ASILIMIA 75 ya wagonjwa 800 waliofanyiwa upasuaji mwaka huu
katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ni watoto wadogo huku
watu wazima wakiwa ni asilimia 25.
Akizungumza na waandishi wa habari jana hospitalini hapo
Dar es Salaam jana, Daktari Bingwa na Mkuu wa Kitengo cha Watoto wa JKCI, Dk.
Godwin Sharau, alisema hali hiyo inatokana na mfumo mbovu wa ulaji wa vyakula
pindi mama anapokuwa mjamzito, kutokuhudhuria kliniki na unywaji wa maji,
vyakula vilivyo na kemikali.
Pia alisema hali hiyo inatokana na mjamzito kutopata chanjo
akiwa katika kipindi hicho.
“Kuna hatari ya watoto wengi zaidi kupata tatizo hili iwapo
jamii haitachukua tahadhari, kwa sababu nimegundua kwamba wanawake wengi hupata
ujauzito huku wakiwa hawajapanga na wenzi wao na kwa sababu hawajapanga
huendelea kunywa pombe, ulaji mbovu wa vyakula pamoja na uvutaji wa sigara,
vitu ambavyo huchochea tatizo hilo.
“Kitaalamu kipindi cha wiki mbili za mwanzo za ujauzito ni
cha muhimu kwa kuwa viungo vya mtoto huanza kujijenga, lakini mfumo huo wa
ulaji na unywaji huenda kuvuruga ukuaji wa mtoto tumboni na ndiyo maana watoto
wengi wanazaliwa na ugonjwa huo,” alisema Dk. Sharau.
Alisema unywaji wa maji na vyakula vilivyoathiriwa na
kemikali ambazo wakati mwingine hutiririka kutoka migodini pia husababisha
mtoto kuzaliwa na tatizo.
“Kwa mfano Mwanza tuliwahi kusikia maji ya migodini
yalitiririka na kuingia kwenye mito, watu wanapotumia maji yale hasa wajawazito
kuna uwezekano mkubwa wa watoto kuzaliwa wakiwa na matatizo ya moyo katika eneo
lile,” alisema Dk. Sharau.
Alisema iwapo mjamzito atapata chanjo maalum katika kipindi
hicho kama ya kuzuia ugonjwa wa rubera hujikuta akipata mafua makali ambayo
mwishowe hupelekea mtoto kuathirika.
“Nawashauri wajawazito kuhudhuria kliniki ili wafanyiwe
uchunguzi mapema kujua kama mimba ipo salama ili waweze kujifungua watoto wao
bila tatizo hili,” alisema.
Awali, Kaimu Mkuu wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, alisema
hata hivyo wanajivunia kufanikisha upasuaji wa watoto hao kwa ufanisi.
“Hivi karibuni tuliwafanyia upasiaji watoto 37 na mmoja
kati yao alifariki, kwetu ni mafanikio licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa
ikiwamo uhaba wa wataalamu, damu ya kutosha pamoja na vifaa,” alisema.
Alisema hivi sasa Taasisi hiyo itakuwa ikijitegemea na ana imani
watafanya kazi kwa kiwango kikubwa hali itakayoisaidia Serikali kuokoa fedha
ambazo zingetumika kuwatibu wagonjwa nje ya nchi.
Chapisha Maoni