Dar es Salaam
IDARA ya Tiba na Upasuaji Moyo Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) kwa kushirikiana na Hospitali ya Prince Sultan Cardiac Center iliyoko
Riyadhi nchini Saud Arabia, itatoa huduma ya upasuaji wa kuziba matundu
yaliyoko kwenye moyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk. Hussein Kidanto alisema upasuaji huo
utafanyika pasipo kufungua kifua kama ilivyozoeleka.
Alisema MNH imeanza kutoa huduma hiyo tangu jana hadi May
16, mwaka huu na kwamba wagonjwa zaidi ya 20 (watoto)wanatarajiwa kupatiwa matibabu.
Alisema tiba hiyo hufanyika kwa kutumia kifaa maalum cha
kuziba sehemu yenye tundu kupitia mishipa ya moyo.
“Taaluma ya matibabu inabadilika kwa kasi kubwa duniani na
ili tuweze kwenda sambamba na kasi hiyo ni lazima tushirikiane na nchi nyinginezo
zilizopiga hatua kubwa kwenye nyanja mbalimbali za matibabu,” alisema.
Alisema MNH imepokea madaktari bingwa hao kupitia taasisi ya
Al Mutanda Islami Trust ya nchini Uingereza.
“Wataalam wetu watajifunza ujuzi huo kutoka kwa wataalamu
hao jambo ambalo litasaidia kupunguza kasi ya wagonjwa wanaoelekwa kutibiwa nje
ya nchi katika siku za usoni.
kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo MNH, Dk
Sulende Kubwoja alisema huduma hiyo itatolewa kwa watoto wenye umri sifuri hadi
miaka 18.
Aliwataka watanzania kujitokeza kutoa damu ili iweze
kutosheleza katika kipindi chote cha upasuaji huo.
Naye Daktari Mshauri na Mwelekezi wa Magonjwa ya Watoto wa
Hospitali ya Prince Sultan, Profesa Jameel Alate alisema wameweza kutoa huduma
kama hiyo kwa nchi ya Sudan na Yemen na kwamba lengo lao ni kuwasaidia watoto
kupona tatizo hilo.
Chapisha Maoni