Mmoja wa madaktari wa macho akimpima mwanafunzi wakati wa upimaji huo. |
KLABU ya Rotary ya Oysterbay kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH), Amana na Mnazi
Mmoja wamefanya upimaji afya kwa wanafunzi
1200 wa Shule ya Msingi Msasani A.
Upimaji huo ulifanyika jana shuleni hapo ambapo pia wazazi
wa wanafunzi hao na walimu wa Shule hiyo walipata fursa ya kupima afya zao na
kuchangia damu Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa upimaji huo
Mwenyekiti wa Rotary, Mhandisi Mohamed Verse (mwenye kofia) alisema waliguswa kufadhili
upimaji huo kwani suala la afya ni jambo la msingi kwa mwanadamu.
“Rotary tumekuwa na utaratibu wa kuisaidia jamii. Hii ni
klabu inayoundwa na wafanyabiashara pamoja na wataalamu mbalimbali. Hii si mara
ya kwanza kusidaia shule hii, tayari tumeshajenga maktaba mbili, tumeweka maji
safi na salama, tumepanda miti, tumejenga ukuta ili kuimarisha ulinzi na awamu
hii tumeona ni vyema tufanye upimaji afya,” alisema.
Alisema Rotary wameweza kuendesha upimaji huo wa afya kwa
wanafunzi hao kwa kushirikiana na wenzao wa kampuni ya Diamond Trust.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Egidius Mjumangoma alisema
amefurahishwa na hatua hiyo ya upimaji afya kwani itasaidia kuwatambua na
kuwasaidia mapema wale watakaokutwa na ugonjwa.
“Watanzania hatuna ule utamaduni wa kupima afya zetu, leo
(jana) wanafunzi wangu wamepata fursa ya kupimwa macho, meno, malaria na
maradhi mengineyo, hii itasaidia kuwatambua na kuwasaidia mapema wale
watakaokutwa na tatizo.
“Nawashukuru mno Rotary maana wamekuwa washirika waaminifu
wa vitendo na si maneno pekee, bado tunaomba wadau wengine waige mfano huu na
kutusaidia bado tuna changamoto mbalimbali zinatukabili,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Elimu na Malezi wa Kata ya Bonde la
Mpunga ambako ipo shule hiyo, Faudhia Kigwe alisema ufadhili wa Rotary katika
sekta ya elimu unapaswa kuigwa na kampuni nyinginezo.
Chapisha Maoni