Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


TAASISI isiyo ya kiserikali iitwayo Unity in Diversity Foundation (UDF) imemuomba Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati suala la kupigwa mnada kwa makontena yake mawili yaliyoko Bandarini.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam juzi Mratibu wa UDF Taifa, Enock Bigaye alisema wamefikia uamuzi huo wa kuomba msaada baada ya kupewa taarifa kuwa yatapigwa mnada kutokana na kudaiwa tozo ya bandari kavu iliyofikia kiasi cha milioni 9.6.

Alisema makontena hayo yaliingia nchini tangu Septemba, mwaka huu yakiwa na vitabu vya msaada zaidi ya 25,000 pamoja na vifaa mbalimbali vya ufundi stadi hata hivyo mchakato wa kuyaondoa ulikuwa mrefu kiasi cha kufikia deni hilo.

“Taasisi yetu inajishughulisha na huduma za kijamii na tangu tuanze tumeingiza nchini makontena zaidi ya 20 na tumekuwa tukivigawa bure vifaa hivyo kupitia kwa Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Wizara mbalimbali.

“Vifaa hivyo tumekuwa tukivipata kutoka kwa wahisani walioko nje ya nchi na kwa awamu hii tumefanikiwa kuingiza makontena hayo mawili moja likiwa na vitabu mbalimbali kwa ajili ya shule za Sekondari vyenye jumla ya Sh milioni 190.

“Kontena lingine lina vifaa vya ufundi  stadi ikiwamo kompyuta mpakato (laptop), vyerahani, na vifaa vingine vya ufundi lakini kwa bahati mbaya yamezuiliwa na nimepewa barua ya ‘nortification’ kwamba yanataka kuuzwa,” alisema.

Alisema baada ya kupewa barua hiyo wameshafanya jitihada mbalimbali ikiwamo za kumwandikia barua Rais Dk. Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) ambazo hata hivyo hazijajibiwa.

Alisema taasisi hiyo imesajiliwa Machi 13, 2006 kwa namba 2004,cap 202 na Msajili wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali chini ya Wizara iliyokuwa ikishughulikia masuala ya maendeleo ya jamii.

“Kwa kawaida huwa tunapewa misamaha ya kodi, makontena yanapofika bandarini hutolewa na kupelekwa bandari kavu lakini yanapopelekwa huko mchakato wa kuyaondoa huchukua muda mrefu hadi zinazidi siku 21 ambapo hutakiwa kulipia kiasi cha Dola 45 ambazo ni sawa na Sh 90,000 kwa sasa.

“Nasikitika kwanini liuzwe wakati wahisani wamenipa msaada huo, nitashindwa kupeleka ripoti kwao na hawatanipa tena msaada na iwapo ningefanikiwa kusambaza msaada huo wa vitabu shule 50 zingefaidika,” alisema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement