Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

 
*Wamiliki walia na ushuru mpya.

* Madereva walia na posho zao. wasema mgomo ni kuanzia wiki ijayo



CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kimesema mgomo wa mabasi  nchini nzima unanukia, endapo Serikali haitashusha gharama za ushuru wa kuingiza mabasi mapya. 


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Taboa, Ennea Mrutu, alisema Serikali imewataka wamiliki wa mabasi kulipa asilimia 25 kama ushuru kwa kila basi jipya linaloingizwa nchini.


“Zamani tulikuwa tunalipa asilimia 10, sasa wamepandisha kiasi hiki, nani atamudu gharama za uendeshaji?


“Basi moja tulikuwa tunalipa Sh milioni 40, sasa tunatakiwa kulipa Sh milioni 94… jamani gharama hizi ni kubwa, mbona tutashindwa kuhudumia Watanzania.


“Kwa hali ya kawaida hatuwezi kukomboa basi, fedha hizi zitatoka wapi jamani? Tuwe wakweli katika hili, kama utaratibu huu ukiendelea hatutaweza kusafirisha abiria,” alisema Mrutu.


Alisema wamiliki hao ambao walikuwa nchini China hivi karibuni, tayari wamekutana na watengenezaji wa mabasi aina ya Yutong ambao wamekubali kuja Tanzania kuzungumza na viongozi wa Serikali waone namna ya kuingiza mabasi mengi zaidi.


Mrutu alisema kama Serikali ikiendelea na msimamo huo, ni wazi kuanzia sasa mgomo wa kusitisha huduma hiyo unanukia.


“Kama Serikali itaendelea na msimamo huu, tutasimamisha huduma, tumeleta mabasi mengi yako bandarini, tumeshindwa kuyakomboa,” alisema Mrutu.


Alisema bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 201/16, haikuweka kipengele chochote cha kupandisha gharama za ushuru, lakini wanashangazwa na hatua hii sasa.


Kutokana na hali hiyo, Mrutu alisema Taboa imewaandikia barua Waziri wa Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Waziri Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Akijibu malalamiko hayo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alikiri kupokea barua ya Taboa na kusema Serikali inalifanyia kazi suala hilo mara moja.


“Nimepokea barua yao, nashangaa kuona wamekuja kwa waandishi wa habari hata kabla hatujazungumza, jambo kubwa ni kwamba tunashughulikia suala lao.


“Kwavile wao wametoa tamko kwenu, na sisi tunajipanga kutoa taarifa rasmi. Nawaomba wajue tulitoa punguzo kwa mradi wa mabasi ya mwendo kasi tu (DART),” alisema Waziri Mkuya.

WAKATI HUO HUO

MADEREVA nchini wametishia kufanya mgomo kwa mara nyingine kuanzia wiki ijayo na kwa muda usiojulikana iwapo serikali kupitia kamati iliyoundwa kushughulikia matatizo yao haitawaita na kuongea nao kuhusu posho zao za ndani na safari za nje.
  
 
Kauli hiyo imetolewa jijini dar es Salaam jana na Katibu mkuu wa Chama cha Madereva, Rashid Salehe (pichani) ambapo alisema madereva hao wamemtuma na kuitaka serikali isimuulize kiongozi yeyote wa madereva kipindi watakapoamua kugoma mpaka  madai hayo yatekelezwe.
 
Alisema kuwa pamoja na kupata  mikataba mipya katika kikao cha mwisho kilichofanyika mwezi uliopita hata hivyo bado madereva wanaendelea kupewa mikataba mingine tofauti na ile waliokubaliana katika kikao hicho cha mwisho.
 
“Madereva bado wanaendelea kupata shida na kusota bila kujua hatima ya posho zao za safari za ndani na nje hivyo tunaitaka Wizara ya mambo ya Ndani na Wizara ya Kazi isije kutuita viongozi na kutuuliza juu ya hili kwa kuwa madereva hao wamechoka hivyo wamenituma baada ya kufanya ziara za mikoa kadhaa na kuniagiza niseme kuwa wataacha kuendesha magari kama serikali haitawaita kujua hatima ya suala hilo” alisema Salehe.
 
Aliongeza migogoro kati ya madereva na matajiri wa magari hayo ni kutokana na  mfumo wa viongozi wa serikali kuhusika kuwafanya biashara hiyo huku wakiwa wanawakandamiza waliochini.
 
“Kuna kampuni ya magari fulani sitayataja jina tajiri wake analugha za matusi na tumeshamrekodi wakati akitoa matusi hayo na tunafikiria kumpeleka huyu bwana mahakamani” alisema Salehe.
 
Alisema kuwa pia kuna gari la kigogo mmoja ambalo lilibeba sumu za mgodini limekwama porini muda mrefu na tajiri wa basi hilo amewatelekeza madereva hao  bila kujali afya zao zinaendelea kuharibika kwa kukaa na sumu hiyo.
 
Salehe alisisitiza kama mfumo uliopo wa vigogo wa sarikali kuwa ndio wamiliki wa mabasi hayo basi kila watakalo kuwa wanafanya litaonekana la kitoto na migogoro haitaisha na ukizingatia wanalindwa na sheria ya mwaka 1955 ambayo wanaitumia mpaka leo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement