MAISHA ya watu katika
nchi zinazoendlea ikiwamo Tanzania yapo hatarini kutokana na asilimia 50 ya
magonjwa yasiyoambukiza kusababisha vifo.
Aidha magonjwa hayo
yamekuwa yakisababisha ulemavu huku gharama
za matibabu zikiwa kubwa hali inayopelekea tatizo hilo kuongezeka na kuwa kubwa
zaidi katika nchi hizo.
Yalizungumzwa hayo
mwishoni mwa wiki jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Magonjwa
yasiyoambukiza, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Auson Rwehimbiza katika
semina na waandishi wa habari iliyolenga kukamilisha mkakati pamoja na mpango kazi
2015/2020.
Alitaja baadhi ya magonjwa
hayo yasiyoambukiza ni moyo na mishipa ya damu, kisukari, kansa na magonjwa
sugu ya mfumo wa hewa.
Alisema magonjwa hayo
yanazidi kuongezeka nchini hasa kwa jamii ya watu waishio mjini na kuongeza
kuwa watu wazima wenye umri wa miaka 80 kuwa na magonjwa hayo kwa asilimia moja
hadi tatu na msukumo wa juu wa damu kwa
Asilimia tano hadi 10.
"Tathmini ya mwaka
2012 iliyohusisha watu wazima katika wilaya 50, inaonesha viwango vya kisukari
viliongezeka kwa asilimia tisa, huku asilimia 27 kwa msukumo wa juu wa damu,"
alisema Dk. Rwehimbiza.
Alisema ongezeko hilo
limetokana na kuongezeka kwa utandawazi, ukuaji wa miji, kutofanya mazoezi ya
mwili, ulaji usiofaa, utumiaji wa tumbaku pamoja na unywaji wa pombe
kupita kiasi.
Alisema Tanzania ilianza
kujihususha na magonjwa yasiyokuambukiza kuanzia mwaka 2009 hadi 2015, kwa
kuandaa mpango mkakati na mpango kazi ambao
ulihusisha utekelezaji wa mpango wa taifa wa kisukari kwa kushirikiana na chama
cha wagonjwa wa kisukari nchini.
"Hadi sasa utekelezaji wa mpango wa taifa
wa kuanzisha kliniki za magonjwa yasiyoambukiza umefikia asilimia 75 katika
hospitali za mikoa na wilaya na vituo vya afya, asilimia 75 ya elimu
zinazotolewa na watoa huduma wa afya katika hospitali za mikoa, wilaya na vituo
vya Afya.
Aliongeza kwamba, Shirika
la Afya Duniani (WHO), liliandaa mpango mkakati ambao ulidhamiria kupunguza
viwango vya sasa vya vifo vitokanavyo na magonjwa hayo kwa asilimia 25 ifikapo
mwaka 2025 na kupendekeza mapendekezo ya hiari lengo ikiwa kufanikiwa kwa
mkakati huo.
Alisema hadi sasa wapo
katika maandalizi ya kutoa elimu kwa jamii ya watu wa kansa,
umoja wa magojwa ya moyo,
umoja wa magonjwa sugu ya mfumo wa hewa pamoja na chama cha wagonjwa wa
kisukari nchini lengo ni kupunguza magonjwa hayo nchini.
Alisisitiza kwamba ulaji
wa vyakula unaofaa na kufanya mazoezi ni moja ya njia za kuepukana na magonjwa
hayo ambayo madhara yake yanapelekea ulemavu na vifo na kuongeza kuwa gahrama
za matibabu kuwa kubwa .
Kwa upande wake Meneja
Mradi John Garder alisema jamii kujenga taratibu za kupima afya
zao ili kujua afya zao
mapema na kutafuta ufumbuzi endapo watakutwa na magonjwa kama hayo
yasiyaombukiza na kuanza tiba mapema ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za
matibabu,vifo na ulemavu.
Alilitaka, Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), kufanya uhakiki wa kushtukiza mara kwa mara wa bidhaa zilizopo
madukani kwani bidhaa nyingi zimepita muda wa matumizi na kupelekea magonjwa.
Chapisha Maoni