tumbo ambapo ndipo anajisaidia hivi sasa.

“Sasa hajambo na anaendelea vizuri na afya yake kiujumla ni nzuri na ametimiza umri wa miezi saba,” anasema.

Hutokeaje?

Mwanamke anapokosa siku za hedhi hasa anapojihisi kuwa ni mjamzito wataalamu wa afya wanashauri azingatie ulaji unaofaa na kuacha kutumia dawa bila ushauri wa daktari kwani zipo dawa ambazo huweza kuathiri utengenezwaji wa mtoto tumboni.

“Huwa tunashauri kufanya hivyo kwa kuhofia kuharibu ule utengenezwaji wa mtoto tumboni kwa sababu katika kipindi cha wiki nane za kwanza ni muhimu kwani viungo vya mtoto huwa vinajitengeneza,” anasema Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Petronila Ngiloi.

Anasema kibaiolojia katika kipindi cha wiki nane cha ujauzito ndani ya tumbo la mama viungo vyote muhimu vya mtoto huwa vimeumbwa.

“Kile kipindi kinachofuata huwa ni uendelezwaji tu wa vile viungo na ukuaji wa mwili wake na huendelea kukaa tumboni hadi kipindi cha miezi tisa na kisha kuzaliwa,” anasema.

Anasema mara nyingi wanashauri mtoto akaguliwe punde tu baada ya kuzaliwa na kwamba ndani ya saa 24 tangu alipozaliwa lazima awe amepata haja ndogo na kubwa.

“Ikiwa hajapata inahitajika kufuatilia kwa ukaribu na kumkagua maumbile yake, je ana kasoro yoyote, anao ule uwazi wa kutolea haja zake au la!

“Ikiwa uwazi haupo ina maana kuna kasoro hivyo ni lazima ndani ya saa 24 awe amepata haja kubwa na ndogo, ikiwa hajapata inahitaji kufuatilia kumuangalia kimaumbile je, ana kasoro yoyote au anao uwazi wa kutolea choo.

“Ikiwa hana uwazi maana yake ana kasoro na anahitajika kufanyiwa upasuaji mdogo wa haraka siku hiyo hiyo ili kumtengenezea njia ya dharura ya kutolea haja,” anasema.

Mama mwingine 

Miriam John (30), Mkazi wa Kigoma anasema siku tatu baada ya mwanawe kuzaliwa alishangaa kuona anapata haja ndogo pekee na hakuwa anapata haja kubwa.

“Huyu ni mwanangu wa nane, nilipojifungua alikuwa ananyonya vizuri kabisa, lakini kila alipokuwa anataka kujisaidia haja kubwa nilimuona akijikamua mno na kutokwa jasho jingi hadi maziwa nayo yanarudi na kuanza kutoka puani na mdomoni.

“Ikabidi nimkague ndipo nikaona ana kasoro, jinsi alivyoumbwa ana sehemu tatu muhimu, ana njia ya haja ndogo, uke lakini pale sehemu ya haja kubwa niliona palikuwa na alama lakini ilikuwa imefunguka kidogo mno na kinyesi kilikuwa kinatoka kidogo mno,” anasema.

Anasema ilibidi ampeleke hospitalini ambako hata hivyo alielezwa kuwa hakukuwa na huduma ya upasuaji hivyo akapewa rufaa kwenda hospitali nyingine.

Anasema wanawake wenzake walimshauri kwamba asiwe na wasiwasi kwani njia hiyo itaendelea kuongezeka kidogo kidogo kadiri mtoto atakavyokua anakua mkubwa.

“Lakini sikuona mabadiliko wala ongezeko lolote la njia ndipo nikapewa rufaa kuja huku Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi,” anasema mama huyo.

Ni mateso makubwa

Dk. Ngiloi anasema  mtoto mwenye tatizo la kukosa njia ya haja kubwa hupata mateso makubwa ikiwamo kujaa tumbo na kushindwa kupumua.

“Tatizo hili ni kubwa, Muhimbili tunapokea watoto kutoka mikoa mbalimbali, hatujafanya utafiti kujua katika watoto kwa mfano 100 wanaozaliwa, wangapi huzaliwa na tatizo hili!.

“Ni watoto wengi tunaona, ndani ya siku tatu mtoto akishindwa kujisaidia haja kubwa, huteseka mno, kwa sababu anakuwa ananyonya kama kawaida na tumbo lake linakaa hewa nyingi, isitoshe ndani ya tumbo la mtoto kuna bakteria ambao hutengeneza gesi mbalimbali.

“Sasa kwa kuwa hajisaidii, hewa na gesi zinaendelea kujaa mtoto husika kushindwa hata kujamba na kujikuta tumbo lake likizidi kujaa kupita kiasi, wengi hufikishwa hospitalini wakiwa na hali mbaya,” anasema.

