Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Zao la mpunga likiwa shambani

Na Cecilia Augustino, aliyekuwa Mbeya


UPO msemo wa Wahenga unaosema kwamba kilimo ni uti wa mgongo na mwingine ambao unasema jembe halimtupi mkulima.

Lakini unapata picha gani unaposikia habari kuhusu kilimo, ukweli ni kwamba watu wengi hasa vijana wanaposikia habari hizi moja kwa moja akili yao huwaza kwamba ni shughuli zinazowafaa watu masikini na wasio na ajira.

Fikra hii imejengeka mawazoni mwao kwa kipindi kirefu na ndiyo maana si ajabu siku hizi kuwaona wengi wao wakikimbilia maeneo ya mijini kwa kigezo cha kutafuta maisha bora.

Hii inatokana na uelewa mdogo na mawazo finyu waliyonayo juu ya sekta hii, jambo ambalo linawafanya washindwe kutambua kwamba wanaweza kujikwamua kimaisha iwapo watajishughulisha na kilimo.

Ukweli ni kwamba kilimo unaweza kukifananisha na dhahabu ambayo hupatikana kwa kuchimbua kidogo tu juu ya ardhi na si sana kama vile inavyopatikana ile dhahabu halisi ambayo ili uipate itakubidi uchimbe kwa kwenda chini ya ardhi zaidi.

Hivi sasa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kugundua siri hii iliyojificha ndani ya kilimo na hivyo wameanza kujishughulisha na kilimo na wameanza kufurahia matunda ya kazi yao.

Riziki Mwaisela (30) ni mmoja kati ya vijana ambao wameamua kujishughulisha na kilimo mkoani Mbeya.

Anasema tayari ameanza kufurahia kazi yake ya kilimo baada ya kuanza kulima kwa kutumia kilimo cha kisasa.

Mwaisela ambaye amefanikiwa kusoma hadi kidato cha nne anasema alianza kujihusisha na kilimo cha mpunga mnamo mwaka 2000.

Anasema awali alikuwa akilima zao hilo kwa mazoea kama ambavyo wakulima wengine nchini hufanya jambo ambalo lilimfanya apate mavuno kidogo.

“Kutokana na kulima kwa mazoea wakati huo nilikuwa nikipata kiasi cha tani mbili hadi tatu kwa hekta moja,” anasema.

Anasema ilipofika mwaka 2013 alijiunga na wakulima wenzake 3,020 wanaolima zao hilo na kuwa kikundi kimoja ambapo waliweza kupatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa.

“Tulipewa mafunzo ya kilimo cha kisasa ambacho kitaalamu wanakiita kilimo shadidi, hiki ni kilimo ambacho kinatuwezesha kupata mavuno mengi kwa kutumia maji kidogo eneo lile lile ambalo awali tulivuna kidogo.

“Tunatumia mbegu zile zile za kawaida lakini tunatengeneza miundombinu ikiwamo mifereji kuelekea shambani jambo ambalo linatusaidia kuhifadhi maji na wakati huo huo mpunga unakuwa ukipata maji ya kutosha shambani,” anasema.

Anasema yeye na wenzake hao walipoanza kulima kwa kutumia kilimo hicho walijikuta mavuno yao yakiongezeka kutoka tani 4. 3 hadi kufikia tani 6.4 mpaka 8 kwa hekta moja.

“Tuna eneo lenye hekta 2,000 na tayari tumeshalima kiasi cha hekta 1,500 kwa hivyo tunatarajia kwamba tutapata mavuno mengi zaidi msimu huu,” anasema.

Mwaisela ambaye ni baba wa watoto wawili na mke mmoja anasema shughuli ya kilimo imemuwezesha kujenga nyumba ya kisasa, kuwasomesha watoto wake katika shule za kimataifa (International School).

“Namshukuru Mungu kupata nafanikio haya na hivi sasa ninatarajia kununua trekta langu pamoja na fuso kwa ajili ya kujiimarisha zaidi,” anasema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Raphael Daluti anasema siku zote Serikali imekuwa ikitambua umuhimu mkubwa wa sekta ya kilimo na ndiyo maana imeanza kuweka mikakati ya kuwawezesha wakulima wadogo wadogo.

Anasema Serikali imejipanga kuisimamia sekta hiyo kwa ukaribu ili kuinua maisha ya mwananchi mmoja mmoja na hatimaye Taifa kwa ujumla.

Daluti anasema ndiyo maana kwa kutambua umuhimu huo iliamua kuiingiza sekta hiyo katika mpango wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

“Mpango huu wa BRN unajumuisha Wizara zipatazo sita ikiwamo hii ya Kilimo, Chakula na Ushirika nyingine zikiwa ni Elimu, Afya, Uchukuzi, Maji na Ujenzi,” anasema.

Daluti anasema kwamba ili kufanikisha mpango huo wa BRN Wizara hiyo iliteua mazao matatu ambayo ni mpunga, mahindi na miwa.

