Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


 
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) ipo katika mchakato wa  kuanza kutoa huduma ya ubingwa wa  juu wa kufanya upasuaji wa kupandikiza sikio kwa watoto waliosumbuliwa na tatizo la usikivu.

Akizungumza na MTANZANIA jana hospitalini hapo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema tayari serikali imepeleka madaktari wapatao watano nje ya nchi kwenda kupata mafunzo hayo.

“Tunatarajia kuanza kutoa huduma ya upasuaji wa kupandikiza sikio hapa Muhimbili hivi karibuni, madaktari wetu wapo nje ya nchi wakijifunza namna ya kufanya upasuaji huo,” alisema.

Alisema katika upasuaji huo, madaktari watakuwa wakiweka kifaa maalumu  ndani ya sikio la mtoto mwenye tatizo la usikivu ambacho kitakuwa kinamuwezesha kusikia vizuri.

“Muhimbili tunatarajia mapema wiki ijayo madaktari hao kuwa wamerejea nchini, pindi watakapowasili basi tutaeleza kwa kina jinsi upasuaji huo utakavyokuwa ukifanyika,” alisema.
Aligaesha (pichani ) alisema Muhimbili itaanzisha huduma hiyo ili kuwezesha watoto wenye matatizo hayo kupata huduma kwa wakati.

Katika jarida la hospitali hiyo la Januari hadi April, mwaka huu Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo, Dk. Edwin Liyombo alinukuliwa akisema kuanza kwa upasuaji huo kutasaidia kuokoa fedha nyingi.

“Mgonjwa mmoja akipelekwa nchini India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji huu hugharimu kati ya Sh milioni 85 hadi 100 kwa hiyo matibabu haya iwapo yatafanyika hapa nchini ni wazi kuwa tutaweza kupunguza gharama hizi kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement