Polisi akikagua uharibifu uliotokea baada ya ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sandali ya Temeke Mikoroshini jijini Dar es Salaam kuchomwa moto baada ya wananchi kugomea matokeo |
WANANCHI wamevamia ofisi ya Mtendaji Kata ya Sandali
Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam na kuichoma moto wakitaka matokeo ya udiwani wa kata hiyo yatangazwe.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Mtaa wa
Sandali, Deodat Chuma alisema kituo hicho kilichomwa moto saa
1:40 asubuhi, baada ya wananchi
kukasirishwa na kucheleweshwa matokeo ikiwa pamoja na kutangazwa mshindi wa
CCM, Abeli Tarimo.
Mwenyekiti huyo ambaye pia alikuwa wakala wa CCM, alisema matokeo hayo baada ya kukatiliwa yalihesabiwa
upya ambako wa CCM akaibuka tena kidedea kwa kuongoza kwa kura 600 wakati awali zilikuwa ni 400, na mgombea wa CUF, Khalid Yahya aliyagomea.
“Matokeo ya awamu ya pili yaliongezeka tena kwa CCM kupata
kura nyingi hali hiyo iliwakera wenzetu wa upinzani,”alisema Chuma.
Alisema kutokana na hali hiyo kundi la vijana walivamia ofisi
hizo ambako ndiko kulikuwa ni kituo cha
kupiga kura na kuichoma moto.
“Vijana hawa walidai wanataka kuchoma moto pia kituo cha
afya, kanisa na shule ya msingi ikiyopo eneo hilo," alisema Chuma.
Chuma alisema amesikitishwa na kitendo hicho kwa sababu ni
siasa chafu ambazo zimepitwa na wakati.
Alisema umefika wakati wanasiasa wakakubaliana na matokeo wanapojitosa katika kinyang’anyiro
mbalimbali.
Pia alisema katika tukio hilo nyaraka mbalimbali zimechomwa
moto yakiwamo masanduku matatu ya kupigia kura ambayo yalikuwa matupu.
"Tunamshukuru Mungu matokeo yalikuwa tayari
yamepelekwa kwa mkurugenzi hivyo hayakuchomwa,"alisema Chuma.
Akizungumzia vurugu hizo, alisema ilitokana pia na wakala
mmoja kupoteza matokeo ya kituo cha Kisiwani ya udiwani ambayo hayajaonekana.
"Hii imetokana na Tume ya Uchaguzi (NEC) kutokuwa na
mawakala makini… ndiyo yote haya yamesababisha,"alisema Chuma.
Khalid Komba ambaye ni wakala wa CUF, alisema
uchaguzi huo haukuwa huru na haki na ulikuwa wa
mabavu.
Alisema tangu Jumapili Mgombea wa CUF, Khalid Yahya
alishinda lakini hawakutaka kumtangaza.
Alisema wamechoshwa
na uongozi wa Tarimo wa CCM kwa kuwa ana miaka 15 ya uongozi ndani ya kata hiyo
na hakuna alichokifanya.
"Huyu diwani anaishi Mbezi ikifika kipindi cha
uchaguzi anakuja kuishi huku...hatumtaki kwanza hata CCM wenyewe wanafahamu
alipita ‘kimagumashi’ katika kura za maoni ndani ya chama chao,"alisema
Komba.
Wananchi wakishangilia nje ya kamba ya polisi baada ya ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sandali ya Temeke Mikoroshini jijini Dar es Salaam kuchomwa moto baada ya wanachi hao kugomea matokeo. |
Alisema wao hawamtaki na wanachokifahamu hawana diwani kwa kuwa
kura hawajampa yeye, aliyepewa hajatangazwa.
Mgombea udiwani wa CUF, Yahya alisema fujo hizo
zilitokea kwa sababu NEC haikutenda haki na kura nyingine walikimbia nazo.
Alisema polisi waliwatafuta mawakala wa NEC wakakamatwa
watatu na hawakuwa na matokeo hayo waliwapa watu wa CCM ambao walikamatwa nayo.
Yahya alisema walitaka kubandika matokeo hayo bila
kukubaliana kwa kuwa yalikuwa ni ya marudio na ni tofauti na ya awali.
"Wakati fujo hizo zinatokea mimi sikuwapo, wananchi
wanamtaka mtu wanayempenda roho zimewauma na wana hasira,"alisema Yahya.
Chapisha Maoni