SERIKALI imekusudia kupeleka nchini Marekani sampuli ya damu na haja kubwa zilizochukuliwa kutoka kwa watu walioripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika huko mjini Dodoma.
Sampuli hizo zitapelekwa katika maabara ya Kituo
cha Udhibiti wa Magonjwa cha Marekani (CDC) jijini Atlanta wakati wowote
kuanzia sasa kwa uchunguzi zaidi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na
waandishi wa habari ambapo alisema sampuli hizo zitakapopelekwa nchini humo
wanatarajia kupata majibu yake katika kipindi kisichozidi wiki moja.
Alisema sampuli hizo zilikuwa ziwe zimekwisha
safirishwa jana kwenda nchini humo lakini hadi kufikia mchana bado walikuwa
hajapokea kibali.
“Mipango imekamilika, kibali bado hatujakipokea
tunatarajia hadi kufikia jioni tutakuwa tumekipata na hivyo kuzisafirisha..
tunatarajia kupokea majibu yake katika kipindi kisichozidi wiki moja,” alisema.
Alisema pamoja na kusudio hilo, sampuli nyingine
zikiwemo damu, haja kubwa, vinyama vya ini na chakula tayari zimepelekwa katika
maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali, Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) na Maabara ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu na Maabara ya Hospitali ya
KCMC (KCRI).
Waziri Ummy alisema sampuli hizo zimepelekwa katika
maabara tofauti tofauti ili kujiridhisha kwa majibu yatakayobainika.
Alisema hadi sasa, sampuli za nafaka pekee, zimefanyiwa
uchunguzi katika maabara ya TFDA na
zimeonesha kuwepo kwa uchafuzi wa sumukuvu (Aflatoxin).
“Jumla ya sampuli 13 kati ya 27 (48%) ziligundulika kuwa
na uchafuzi wa sumukuvu kwa kiasi kisichokubalika kwenye nafaka kwa
mujibu wa viwango vya kitaifa na zote zilitokana na mahindi. Kati ya sampuli
hizo zenye sumukuvu, sampuli 12 zilitoka wilaya ya Chemba na sampuli moja ilitoka
wilaya ya Kondoa.
“Sampuli saba kati ya hizo 12 zilikuwa na kiasi kikubwa cha sumukuvu kinachozidi 150 µg/kg (micrograms per kilogram)
kwa total aflatoxins, ambapo wigo wa
aflatoxin B1 katika sampuli hizo ni
kati ya 157.1 – 194.4 µg/kg,” alisema.
Waziri huyo alisema kiasi kama hicho kiliwahi
kuhusishwa na madhara yatokanayo na sumukuvu katika nchi za
India, China na Kenya.
“Dalili za madhara ya sumukuvu zinafanana na dalili za ugonjwa usiofahamika
uliojitokeza katika Wilaya za Chemba na Kondoa. Hivyo upo uwezekano mkubwa kwamba ugonjwa huu
umesababishwa na ulaji wa chakula kilichokuwa na sumukuvu na kuleta madhara,”
alisema.
Alisema katika jitihada za kutambua kiini cha ugonjwa
huo, Wizara imepeleka jopo la wataalam mkoani Dodoma ili waweze kushirikiana na
wenzao walioko huko kufanya uchunguzi wa kina.
“Bado nasisitiza kuwa haya bado ni matokeo ya awali
miongoni mwa uchunguzi unaofanywa katika kubaini kwa uhakika chanzo cha ugonjwa
huu. lakini ni vyema tukaanza kufanyia kazi matokeo haya wakati tukiendelea
kusibiri uchunguzi unaoendelea kufanyika katika maabara nyingine nje ya nchi,”
alisema.
Alisema ugonjwa huo uliliripotiwa na Wizara Juni 19,
mwaka huu katika Wilaya za Chemba na Kondoa, Mkoani Dodoma ambapo kwa wakati
huo kulikuwa na jumla ya wagonjwa 21 na vifo saba.
Alisema kumekuwako
na ongezeko la wagonjwa 11 katika kipindi cha wiki moja ambapo hadi kufikia
Juni 24, mwaka huu idadi ya wagonjwa 32
huku idadi ya vifo ikiwa imebakia saba.
“Tangu ugonjwa huu ujitokeze jumla ya wagonjwa 12 wamepatiwa
huduma ya matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na watatu kati yao wamefariki
dunia. Wagonjwa 18 wametibiwa katika Hospitali ya Kondoa, wanne kati yao
wamefariki. Wagonjwa wawili hawakuwahi kulazwa hospitali.
“Hadi jana (juzi) kulikuwa na jumla ya wagonjwa tisa
ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, na 14 wako katika Hospitali
ya Wilaya ya Kondoa. Wagonjwa watatu waliolazwa Hospitali ya Mkoa Dodoma, na
wawili waliolazwa Kondoa, bado hali zao ni tete,” alisema.
Alisema wizara ya Afya itaendelea kufanya kazi kwa
ukaribu na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Nchi, Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kipindi hiki cha
kutambua na kudhibiti ugonjwa huu.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia
sahihi za uandaaji wa chakula utakaosaidia kupunguza kiasi cha sumukuvu kwenye nafaka
ambazo hazijaharibika sana. Njia hizi ni pamoja na kuchambua nafaka
zilizoharibika (zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi), kukoboa mahindi
kabla ya kusaga au kuacha kutumia nafaka zitakazoonekana kuharibika sana,” alisema.
Alisema Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya
kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni pamoja na
kujenga uwezo wa kupima sumukuvu katika damu na mkojo miongoni mwa taasisi za
ndani ya nchi.
“Tutaendelea kutoa matibabu kwa wanachi
walioathirika na Ugonjwa huu, kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali
ya Wilaya ya Kondoa pamoja na kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama Shirika
la Afya Duniani (WHO) na Shirika la CDC katika kudhibiti ugonjwa huu,” alisema.
Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed
Bakari alisema kemikali ya sumukuvu hutokea pale ambapo vyakula hususan nafaka
zinapokuwa hazijahifadhiwa vizuri.
“Nafaka zisipohifadhiwa vizuri huzalisha fangasi ambayo
hutengeneza sumukuvu, kiwango cha sumukuvu kinapokuwa kikubwa husababisha
madhara na athari kwenye ini, hali inayopelekea mgonjwa kutapika, kuharisha
damu na nyinginezo,” alisema.
Chapisha Maoni