Kuku wakiwa wanauzwa sokoni |
UKIPANDA daladala linalotoka Makumbusho kupitia Sinza ukifika kituo cha Shekilango, Makondakta wengi wamepabadili jina sasa panaitwa mahakama ya kuku.
Soko la Shekilango, Manispaa ya Kinondoni limejipatia umaarufu wa jina hilo kutokana na kuwapo kwa machinjio ya kuku.
Hata hivyo, Manispaa sasa imeamua kuifunga kwa
muda usiojulikana kutokana na kukithiri kwa uchafu.
Machinjio
hayo yalifungwa jana na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ubungo, Shabani Kambi baada
ya kutembelea sokoni hapo ili kujionea hali ya usafi ilivyo.
Akizungumza mara baada ya kufunga machinjio hayo, Kambi alisema hadi sasa katika
Kata yake kuna wagonjwa 11 wa kipindupindu ambao wanatoka mitaa ya NHC, Chuo
Kikuu, Kibo na Msewe.
“Wiki
iliyopita nilipita nikawaambia wazingatie usafi lakini leo (jana) nimekuja hapa
naona hakuna kilichofanyika, sasa nafunga machinjio yote hadi
mtakapojirekebisha,” alisema Kambi.
Licha ya
kufunga machinjio hayo, Ofisa huyo pia aliwaamuru mama lishe wanaofanya
shughuli zao katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo kuacha biashara hiyo kuanzia
leo hadi hali ya ugonjwa huo itakapotulia.
Katika hatua
nyingine, Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya kijamii
(CCI), limeanza kutembelea maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kinondoni ili kutoa
elimu kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa huo.
Ofisa
Uhamasishaji masuala ya afya katika shirika hilo, Pudenciana Lukago, alisema
elimu hiyo inatolewa kwa ushirikiano wa mtandao wa vikundi mbalimbali vya
kijamii (Federation) vilivyoko kwenye Manispaa hiyo.
Aliyataja
maeneo ambayo wamekwishatembelea kuwa ni Ubungo, Mburahati, Mwananyamala,
Kigogo na Magomeni.
“Moja ya
majukumu yetu ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu usafi wa mazingira na kote ambako
tumepita tumebaini watu wengi hawana elimu ya kutosha juu ya ugonjwa huu,”
alisema Lukago.
Chanzo, MTANZANIA
Chapisha Maoni