MKURUGENZI wa Kampuni ya Lino International
Agency, Hashim Lundenga (Pichani) amejitoa katika Kamati ya Miss Tanzania na kuunda
timu nyingine ambayo itasimamia kinyang’anyiro hicho, kuanzia sasa ikiwahusisha warembo kadhaa akiwamo Jokate Mwegelo (Kidoti).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Lundenga alisema
kuwa Kamati mpya ina wajumbe 12, ikiongozwa na Mwenyekiti Juma Pinto ambaye ni
Mkurugenzi wa Jambo Concept, wakati Makamu wake ni Lucas Rutta na Katibu ni Doris Mollel.
Wajumbe ni Miss Tanzania 1999 Hoyce Temu, Mohamed
Bawazir, Gladyz Shao, Magdalena Munisi, Shah Ramadhani, Hamm Hashim, Khalfani
Saleh na Ojambi Masaburi, wakati Jokate akiwa ni Msemaji wa Kamati hiyo.
“Kamati iliyomaliza muda wake ilidumu kwa miaka
21, imefika wakati wale tuliokuwapo tumechoka na hivyo kutulazimu kukasimu
nafasi hizi kwa wengine ili tupate mawazo mapya yatakayosaidia kuboresha kama
tulivyoelekezwa na BASATA (Baraza la Sanaa la Taifa),” alisema.
Kwa upande wake, Pinto alisema: “Kamati imeanza
kazi mara moja kuanzia leo (jana) baada ya kutambulishwa kwa waandishi wa
habari, mashindano huenda yakafayika mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa
mwaka ujao hii ni kulingana na hali halisi kwamba tupo katika kipindi cha
uchaguzi.”
Aliongeza: “Tutaanza na changamoto zilizojitokeza
mwaka jana, tutakutana na BASATA ili watupe miongozo ambayo itatufaa zaidi
kusimamia na kuendesha mashindano hayo.”
Akisisitiza katika hilo, Jokate alisema watafanya
juu chini kurudisha hadhi ya mashindano hayo na kuyafanya yawe kama yale ya
kimataifa.
“Tunatarajia kuamsha hisia mpya, tutatumia uzoefu
wetu kuhakikisha mashindano yanakuwa bora kwa pamoja na kuwapata wawakilishi
ambao watazingatia miiko,” alisema.
Mbali ya kamati hiyo ya akina Pinto, pia
imeteuliwa sekretarieti itakayosimamia mashindano hayo inayoundwa na Dk Ramesh
Shah, Hidan Rico, Yasson Mashaka na Deo Kapteni.
Shindano hilo lilifungiwa kwa miaka miwili
Desemba mwaka jana na BASATA kwa madai ya kukiukwa kwa taratibu, kabla ya
kufunguliwa mapema mwezi huu baada ya Lundenga na timu yake kurekebisha baadhi
ya kasoro zilizojitokeza.
Chapisha Maoni