Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


 
NAIBU Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (mwenye suti) ameagiza kusimamishwa kazi mara moja askari watatu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa tuhuma ya wizi wa mafuta ya ndege na mizigo ya abiria.

Amewataja askari hao kuwa ni Halfan Kisana, Mussa Mandauli na Abias Mwanza ambao walipangiwa kuwako katika kituo cha Jeshi hilo huko katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Masauni alitoa agizo hilo jana katika kikao chake na watendaji wa jeshi hilo kilichofanyika katika ukumbi wa VIP alipofanya ziara ya ghafla uwanjani hapo.

“Mmenisomea ripoti yenu lakini nashangaa mmeshindwa kunifafanulia suala la wizi wa mafuta kwamba mmekamata wezi wangapi na kiasi gani cha mafuta yaliyoibiwa lakini ninazo taarifa kuwa baadhi ya askari wakiwamo hao niliowataja wanadaiwa kuhusika katika  wizi huo.

“Nina taarifa kwamba Kisana na mwenzake Mandauli Oktoba 7, mwaka jana, saa mbili asubuhi wakitumia gari la mkuu wa kituo wa kikosi cha zimamoto aina ya Landrover yenye namba ST 2948 walikamatwa katika lango la kuingilia katika kikosi cha Jeshi la Wananchi (603 KJ) wakiwa wamepakia madumu kumi ya lita 20 yakiwa na mafuta ya ndege,” alisema.

Alisema tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi hata hivyo askari hao hawakuchukuliwa hatua zozote badala yake walipandishwa vyeo.

“Hii haiwezekani, nataka askari hawa wasimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike haraka ndani ya siku 14. Maana rubani naye ni binadamu... anakwenda na kuweka mafuta kwenye ndege yake baadae anakuja kuiwasha na kuondoka akijua yapo mafuta ya kutosha, kumbe yameibiwa bila yeye kujua matokeo yake ndege inakwenda kuanguka, hatukubalini na suala hili,  lazima hatua zichukuliwe dhidi yao ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema.

Naibu Waziri huyo aliagiza jeshi hilo pia kuwatafuta wamiliki wenye gari namba T. 225 AWM aina ya Salun GX na gari namba T 786 AWZ ambayo pia yanadaiwa kutumika kubeba mafuta yanayokuwa yameibiwa.

Alifafanua kuwa gari namba T786 AWZ ilikutwa ikiwa imebeba mafuta Januari 8, mwaka huu huku lenye namba  T 225 AWM ilibeba mafuta Januari 13, mwaka huu.

“Na hii yenye namba T 225 AWM nimeiona hapa uwanjani leo (jana) nataka wahusika wote watafutwe, wahojiwe na waeleze yale madumu yaliyokutwa kwenye magari yao walipeleka wapi mafuta na hata ikibainika kuwa wahusika ni askari wenyewe wachukuliwe hatua.

“Kwa sababu hatuwezi kufika pahala tukawa na watu wa usalama ambao nao ni wezi, nasikia kuna baadhi yenu hamtaki kukaguliwa suala hilo nataka likome mara moja vinginevyo hawa wanaokataa kukaguliwa wanaweza kutumiwa na watu kupitisha nyara za serikali zilizoibwa.

“Awali nimewaeleza kwamba mnafanya kazi nzuri ya kulinda usalama lakini hawa wachache watatuchafua nimewataja hadharani ili wajue tunawajua na tutawashughulikia,” alisema.

Alisema askari mwingine Abiasi Mwanza amekuwa akishirikiana na mfanyakazi wa kampuni ya Swispot, Lucas Mwaganda kuiba mizigo ya abiria uwanjani hapo.
“Nina taarifa kwamba Agosti 26, 2014 saa nane usiku, Mwanza na Mwaganda walinaswa na kamera za usalama (CCTV) wakiiba mizigo ya abiria iliyokuwa kule ‘Cargo’. 

Mwaganda aliingia na kuitoa mizigo hiyo kisha aliwasiliana na Mwanza ambaye alifika na pikipiki na kuichukua mizigo na kuondoka nayo,” alisema.

Alisema tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi hata hivyo Askari Mwanza alihamishwa na kupelekwa Makao Makuu ya jeshi hilo ambako alipandishwa cheo na kuwa ‘Inspector’.

“Pamoja na hayo nataka muwasilishe ofisini kwangu ndani ya siku 14 mikakati yenu endelevu ya namna ya kuepukana na aibu hii, na hii ni kwa viwanja vyote vya ndege nchini. 

“Na kule upande wa Idara ya Uhamiaji nimechukua ripoti yao nakwenda kuiangalia kuona kama mapato ya visa tunayopata kama yanaendana na idadi ya wateja wanaoingia nchini... maana tumepata taarifa kwamba kuna vijana wanataka kupata utajiri wa haraka haraka hapa, tutachunguza suala hili,” alisema.

Awali Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Zimamoto JNIA, Martin Otieno alisema wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali uwanjani hapo ikiwamo upungufu wa askari.

“Tumefanikiwa kupunguza uhalifu lakini bado tunakabiliwa na changamoto ya wizi wa mafuta ya ndege na tuna upungufu wa askari 99 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi hapa uwanjani katika maeneo 31 tunayoyasimamia,” alisema

Naibu Waziri huyo, pia alikutana na Maofisa Wakuu wa Jeshi hilo katika kikao chake cha ghafla alichokifanya ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo, Posta jijini Dar es Salaam mapema asubuhi.

“Niliwaagiza kuwa wanatakiwa kuanzisha mara moja kitengo maalumu cha kupokea malalamiko ya wananchi,” alisema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement