Wizara imepokea taarifa kuwa Kamati
ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Shinyanga imevamia ofisi za shirika la Jhpiego
mkoani humo na kukamata baadhi ya watumishi wake kwa madai ya shirika hilo
kugawa mafuta maalumu yanayodhaniwa kutumiwa kuhamasisha ngono za jinsia moja. Baada
ya taarifa hiyo wizara inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
Si kweli kwamba shirika la Jhpiego
limekuwa likihamasisha ngono baina ya wapenzi wa jinsia moja. Shirika hilo
kupitia mradi wa “Sauti” linasaidia serikali katika jitihada za kupambana na
maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa makundi yaliyopo kwenye hatari kubwa ya
maambukizi.
Moja ya makundi yanayolengwa ni
wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao. Shirika limekua likitoa elimu ya
mabadiliko ya tabia kwa wanaume hao huku likiwapatia mafuta hayo kama sehemu ya
kuwasaidia kupunguza hatari ya maambukizi.
Mafuta hayo yaliingizwa nchini kwa
kufuata taratibu za kisheria kwa ufadhili wa Mfuko Maalumu wa Rais wa Marekani
wa kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI (PEPFAR).
Ndugu wanahabari, kama mtakumbuka
hivi karibuni Wizara kupitia kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu ilisitisha ugawaji wa mafuta hayo maalumu
(vilainishi) miongoni mwa makundi hayo maalumu.
Kufuatia agizo hilo, Wizara
iliagiza Shirika hilo kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha katika ofisi za
PEPFAR zilizopo Ubalozi wa Marekani ili yapelekwe katika nchi nyingine
zinazofadhiliwa na PEPFAR ambazo matumizi ya mafuta hayo hayajazuiwa.
Ndugu wanahabari, Shirika hilo lilitekeleza
agizo la wizara la kukusanya mafuta hayo na kuyaweka katika ofisi zao za kanda,
tayari kuyasafirisha kuja jijini Dar es Salaam, ambapo umeandaliwa utaratibu
maalumu wa kuyapeleka katika nchi nyingine bila kuyaharibu.
Mnamo tarehe 27 mwezi July, mwaka
2016 Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Shinyanga ilivamia Ofisi za Shirika
hilo na kuchukua mafuta hayo bila kuelewa utaratibu uliotolewa na Wizara wa
kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha katika ofisi za PEPFAR.
Zoezi hilo la kamati ya Ulinzi na
Usalama halikushirikisha wizara ya Afya wala wadau wa sekta ya Afya wilayani
humo, ambao wanaelewa vizuri utaratibu uliowekwa na wizara kukusanya mafuta
hayo na kuyarudisha mahali husika bila kuyaharibu.
Ndugu wanahabari, tayari Wizara
imeshamuandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga kutaka mafuta hayo
yaliyochukuliwa kurudishwa katika ofisi za mradi wa Sauti zilizopo mtaa wa
Mwasele, kata ya Kambarage mkoani Shinyanga ili zoezi la kuyakusanya na
kuyarudisha Dar es Salaam liweze kuendelea.
Mwisho, Wizara inapenda kuwajulisha
kuwa shirika la Jhpiego ni miongoni mwa wadau wakuu wa Serikali ambao wamekuwa
wakisaidia huduma mbalimbali za Afya nchini ikiwemo kusaidia ujenzi wa vituo
vya afya, kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kuboresha Afya ya mama
na mtoto na Uzazi wa Mpango kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Hivyo serikali
imeridhia shirika hilo kuendelea kutoa huduma mbalimbali za afya bila kutumia
mafuta hayo.
Imetolewa na:
Michael O. John
Kaimu Katibu Mkuu,
Chapisha Maoni