Anasema kupitia mazao hayo walilenga kuzalisha kiasi cha tani 290,000 za mchele,150,000 za sukari na 100,000 za mahindi.

Anasema walilenga kuzalisha tani hizo kutoka katika mashamba mapya ya uwekezaji yenye jumla ya hekta 330,000 na 350,000 kutoka katika maeneo ya wakulima wadogo.

“Katika kutekeleza mkakati huu Wizara imelenga kuwahusisha takriban wakulima wadogo 400,000 katika utaratibu wa kilimo cha kibiashara chenye mahusiano makubwa kati ya wawekezaji na wakulima wadogo wanaozunguka mashamba ya uwekezaji ndani ya muda wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2015/16,” anasema.

Anasema ili kufikia malengo hayo Wizara ilianzisha mashamba 25 ya uwekezaji kwa mazao ya mpunga na miwa, skimu 78 za umwagiliaji zinazoendeshwa kitaalam na kwa soko la pamoja la mchele pamoja na maghala 275 yenye mfumo wa pamoja wa soko la mahindi.

Anasema katika utekelezaji wa mikakati hiyo, maji ni pembejeo muhimu katika uendeshaji wa kilimo ambayo inahitajika.

Anasema kutokana na umuhimu huo, Serikali iliandaa mpango kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji (National Irrigation Master Plan – NIMP) wa mwaka 2002.

Anasema mpango wa NIMP uliainisha eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kuwa ni hekta milioni 29.4.

“Lengo la Serikali ni kufanya umwagiliaji uweze kuchangia kwa kiasi kikubwa kuleta mapinduzi ya kijani na kuliwezesha Taifa kufikia lengo la kujitosheleza kwa chakula na kupunguza umaskini wa kipato kupitia ukuaji mpana na endelevu wa uchumi,” anasema.

Anasema lengo hilo linatakelezwa ndani ya Mpango huo wa BRN, Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) pamoja na Mpango wa Kuendeleza Kilimo kupitia Ukanda wa Kusini wa Tanzania (SAGCOT).

Anasema katika kutekeleza Mpango wa BRN, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iliandaa malengo yafuatayo.

“Tumelenga kujenga na kukarabati miundombinu katika skimu 78 za wakulima wadogo, katika awamu ya kwanza tumeboresha skimu 19 kati ya 39 pia tumekamilisha ujenzi wa mabanio mawili kati ya matano,” anasema.

Anasema wamesajili vyama 20 vya umwagiliaji katika Wilaya za mkoa wa Iringa, Mbalali na Mpanda.

Vile vile tayari wamesambaza mashine 30 za kuvuna mpunga na nyingine nane za kukobolea ambazo zimegawiwa kwa skimu nne.

“Skimu ya Mbuyuni Kimani tumepeleka mashine 11 za kuvuna na mbili za kukoboa, Uturo saba za kuvuna na mbili za kukobia, Ipatagwa saba za kuvuna na tatu za kukoboa na Magozi tano za kuvuna na moja ya kukoboa,” anasema.

Anasema wameanza kujenga na kukarabati  maghala ya kuhifadhia mpunga ambapo tayari usanifu umekamilika kwa jumla ya maghala nane.

“Tumeanza ujenzi wa majengo ya mashine za kukoboa na kupanga madaraja ya mpunga, katika skimu ya Mbuyuni Kimani (Mbalali) na Magozi na Pawaga (Iringa) ujenzi upo hatua ya kuezeka, skimu ya Uturo na Ipatagwa (Mbalali) upo hatua za msingi na utakamilika Juni, mwaka huu,” anasema.

Anasema wameendelea kutoa mafunzo ya teknolojia ya kilimo shadidi cha mpunga (SRI) kwa maofisa ugani na mafundi sanifu na wakulima.

Anasema mafunzo hayo yanatolewa kwa wakulima na maaofisa ugani wa Wilaya ya Mbarali (Mbeya) na Iringa (vijijini).

“Jumla ya wakulima 620 na maofisa ugani 19 wamepatiwa mafunzo hayo na mashamba darasa yapatayo 13 yameanzishwa katika Wilaya hizo kwa ajili ya kulinganisha tofauti za kilimo shadidi na kile cha kawaida.

“Eneo lililolimwa ni hekta 19.6 ambazo ni sawa na ekari 49 na wastani wa uzalishaji katika kilimo shadidi ni tani 9.4 kulinganisha na kilimo cha kawaida ambacho huzalisha tani 4.5 kwa hekta.

Anasema wameboresha mifereji mikuu na ya mashambani imefanyika kwa urefu wa km 11.5 kati ya 42.8 na kwamba hivi sasa wanaendelea na maboresho katika mashamba yaliyoko Wilaya ya Mbalali, Iringa na Mpanda na tumeanzisha vyama 20 vya wamwagiliaji katika maeneo hayo,” anasema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement