Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokuwa wakimuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, katika harakati za kusaka urais, wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge kupitia chama hicho.
Kabla
ya hapo, kulikuwa na uvumi kuwa wabunge hao hawatachukua fomu kutokana
na kukatwa kwa Lowassa katika kinyang’anyiro cha urais.
Baadhi
ya wabunge hao ambao wamechukua fomu hizo na kuzirejesha jana ni pamoja
na Kangi Lugola (Mwibara), Andrew Chenge (Bariadi Mashariki), Philipo
Mulugo (Songwe).
Tanga
Mkoani Tanga, wabunge watatu waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa nao wamechukua na kurudisha fomu za kuomba kutetea majimbo yao.
Wabunge
hao ni Stephen Ngonyani maarufu kama Majimarefu ambaye ni Mbunge wa
Korogwe Vijijini, Beatrice Shelukindo (Kilindi) na Henry Shekifu wa
Lushoto.
Mtandao
huu umefuatilia mchakato wa uchukuaji na urudishaji fomu ndani ya CCM
ambao ulihitimishwa jana saa 10:00 jioni na kubaini kuwa wabunge hao
wameshachukua na kurudisha fomu za kutetea nafasi zao licha ya kuwapo
kwenye ushindani mkali kutokana na idadi ya wagombea kuongezeka kwenye
majimbo yao.
Katika
majimbo yote 11 ya Mkoa wa Tanga, wabunge wote waliokuwapo katika awamu
inayomalizika, wamejitosa tena na kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo.
Kwa sasa Mkoa wa Tanga una jumla ya majimbo 12 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuongeza jimbo moja la Handeni Vijijini.
Kilimanjaro
Vigogo
watano wa CCM mkoani Kilimanjaro wakiwamo Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango-Malecela na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey
Mwanri, ni miongoni mwa mawaziri `waliokabwa koo' kwa kupata upinzani
mkali ndani ya majimbo yao.
Wengine
ni Waziri wa zamani wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Mathayo David
Mathayo, ambaye anakabiliwa na upinzani mkali baada ya makada wenzake 13
kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea kiti hicho katika Jimbo la
Same Mashariki.
Waliojitosa
kutaka kumng’oa Dk. Mathayo David ni John Chaggama, Daniel Mkemi,
Alfred Ngelula, David Mawa, Amon Shahidi, Gerald William, Katery Daniel,
Yusuph Singo, Michael Mrindoko, Ahadi Kakore, Jordan Mmbaga na Mwalimu
John Singo.
Anne
Kilango naye anakabiliwa na upinzani baada ya makada wanane akiwamo Dk.
Michael Kadeghe, Dk. Eliji Kibacha, Semi Kiondo, Abraham Shakuri,
Nyangasu Werema, Daudi Mambo na Ombeni Mfariji kujitosa kuwania kiti cha
ubunge wa jimbo hilo.
Kigogo
mwingine aliyepata upinzani, ni Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwanri,
ambaye jimboni kwake, wazee wa kimila wa jamii ya wafugaji wa Kimasai
wamelazimika kumwangukia, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
(Nec), Meijo Laizer, kujitoa katika orodha ya makada watatu waliotangaza
kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea kiti hicho.
Kwa upande wa Jimbo Moshi Mjini ambalo kwa muda mrefu limekuwa ngome ya Chadema, makada 12 wamejitokeza kuwania kiti hicho.
Makada
hao ni Patrick Boisafi, David Mosha, Buni Ramole, Priscus Tarimo,
Edmund Utaraka, Shaniel Ngindu, Innocent Siriwa, Amani Ngowi, Omari
Mwariko, Michael Mwita, Daudi Mrindoko na Khalifa Kiwango.
Katika
Jimbo la Moshi Vijijini, Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara, Dk.
Cyril Chami, amekutana na kikwazo baada makada watano kujitokeza kutaka
kuteuliwa kugombea kiti hicho, huku Jimbo la Vunjo likiwa na watia nia
wanane ambao wanakabana koo kutaka kuteuliwa kugombea kiti hicho.
Dodoma
Waziri
wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge anayemaliza muda wake Jimbo la
Kibakwe, George Simbachawene, Livingstone Lusinde (Mtera), Gregory Teu
(Mpwapwa), Omari Badwel (Bahi) na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano, Job Ndugai (Kongwa), ni miongoni mwa makada waliochukua fomu
kutetea nafasi zao.
Bahi;
Mbunge
wa sasa Badwel atapambana na Pascal Mwaja, Levison Chilewa, Donald
Mejitii, Hebron Kipiko, Anthony Lyamunda, Salum Kanyika na Kondo
Chaurembo.
