Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam
DEREVA wa basi la UDA lenye namba za usajili T. 696 CVB
ambalo liligonga treni juzi na kusababisha kifo cha mtu mmoja papo hapo na
majeruhi zaidi ya 20, Majuto Hamis (PICHANI) amefunguka na kuzungumzia tukio hilo.
Akizungumza na matukionamaisha katika wodi 2B iliyoko kwenye jengo
jipya la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) ambako amelazwa
kwa ajili ya kupata matibabu, alisema ilikuwa ajali mbaya mno.
“Sikutegemea…ilikuwa ni usiku wa saa tatu nilikuwa nimepakia
abiria wangu wapatao 40 tulikuwa tunatoka Kariakoo kunaelekea Mbagala lakini
safari yetu iliishia pale eneo la Kamata na sasa nipo MOI nikiwa nimevunjika
miguu yangu yote miwili.
“Jambo ambalo nakumbuka, katika eneo lile, hakuna kielelezo
chochote kinachomtaarifu dereva kuwa mbele yake kuna reli inakatisha kwenye
barabara hivyo aendeshe kwa uangalifu.
“Sasa mchana huwa ni rahisi kujua kama kuna treni inakatisha maana
kunakuwa na nuru tofauti na usiku kwani huwa kuna giza,” alisema.
Hamis alisema kwa kuwa hakuna alama ya kiashirio kwenye eneo
hilo, alijisahau kibinadamu na kwamba alishtuka tayari ajali imetokea.
“Sikukumbuka kabisa nikawa naendelea na safari ghafla tukawa
tayari tumekutana na treni ile na kupata ajali,” alisema kwa masikitiko.
Alisema hadi sasa hajui iwapo kondakta wake alisalimika
katika ajali hiyo ingawa amesikia wengi walijeruhiwa.
“Naiomba serikali hasa Kikosi cha Usalama Barabara waende
katika eneo lile wakaweke kibao ili ajali nyingine zisiendelee kutokea, tena ingefaa
zaidi katika maeneo ambako reli inakatisha barabara pawe na mageti wakati treni
inakatisha wafunge kwa muda,” alisema.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alisema walimpokea Hamis
na majeruhi wengine baada ya kupatiwa srufaa toka Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH).
“Tuliwapeleka moja kwa moja katika chumba cha dharura na sasa
wanapatiwa matibabu wodini,” alisema.
Naye Ofisa Uhusiano wa MNH Neema Mwangomo alisema hadi
kufikia jana tangu aAjali hiyo itokee walipokea majeruhi 49.
“Majeruhi 19 walitibiwa na kuruhusiwa, 22 walipelekwa MOI
hivyo MNH tumebaki na wanane,” alisema.
Chapisha Maoni