Ni wazi sasa uhamasishaji juu ya kuepuka matumizi ya uvutaji wa
sigara yamefikia pazuri kufuatia ujumbe wa mwaka huu usemao“jiandae kwa pakiti
zisizo na matangazo wala vivutio”
Kufuatia ujumbe huo, jamii imehamasishwa kujiepusha au kujikinga
na vivutio mbalimbali vya matangazo yanayohamasisha matumizi ya sigara ambayo
ina madhara makubwa kiafya.
Rai imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juu ya
Siku ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku Duniani yaliyohadhimishwa leo duniani kote.
“Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inaadhimisha siku
hii, kwa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kutoa
elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na matumizi ya sigara na bidhaa za
tumbaku,” amesema.
Amesema tafiti nyingi zinathibitisha madhara yatokanayo na
matumizi ya tumbaku ni pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kama vile
saratani, magonjwa ya mishipa ya damu na moyo, kiharusi, magonjwa ya njia ya
hewa.
“Tafiti pia zinaonyesha takriban watu 6,000,000 hupoteza maisha
duniani kwa mwaka kwa utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake,” amesema.
Waziri Ummy amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kupinga
matumizi ya tumbaku duniani kwa mwaka 2016, inalenga kuelimisha na kuhamasisha
jamii kuachana na matumizi ya tumbaku na kusisitiza kwa wazalishaji kutokuweka
maandishi au nembo zinazovutia ili kuishawishi jamii kutumia bidhaa hizo.
“Tumbaku imekuwa ikisababisha madhara kiafya kama vile magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza. Magonjwa hayo ni magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, ugonjwa wa kisukari na magonjwa ya njia ya hewa,” amesema.
Siku ya kupinga matumizi ya Tumbaku Duniani huadhimishwa kila
mwaka Mei 31.
Chapisha Maoni