Mpwapwa:
Mbunge
wa sasa Teu, amepata wapinzani ambao ni George Lubeleje, June Fusi,
Nyange Mtoro, Charles Kuziganika, Rehema Halahala, Emmanuel Mbeho na
Gabriel Hango.
Kibakwe:
Simbachawene atapambana na Amani Bendera, Gabriel Mwikola, Sabas Chambas, Shahel Gayesh, Aclay Mnyang’ali na Solomoni Ngiliule.
Kongwa:
Ndugui
amepata wapinzani wake ambao ni Samwel Chimanyni, Dk. Elieza
Chilongani, Epafra Mtango, Pascal Mahinyila, Hussein Madeni, Simon
Katunga na Joseph Palingo.
Mtera:
Lusinde atapambana na Richard Masimba, Samwel Malecela, Essan Mzuri, Lameck Lubote na Dk. Michael Msendekwa.
Chilonwa:
Waliojitokeza
kutaka kuwania jimbo hilo ni Peter Nasoni Mlugu (Mwalimu wa Shule ya
Msingi Chilonwa), Kusakula Amosi (mfanyabiashara jijini Dar es Salaam),
Chibutii Masagasi, Charles Ulang, (Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya
Chamwino) na Vincent Chomol.
Wenslous
Mazanda (Mwalimu wa Shule ya sekondari Mpunguzi), Joel Mwaka
(Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi, Wilaya ya Chamwino), Daniel Robina
Logoha, Palolet K. Mgema (Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea), Deo Ndejembi,
Godrick Ngoli, Anderson Kusenha Magolola na Kk. David Mapana.
Kyela
WANACHAMA
10 wamejitokeza kuchukua fomu ya kuwania ubunge Jimbo la Kyela mkoani
Mbeya kupambana na Mbunge wa sasa, Dk. Harrison Mwakyembe.
Dk.Mwakyembe
ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alichukuliwa fomu
na baadhi ya wananchi ambao walijichangisha fedha na kumkabidhi jana
mjini Kyela ambaye alizirudisha Makao Makuu ya CCM Kyela.
Wengine
waliochukua fomu na kurejesha katika jimbo hilo ni Gabriel Kipija,
ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, John Mwaipopo,
Profesa Leonard Mwaikambo, Gwakisa Mwandembwa, Vincent Mwamakingula,
George Mwakalinga, Benjamin Richard, Asajile Mwambambale na Ackim
Jackison.
Mbeya Vijijini
Waliochukua
fomu Jimbo la Mbeya Vijijini ni Mbunge wa sasa, Luckison Mwanjale, Oran
Njera, Godon Kalulunga (Mwandishi wa Habari),Japhet Mwanasenga,
Anderson Kabenga, Walimu Sikwembe, Kassim Chakachaka.
Ileje
Aliko Kibona (Mbunge wa sasa) na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janneth Mbene.
Mbeya mjini
Nwaka Mwakisu, Aman Kajuna, Charles Mwakipesile
Vwawa
Mchungaji Tito Nduka, Japhet Hasunga na Mtella Mwampamba.
Maswa Magharibi
Waliochukua fomu ni Michael Bukwimba, Mashimba Ndaki, Benjamin Rungu, Aaron Mbojo (Mjumbe wa Nec) na Henry Mbichi.
Maswa Mashariki
MEMBE NASTAAFU SIASA
Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe, amesema hatogombea wadhifa wowote kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kwamba anapanga kujishughulisha na masuala yake ya kibinafsi.
Membe
ambaye alikuwa akitafuta tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili
kuwania urais mwezi Oktoba lakini akashindwa kufikia lengo hilo, amesema
kuwa, hatotafuta nafasi ya ubunge katika jimbo lake la Mtama.
Hata
hivyo amesema ataendelea kukiunga mkono chama chake cha CCM na
atampigia debe mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Bw. John
Magufuli.
Awali kulikuwa na tetesi kwamba Membe angegombea ubunge baada ya kukosa nafasi ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Huku
hayo yakijiri, chama cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kupata pigo baada
ya baadhi ya wabunge wake kutangaza kuwa hawatogombea tena nafasi zao
kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Tayari
madiwani 20 wa CCM katika jimbo la Monduli wametangaza kuhamia Chadema
na kumtaka mbunge wao, Edward Lowassa kufuata mkondo huo.
PINDA SIGOMBEI TENA
Waziri mkuu Mizengo Pinda amekataa ombi la wananchi wa jimbo lake la uchaguzi la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo aliyoianzisha.
Akizungumza
baada ya Ibada ya Jumapili katika kigango cha Kanisa Katoliki cha
Kibaoni wilayani Mlele (Jumapili, Julai 19, 2015), Waziri Mkuu Pinda
amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa
akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa yeye
kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa jimbo la Katavi.
