Dar es Salaam
SERIKALI imeshauriwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha za
bajeti yake katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ushauri huo ulitolewa Dar es Salaam jana na wadau wa
maendeleo walioshiriki katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Policy Forum
uliojadili iwapo fedha zilizotengwa katika sekta ya elimu na afya ya uzazi
zinakidhi.
Akizungumza katika mdahalo huo, Ofisa Utafiti na Uchambuzi
na Sera wa HakiElimu, Makumba Mwenezi, alisema licha ya Serikali kutenga Sh trilioni
3.8 katika sekta ya elimu lakini Sh trilioni 3.2 zimepelekwa katika mambo ya
kawaida huku Sh bilioni 600 pekee kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Tunawekeza kiasi kikubwa cha fedha katika mambo ya kawaida
na hata kile kidogo tunachowekeza kwa ajili ya miradi ya maendeleo tunakipeleka
katika elimu ya juu, kwa kuwapatia mikopo wanafunzi lakini tunajisahau kuwekeza
katika ngazi ya msingi na sekondari ambako ndipo panapohitaji nguvu kubwa ya
uwekezaji,” alisema Mwenezi.
Alisema sekta ya elimu imekuwa inakabiliwa na changamoto
kubwa kutokana na kuwa chini ya idara nyingi za Serikali jambo linalosababisha
kutokuwapo kwa uwazi wa matumizi ya fedha hizo zinazotengwa.
“Ipo chini ya Tamisemi pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Stadi, tuieweke chini ya idara moja ili fedha inapotengwa tujue kiasi
chake na jinsi kitakavyotumika na hii itaondoa mianya ya ufujaji wa fedha na kila
mara ripoti ya CAG inaonyesha udhaifu huo,” alisema Mwenezi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya Vijana ya Umoja wa
Mataifa (UNA), Robert Kasenene, alisema Serikali inapaswa kuwekeza zaidi katika
utoaji wa elimu ya uzazi wa mpango na kuongeza wataalamu wa kutoa huduma na si
dawa peke yake.
“Hivi karibuni Wizara ya Afya itawasilisha bajeti yake
inabidi ihakikishe inalifanyia kazi jambo hili kwa sababu tunahitaji kutoa
elimu zaidi juu ya jambo hili,” alisema Kasenene.
Chapisha Maoni