Tanzania jana iliungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya malaria duniani. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu aliadhimisha kwa kuwaongoza waandishi wa habari huko mjini Dodoma kupima malaria kwa kutumia kipimo cha haraka (mRDT).
Baada ya shughuli hiyo Waziri Ummy alitoa tamko rasmi ambapo alisema ugonjwa huo bado ni tishio hasa kwa maeneo ya vijijini kuliko mijini licha ya takwimu kuonesha umepungua hadi asilimia 50 toka mwaka 2007/8 hadi 2011/12.
Kiwango cha maambukizi katika maeneo ya vijijini ni asilimia 10.7 na mijini asilimia 3.4.
'Kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya malaria kunatupa sababu ya kujipongeza na kumshukuru kila mdau aliyechangia kwa namna moja au nyingi katika jitihada hizi lakini bado tunatakiwa kupambana na kufikia lengo letu la kupunguza kiwango hicho hadi kufikia asilimia 5," alisema
Takwimu za vituo vya afya zinaonesha
kuwa takribani watu milioni 12 hupata ugonjwa wa malaria kila mwaka hapa nchini
huku makundi yanayoathirika zaidi ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano
(5) na mama wajawazito.
“Ikumbukwe ugonjwa huu wa malaria ni hatari kwa uhai wetu,
maendeleo na ustawi wa Taifa letu, na ndiyo moja ya sababu kubwa inayochangia katika
kupunguza kasi ya maendeleo ya jamii, hii ikiwa ni pamoja na kuleta vifo
na madhara mengine yatokanayo na malaria” iliongeza taarifa hiyo.
Waziri aliwataka wananchi na wadau wote kuona umuhimu na kushiriki
katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya
mikakati ya kuuthibiti ugonjwa huo, na kusema kuwa iwapo mikakati hiyo
itatekelezwa ipasavyo ni dhahiri kuwa maambukizi yataendelea kupungua kwa kiasi
kikubwa na hatimaye kumaliza kabisa tatizo hilo.
Alisema mikakati inayotekelezwa na Wizara kwa kushirikiana
na wadau ni pamoja na Udhibiti wa mbu kwa kutumia njia mbalimbali,
kama vile kutumia vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu; unyunyuziaji wa
viuatilifu ukoko katika kuta ndani ya nyumba, kusafisha mazingira na kuua
viluwiluwi vya mbu kwa kutumia viuadudu vya kibailojia hasa katika maeneo ya
mijini.
Waziri Ummy alisisitiza wananchi kuzingatia kupima ili kujua uwepo
wa vimelea vya malaria kabla ya kutumia dawa, kumaliza kozi ya dawa kulingana
na maelekezo ya mtoa huduma, kutumia vyandarua vyenye viuatilifu kila siku
wakati wa kulala, kuzingatia usafi wa mazingira kuzuia mazalia ya mbu.
Chapisha Maoni