Amesema
yeye ataendelea kuwa karibu na wananchi wa Katavi wakati wote na kwa
vile atakuwa na muda wa kutosha atashiriki kikamilifu katika mikakati
mbalimbali ya kuwaletea maendeleo wananchi ili waweze kujikwamua kutoka
kwenye umaskini.
Mheshimiwa
Pinda aliwaasa wananchi wa jimbo la Katavi wawe makini katika kuchagua
mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi
katika uchaguzi ujao.
Akimshukuru
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani Mlele,
Padri Aloyce Nchimbi aliwaasa wananchi wa Wilaya ya Mlele kumuenzi
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hata atakapokuwa amestaafu kwani
bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea maendeleo.
Waziri Mkuu yuko kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele kwa ajili ya mapumziko mafupi.
MWINYI, HAIKUWA RAHISI KUMPATA MAGUFULI.
Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa shughuli ya kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM haikuwa rahisi na akashukuru kwamba imemalizika kwa amani.
Mchakato
huo ulihitimishwa Julai 12 mjini Dodoma wakati Mkutano Mkuu wa CCM
ulipopitisha jina la Dk John Magufuli kugombea nafasi ya kuongoza
Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda
wake mwishoni mwa mwaka.
Jumla ya makada 38
walijitokeza kuwania nafasi hiyo, na majina matano ndiyo yaliyopitishwa
kwenda Halmashauri Kuu na baadaye matatu kwenda Mkutano Mkuu.
Mchakato
wa urais ndani ya CCM ambao kwa kawaida hutawaliwa na msuguano kabla ya
kumalizika kwa maridhiano, safari hii ulienda mbali zaidi baada ya
wajumbe watatu wa Kamati Kuu kupinga nje ya kikao uamuzi wa chombo hicho
na baadaye wajumbe wa Halmashauri Kuu kumwimbia mwenyekiti wao, Jakaya
Kikwete wimbo wa kuonyesha wana imani na Edward Lowassa baada ya jina la
mbunge huyo wa Monduli kuenguliwa na Kamati Kuu.
Jana,
akitoa hotuba fupi baada ya kumalizika kwa sala ya Eid el Fitr kwenye
viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mwinyi alizungumza kwa
mara ya kwanza hadharani kuhusu mchakato huo, akidokeza hali ilivyokuwa.
“Haikuwa
kazi rahisi kwenye mchakato huu wa kumtafuta mgombea mmoja atakaye
peperusha bendera ya CCM,” alisema Mwinyi lakini akawahi kuipoza kauli
hiyo kwa kuelezea amani ilivyotawala mwishoni.
“Kama ni jahazi basi sasa tunashukuru limefika pwani salama.”
“Uchaguzi
huu ni kwa ajili ya kuwapata viongozi wetu, tunataka viongozi bora wa
kutuletea maendeleo, mapatano na wenye mahaba na wananchi.”
Akizungumza
hadharani kwa mara ya kwanza baada ya mchakato huo wa kumtafuta mgombea
wa urais kukamilika mjini Dodoma, Mzee Mwinyi alimshukuru Mungu kwa
mchakato huo kuisha salama.
“Haikuwa kazi rahisi kwenye
mchakato huu wa kumtafuta mgombea mmoja atakaye peperusha bendera ya
CCM, kama ni jahazi basi sasa tunashukuru limefika pwani salama.
“Sasa,
ninawaomba Watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi wa
nchi tunaoufanyika kila baada ya miaka mitano,“ alisema Rais Mwinyi
ambaye alikuwa mmoja ya wajumbe wa Baraza la Ushauri waliofanya kazi ya
kutuliza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM hadi kuafikiana kuendelea na
mchakato wa kumpata mgombea urais.
Aliwasisitizia
Watanzania kuacha tabia ya kupenda mno na kuacha kubaguana, akisema
hakuna aliye bora na kuwataka kuzidisha mapenzi miongoni mwao na
kusherehekea vyema Sikukuu ya Eid el Fitr.
“Hakuna jambo lenye maana kama hili la kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kutufikisha salama siku kama hii ya leo (jana) ambayo tunasherekea Sikukuu ya Eid,” alisema Mwinyi.
“Hakuna jambo lenye maana kama hili la kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kutufikisha salama siku kama hii ya leo (jana) ambayo tunasherekea Sikukuu ya Eid,” alisema Mwinyi.
Awali Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad
Mussa Salum aliwasisitizia wananchi umuhimu wa kusherekea sikukuu hiyo
katika hali ya amani na utulivu.
Pia, aliwashauri
wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao sehemu zenye maadili ili
washerehekee kama ambavyo Mwenyezi Mungu anapenda.
