Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TAASISI
ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kufanya tena upasuaji
mkubwa wa kihistoria kwa kuweka betri katika moyo wa mtu mzima ambao unashindwa
kusukuma damu kwenye mishipa ipasavyo.
Akizungumza
na matukionamaisha hospitalini hapo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo
wa JKCI, Peter Kisenge alisema upasuaji huo utakuwa ni wa mara ya kwanza
kufanyika nchini.
“Kweli
tumefanya upasuaji mara nyingi hapa JKCI, lakini hatujawahi kufanya upasuaji
huu wa kuweka betri kwenye moyo wa mtu mzima ambao misuli yake imechoka na
haiwezi tena kufunguka, kusukuma damu kwenye mishipa,” alisema.
Alisema
utendaji kazi wa moyo huo upo chini ya kiwango cha asilimia 20 ndio maana
mgonjwa huyo atamfanyia upasuaji huo ili betri hiyo iweze kumsaidia moyo wake
kufanya kazi sawa sawa.
Jengo la JKCI
“Tutakwenda
kuweka kifaa hicho ambacho kitaalamu kinajulikana kama Pacemaker CRTD kwa
mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 68 ambaye moyo wake umechoka na hivyo
kushindwa kusukuma damu kwenda kwenye mishipa ili isafiri mwilini na yeye aweze
kuishi,” alisema.
Alisema
iwapo mambo yatakwenda kama yalivyopangwa na kwa neema za Mwenyezi Mungu
wanatarajia upasuaji huo kufanyika Agosti 13, mwaka huu.
“JKCI
tutafanya upausaji huo kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa moyo kutoka
nchini Kenya na tuna imani kuwa tutafanikiwa,” alisema.
Hivi
karibuni, Taasisi hiyo iliweza kufanikisha upasuaji mwingine wa kwanza kwa
kuweka betri katika moyo wa mtoto mwenye umri wa miaka sita.
Kwa
mujibu wa madaktari wa JKCI, mtoto huyo, Happiness Josephati (pichani na mama yake) hakuzaliwa na
betri ya asili ambayo Mwenyezi Mungu huiweka katika kila mwili wa mwanadamu
wakati ambapo viungo huumbwa akiwa tumboni mwa mama yake.
Elitruda
Malley ambaye ni mama mzazi wa Happiness aliliambia gazeti hili kuwa awali
alikuwa hawezi kufanya mambo ambayo watoto wa umri wake wanayafanya kwani kila
mara alikuwa akipoteza fahamu.
Mkurugenzi wa jkci, Profesa Mohamed Janabi
Hata
hivyo baada ya kufanyiwa upasuaji huo hivi sasa afya yake imeimarika na wakati
wowote wataruhusiwa kurejea nyumbani kwao Arusha.
Chapisha Maoni