MANISPAA ya Kinondoni imeingia hasara ya Sh bilioni
1.7 kwa kumlipa mkandarasi kujenga barabara ya mabatini ambayo ilianza kujengwa
tangu 2007 na hadi leo bado haijakamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika
barabara hiyo ambako alifanya ziara ya ukaguzi pamoja na kamati ya fedha, Meya
wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (Chadema) alisema kutokana na hali hiyo
Manispaa imewasimamisha kazi wahandisi wake waliosimamia kazi hiyo.
Alisema barabara hiyo ambayo inajengwa chini ya
kampuni ya Del Monte ilipaswa kuwa imekamilika na kutumika lakini haijakamilika
licha ya kuwa Manispaa tayari imekwisha tumia kiasi hicho cha fedha.
“Nilisikia
mkoa umetoa tamko kwamba kampuni hii inapaswa kusimama kufanya kazi tena nchi
nzima, nikashangaa maana tumeambiwa kuwa inapaswa kuongezewa Sh milioni
700 kwa ajili ya kumalizia kazi.
“Nikaona vyema nije eneo la tukio ili nijue ukweli kuhusu
mradi huu, nimebaini kile kilichoelezwa kwenye makaratasi si ukweli halisi,
kwamba kampuni hii haikuhusika kupanga mchoro wa barabara hii, kazi hiyo
ilitathminiwa na wahandisi wa Manispaa na kampuni ilipokea mchoro,” alisema.
Alisema kwa hali hiyo wahandisi wa Manispaa ndio
wanaopaswa kuwajibika kwa makosa yaliyopelekea kubomolewa kwa barabara hiyo na
kuanza kujengwa upya.
“Kwa maana hii inapaswa wakandarasi kuwa makini siasa
zisije zikawaharibia kazi, naona wazi kwamba barabara za Kinondoni zinatumika kwa
watu kutaka kujipatia umaarufu, leo nimeujua ukweli na tuliwatuma vyombo vya
dola kuchunguza hili.
“Sitaki kutumia siasa hapa, ndio maana nikaja
kuwasikiliza mnieleze ukweli, ili tumalize matatizo haya ya fedha kutumika huku
barabara zikiwa hazijajengwa, sitaki kuwaachia mzigo viongozi watakaokuja
baadae,” alisema.
Meya Jacob alisema pamoja na barabara hiyo ipo
nyingine ya Akachube ambayo Manispaa itairudia kwa Sh bilioni 1.2 kwakuwa
haijajengwa katika kiwango kinachotakiwa.
“Kama leo hii kiongozi anaagiza kampuni isimame
kufanya kazi bila kueleza kwa kina sababu ya kufanya hivyo kama hizi mlizoeleza
tuna kila sababu ya kuhisi kwamba pengine anaujua ukweli na anataka kumtorosha
mkandarasi husika,” alisema.
Alisema ameiagiza Del Monte kumalizia kazi hiyo kwani
kwa hali ilivyo inaonesha wazi kosa hilo lilikuwa la wahandisi wa Manispaa
hiyo.
“Uchunguzi unaendelea dhidi yao na atakayekutwa na
hatia atabeba mzigo wake. Hatutaki kuingia tena kwenye deni ambapo hivi sasa
kuna mkandarasi anadai Manispaa Sh bilioni 2.1 kwa kusimamishwa bila barua
maalumu,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Del Monte, George Lupia alisema
walijenga barabara hiyo kwa mchoro na vipimo walivyopewa na wahandisi wa
Manispaa hiyo katika tenda yao.
“Tuliijenga na ikakamilika kabisa... baadae
tuligundua kuwa inacheza, tukachukua udongo na kuupima tukagundua kuwa eneo
hili lina maji mengi, tukaandikia barua Manispaa kuwa tunairudia kwa gharama
zetu wenyewe,” alisema.
Wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda alinukuliwa na vyombo vya habari kuwa ameisimamisha kazi kampuni hiyo
kwa kufanya kazi chini ya kiwango.
Chapisha Maoni