Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Simon Sirro alipozungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) hivi karibuni |
KATIKA hali ya kushangaza shehena ya matofali Tani 14.2 imesafirishwa
hadi nchini Ujerumani kupitia Bandari ya Dar es Salaam badala ya shehena ya
tumbaku iliyopaswa kusafirishwa kwenda nchini humo.
Matofali hayo yalifungashwa pamoja na boksi 28 za tumbaku
baada ya kuibwa boksi 71 zenye thamani ya sh milioni 150.
Taarifa hiyo ilitolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam
alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema tumbaku hiyo ambayo ni mali ya mfanyabiashara Ahmed
Huwel (36) mkazi wa Msasani Rejent zilikuwa jumla ya boksi 99 zenye uzito wa
kilo 200 kila moja ambazo alizinunua katika kiwanda cha Alliance One Tobacco
Tanzania Ltd kilichoko Morogoro kwa ajili ya kuzisafirisha kwenda Ujerumani.
Alisema jeshi la polisi lilipata taarifa juu ya wizi huo
kutoka kwa mfanyabiashara huyo Januari 6, mwaka huu saa nane mchana ambapo
alifungua kesi ya wizi dhidi ya Mohamed Waziri mkazi wa Kigogo ambaye ndiye
dereva aliyemtuma kuchukua mzigo huo kiwandani.
Alisema mfanyabiashara huyo alitambua juu ya wizi huo baada
ya kuelezwa na walioko Ujerumani Januari 4 mwaka huu kwamba walipokea shehena
hiyo ya matofali pamoja na boksi 28 za tumbaku.
“Huwel alieleza
kwamba siku ya tukio mtuhumiwa akiwa na gari aina ya Scania T. 628 CXL yenye ‘Trailer’
T. 775 CGC alimtuma kwenda mkoani Morogoro katika kiwanda hicho kuchukua
tumbaku hizo boksi 99.
“Mtuhumiwa aliondoka Morogoro kuja Dar es Salaam kuleta
mzigo huo bandarini kwa ajili ya kusafirisha kwenda nchini ujerumani.
Lakini alipofika
eneo la Mabibo aliingia kwenye ‘yard’ ya kuegesha magari ya Samwel Tarimo
ambapo mtuhumiwa (dereva) alishirikiana na mtoto wa mwenye yard hiyo, aitwaye
Samson Tarimo... walifungua ‘seal’ ya kontena na kuiba maboksi hayo 71,”
alisema Kamanda Sirro.
Alisema baada ya kupata taarifa hiyo, jeshi hilo lilianza
msako mara moja ambapo dereva wa gari hilo alikamatwa na kuambatana na askari
kwenda kwenye eneo la tukio ambako upekuzi ulifanyika.
Alisema katika upekuzi huo waliwakamata watuhumiwa wengine
wawili ambao ni Saimon Tarimo (mtoto wa mwenye ‘yard’hiyo) na Felix Tarimo
ambaye ni fundi magari mkazi wa Mbezi Tangibovu.
Alisema baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa walikiri kufanya
tukio hilo na kueleza kuwa mzigo huo ulikuwa umepelekwa mafichoni mkoani Tanga
Januari 9, mwaka huu ambapo askari walifanya ufuatiliaji na kukamata maboksi
54.
“Maboksi mengine 17 yalikamatwa mkoani Kilimanjaro, Wilaya
ya Rombo, eneo la Tarakea Januari 17, mwaka huu yakiwa yamefichwa kwenye nyumba
moja kwa ajili ya kuvushwa kwenda Nairobi, Kenya, pia kwenye tukio hilo gari
aina ya Fuso lenye namba T. 611 AKA ambalo lilikodiwa na watuhumiwa Mabula na
Mushi kwa ajili ya kusafirisha mzigo huo kutoka Mabibo, Dar es Salaam kwenda
Rombo-Tarakea lilikamatwa,” alisema.
Alisema hata hivyo upelelezi bado unaendelea na watuhumiwa
pamoja na vielelezo ambavyo ni maboksi ya tumbaku 71, sampuli ya matofali na
magari yaliyotumika kwenye wizi huo vinashikiliwa na jeshi hilo.
Chapisha Maoni