Anaongeza “Lakini haya yote yanaweza kuepukwa ikiwa mkunga atakuwa makini baada tu ya kumzalisha mama akamkagua mtoto husika kwa sababu ikigundulika mapema mtoto anafanyiwa upasuaji wa dharura kumsaidia.

“Lakini wale ambao wakunga hawakuweza kuwabaini, mama anaweza kufanya mwenyewe nyumbani kwa kuhakikisha anamkagua mwanawe kama ana matundu yote muhimu yanayohitajika,” anasema.

Matatizo mengine

Dk. Ngiloi anasema ikiwa mtoto hatafanyiwa upasuaji huo wa dharura kumsaidia kutoa haja zake, hali yake huendelea kuwa mbaya kiasi cha kushindwa kupumua vema kabisa.

“Kwa hiyo hatua ya kwanza ni kumfanyia upasuaji mdogo, baada ya kufanya vipimo mbalimbali, mtoto mdogo anapozaliwa na hitilafu tunaangalia kama atakuwa na hitilafu nyingine pia.

“Kwa utafiti tuliofanya watoto wanaozaliwa na tatizo hili wapo ambao huzaliwa na tatizo la koo, figo au wengine huzaliwa na figo moja tu, wapo wanaozaliwa pia na hitilafu ya mgongo au moyo.

“Tunachunguza kama figo zake zipo vizuri, uti wa mgongo, moyo na viungo vingine pia, kisha tunaangalia tatizo la njia kutofungua lipoje, wapo ambao huwa ipo karibu na wengine njia ile huwa ipo mbali mno kiasi cha ile misuli ya kuzuia choo huwa haipo.

Anasema wapo watoto waliozaliwa na tatizo hilo wakifanyiwa upasuaji hupona kabisa lakini miongoni mwao wapo ambao baada ya upasuaji hupata shida ya kuzuia haja kubwa.

“Wengi huja na shida ya kujichafua kwa sababu husindwa kujizuia kwani misuli huwa haipo, lakini kwa wote tunaona ni bora yule ambaye hapati choo tunaweza kumpa dawa za kumsaidia kulainisha choo au kumpatia orodha ya vyakula anavyotakiwa kula ili apate choo.

“Lakini wale wanaoshindwa kuzuia choo changamoto huwa kubwa mno hasa pale anapokafikia umri wa kwenda shule, hawa huwa wanahitaji uangalizi maalum wa kuwasaidia namna gani waishi kwa kukabiliana na hali hiyo ili waishi vema katika jamii kama watoto wengine,” anabainisha.

Anasema kwa kuwa upasuaji huo uchukua muda mrefu wa hadi zaidi ya saa mbili au tatu ndiyo maana hulazimika kumfanyia upasuaji wa dharura kufungua njia ya haja pembeni ya tumbo.

“Kwa kawaida mtoto mchanga hatupendelei kumuweka kwenye upasuaji mkubwa ataendelea vizuri hadi miaka miwili hadi mitatu ndipo tunamfanyia upasuaji mkubwa.

“Mtoto mchanga wa siku moja au mbili, mwili wake hushindwa kuhimili ile nguvu ya nusu kaputi, hata nyama zake zinakuwa hazijakomaa vizuri na hata tunapomfanyia upasuaji ule uponaji wake huwa si rahisi,” anasema. 

Anasema upasuaji huwa mgumu hasa kwa watoto wa kike pale ambapo njia zote huungana katika njia moja.

“Yaani mtoto wa kike ana matundu matatu wapo ambao huzaliwa njia zote tatu, ya haja kubwa, haja ndogo na uke zimeungana na kuwa njia moja, ni tatizo ambalo huhitaji umakini mkubwa katika upasuaji wa mtoto husika.

“Kwa kawaida njia ya haja ndogo inapaswa kuwa juu ya njia ya uzazi na ile ya choo inapaswa kuwa nyuma, lakini zimeungana kuwa moja, inabidi tumfanyie upasuaji kutenganisha kila moja ikae mahala pake,” anabainisha. 

Anashauri wazazi kuwawahisha watoto wao hospitalini ili wafanyiwe upasuaji mapema.

“Wazazi wa mtoto husika wanapoona dosari wasijaribu kumfanyia kitu chochote, labda kumchoma ili kuifungua au kuangaika kwa waganga wa kienyeji haitasaidia, wasimfiche ndani, mtoto akichelewa mno matibabu hufariki dunia,” anashauri.

Miriam naye anashauri wazazi kukagua watoto wao na kwamba wanapoona kasoro yoyote katika maumbile yao watoe taarifa mapema ili watoto wao wafanyiwe matibabu sahihi.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement