MKURUGENZI Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini (NBS), Dk. Albina
Chuwa (pichani), amewashauri vijana kujitokeza kusomea fani hiyo ili waje kushika nafasi
pindi walioko hivi sasa watakapostaafu.
Aidha amesema wakati umefika kwa watakwimu wa bara la Afrika kubadili
mifumo ya uendeshaji kwenye ukusanyaji ili kuendana na hali halisi.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Dk. Chuwa kwenye Maadhimisho
ya Siku ya Takwimu Duniani, yaliyofanyika Dar es Salaam katika Chuo cha Takwimu
Mashariki mwa Afrika.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuziwezesha nchi za Afrika kufanikisha
utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyopitishwa hivi
karibuni na Umoja wa Mataifa (UN) kwa haraka.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukifanya kazi kwa mazoea, lakini wakati
umefika kwa nchi zetu za Afrika kubadilika, ni lazima tushirikiane na wadau
mbalimbali wa takwimu, hasa sekta binafsi, kwani wanazo takwimu nyingi hivyo
tunahitaji kuzikusanya na kuziweka pamoja.
“Lazima tuwekeze kwa vijana kwa kuwafundisha kwa sababu itafika
kipindi tunaweza tusiwepo, hivyo lazima vijana waingie kushika nafasi hizi ili
wasaidie nchi zao na dunia kwa ujumla,” alisema Dk. Chuwa.
Alisema yanahitajika mabadiliko na kutumia njia za sayansi na
teknolojia katika ukusanyaji wa takwimu ili kuendana na wakati tuliopo.
“Kazi ya kutumia njia za zamani katika ukusanyaji wa takwimu ni ghali,
kwa mfano hapa nchini ili kufanya utafiti wa matumizi kwa kaya inagharimu kiasi
cha Sh bilioni 12 pekee na hii si sensa ya jumla,” alisema Dk. Chuwa.
Dk. Chuwa alisema iwapo hatua hizo hazitachukuliwa kuna uwezekano siku
zijazo mashirika makubwa duniani yatachukua nafasi za watakwimu wa mataifa
mengine na hivyo hawa waliopo watapoteza nafasi zao.
“Ni vizuri sisi wenye nafasi hivi sasa tuwahamasishe wengine
kujiendeleza kimasomo ili kujijenga kitaaluma na tuondokane na ule utegemezi wa
kutumia wataalamu wa nje ya nchi,” alisema Dk. Chuwa.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Frank Mkumbo, alisema
ili kupata takwimu zilizo bora ni lazima ukusanyaji wake uzingatie ubora katika
uandaaji na usambazaji wa takwimu husika.
“Tunajitahidi kuyafundisha hayo hapa chuoni, tunazingatia suala la
matumizi ya teknolojia, wanafunzi wetu wanatoka katika nchi zinazozungumza
lugha ya Kiingereza, lakini kuna changamoto kwamba wengi hushindwa kusoma
kutokana na kukosa ufadhili,” alisema Dk Mkumbo.
Chapisha Maoni