Ulaji wa chakula maarufu ‘chips’ umeelezwa kuwa hatai kwa
wajawazito kwani huchochea kwa asilimia 80 ya mama kujifungua mtoto mwenye
tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi.
Chakula kingine kinachochangia hali hiyo ni ulaji wa
vyakula vya viwandani.
Hayo yalielezwa juzi na Mtaalamu wa Masuala ya Lishe wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Denis Mbinga alipozungumza na matukionamaisha
hospitalini hapo.
Alisema matatizo ya watoto kuzaliwa na vichwa vikubwa,
mgongo wazi na magonjwa mengineyo katika siku za karibuni yameongezeka kutokana
na ulaji wa vyakula visivyofaa hasa vile vya kusindika na kuacha vya asili
vilivyoliwa na wazee wa zamani.
“Kwa kawaida kuna milo mikuu mitatu ambayo tunatakiwa
kuipata asubuhi, mchana na jioni. Mlo kamili ni lazima uzingatie vyakula kutoka
kwenye makundi makuu matano ambayo ni yale ya nafaka, mizizi na ndizi mbivu, vyakula
vyenye asili ya wanyama, mbogamboga, matunda aina zote, mafuta na sukari.
“Katika makundi haya mwili hupata nishati lishe, protini
ambayo hujenga mwili, vitamin na madini ambayo hulinda mwili pamoja na kuupa
mwili joto,” alisema.
Alisema hata hivyo wengi wanashindwa kuzingaia kula mlo
kamili kwa kuzingatia makundi hayo ya vyakula aliyoyataja.
“Katika nchi zilizoendelea watu wanapohitaji kupata watoto
huzingatia suala la lishe miezi mitatu kabla huku kwetu barani Afrika hili ni
tatizo kwani asilimia kubwa ya wanawake hujikuta tayari wakiwa wajawazito bila
ya kujiandaa kuubeba,” alisema.
Naye Elizabeth Lyimo ambaye pia ni mtaalamu wa kitengo
hicho pia aliwashauri wanawake kuwahi mapema kliniki ili kufuatilia mwenendo wa
afya zao na watoto waliowabeba tumboni.
“Hii itasaidia kubaini mapema kama kuna tatizo lakini kama
wakichelewa hatari huwa kubwa zaidi ya kupata watoto wenye matatizo hayo pamoja
na udumavu,” alisema.
Chapisha Maoni