“Leo
(jana) ni siku ya furaha, naomba tusherekee maeneo salama pia Waislamu
msisahau kufunga sita kwani ina malipo makubwa,” alisema Alhad Salum.
Mkoani
Geita ambako ilifanyika sala ya kitaifa ya Eid, Makamu wa Rais, Dk
Mohamed Gharib Bilal alihutubia Baraza la Eid na kusema kipindi hiki
kinahitaji utulivu, kuelewa na kuheshimiana pamoja na kudumisha uhusiano
ili Taifa lipate viongozi bora.
“Tuwe watulivu ili
Tanzania ibaki kuwa nchi ya kukimbiliwa na isiwe nchi ya kukimbiwa...
sisi tusiwe wakimbizi, tuwe watu wa kupendana, kuvumiliana na
kuthaminiana. Tusifikie hatua ya kuchukiana, kuuana na kufanyiana
ukatili,” alisema Dk Bilal.
Alisema amani inaweza
kuvunjwa na mtu yoyote kwa namna yoyote ile, akaharibu mazuri na heshima
ya Taifa na akawaomba wananchi na waumini wote wasifikie hatua hiyo
akisema ndiyo wenye uwezo wa kuifanya nchi yao kuwa ya amani.
“Tuishi
kwa kuheshimiana, kupendana na kuvumiliana tushikamane katika, hali
iliyopo sasa kwa nchi yetu siyo nzuri. Si ajabu hivi sasa tunavyoongea
kuna sehemu mabomu yametokea, si ajabu kuna watu wameuawa kikatili. Hii
yote ni sababu watu sasa wanapoteza misingi ya kuheshimiana, upendo na
kuvumiliana,” alisema Bilal kwenye Viwanja vya Karangara.
Awali
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania, Bakwata, Sheikh Suleiman
Lolela alisema waumini na wananchi wote waitumie vyema nafasi ya
Uchaguzi Mkuu kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaoendeleza
amani.
Kisiwani Unguja, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed
Shein amewataka viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kijamii na
madhehebu ya dini kulinda na kuheshimu msingi na malengo ya kuanzishwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akiuhutubia kwenye
Baraza la Eid el Fitr lililofanyika Ukumbi wa Bwawani na kuhudhuriwa pia
na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad jana, Dk Shein
alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kufanya siasa kwa kuzingatia
misingi ya Katiba na sheria kwa madhumuni ya kuendeleza na kulinda amani
na umoja wa kitaifa kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
“Tunaweza
kushindana bila ya kulaumiana, kukejeliana na tunaweza kushindana bila
ya kudharauliana au kuhasimiana,” alisema Dk Shein kwenye shughuli hiyo
iliyotaliwa na hali ya utulivu.
Alieleza kuwa vyama vya
siasa vimeanzishwa na vipo kwa ajili ya kushindana kwa sera kwa
madhumuni ya kuchochea maendeleo ya Zanzibar na siyo kugombanisha watu
na kuvuruga misingi ya amani na umoja wa kitaifa.
Kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, sheikh wa mkoa, Ahmed Zuber aliwataka Watanzania kudumisha amani na umoja.
Zuber
alisema dunia sasa imechafuka kutokana na uvunjifu wa amani
unaochochewa na siasa chafu hivyo Watanzania bila kujali dini wala
itikadi zao wanapaswa kuilinda amani iliyopo sasa.
“Tunahitaji
utulivu. Nchi nyingi huharibikiwa kipindi kama hiki cha uchaguzi, amani
hupotea kipindi hiki cha uchaguzi. Ndugu zangu Waislamu na msio
Waislamu tukiichezea amani hii iliyopo sasa, tujue hakika hatuna kwa
kukimbilia,” alisema.
Mkoani Tanga,
imamu wa Msikiti wa Ibadhi, Sheikh
Mohammed Said aliitaka jamii kudumisha amani na utulivu uliopo na kuacha
kushabikia vyama vya siasa.
Sheikh huyo alisema ni
wajibu wa kila mtu kutambua kuwa amani iliyopo ikitoweka ni vigumu
kuirejesha na hivyo kila mmoja ahakikishe anatambua wajibu wake.
Alisema
wakati wa uchaguzi, hutokea jamii kuhamasishana kwa mambo ya kisiasa,
jambo ambalo alisema ni baya na halifai kutokea na hivyo kutaka kila
mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake.Mkoani Lindi, Sheikh Salimu Nalinga akitoa salamu za Eid el Fitr aliwataka Waislamu kuchagua viongozi waadilifu ili kuifanya nchi kuendelea kuwa ya amani na utulivu
Chapisha Maoni