Binadamu pekee aliye hai, ambaye
inatambuliwa kwamba alizaliwa katika karne ya kumi na tisa, leo
anasherehekea sikukuu yake ya 117 tangu kuzaliwa kwake.
Emma Morano, alizaliwa katika jimbo la Piedmont karibu na mji wa Milan, Italia tarehe 29 Novemba, 1899.
Wakati
huo, kampuni ya magari ya Fiat ilikuwa tu ndiyo imeanzishwa. Klabu ya
soka ya Milan nayo ilikuwa imeanzishwa wiki chache awali.
Ameshuhudia wafalme watatu wa Italia wakitawazwa na kuondoka, alizaliwa wakati wa utawala wa Mfalme Umberto wa Kwanza.
Aidha, katika maisha yake, kumekuwepo na Baba Watakatifu kumi na mmoja.
Isitoshe, alishuhudia Vita Vikuu vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.
Mwaka huu, alitambuliwa kuwa mwanamke mkongwe zaidi aliye hai baada ya kifo cha Mmarekani Susannah Mushatt Jones mwezi Mei.
Ndiye pia binadamu pekee aliye hai ambaye alizaliwa miaka 1800.
Bi Morano anasema sana amekuwa na maisha marefu kutokana na jeni.
Mamake aliishi hadi miaka 91. Dadake wengi pia walifariki wakiwa na umri mkubwa.
Anasema
kwa kiwango fulani, lishe yake imechangia. Anasema amekuwa akila mayai
matatu - mawili yakiwa mabichi, kila siku kwa zaidi ya miaka 90.
Alianza
hayo alipokuwa mwanamke kijana, baada ya madaktari kugundua alikuwa na
ugonjwa wa anaemia, ambapo mgonjwa hupungukiwa na seli nyekundu za damu
au haemoglobini, muda mfupi baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.
Siku hizi amepunguza na hula mayai mawili pekee, na biskuti kadha.
Hilo
linaenda kinyume kabisa na ushauri wa sasa wa madaktari kuhusu jinsi ya
kuishi maisha marefu na yenye afya, daktari wake wa miaka 27 Carlo Bava
ameambia AFP.
"Emma hula mboga chache sana, na hali matunda sana.
Nilipokutana naye alikuwa anakla mayai matatu kila siku, mawili mabichi
kila asubuhi na moja la kupikwa mchana saa sita na kisha anakula kuku
chakula cha jioni."
Licha ya haya, Carla anasema, mwanamke huyo anaonekana kuwa na "maisha tele".
Jambo jingine ambalo Bi Morano anasema huenda limechangia maisha yake
marefu, ni hatua yake ya kumfukuza mumewe mwaka 1938 baada ya mtoto
wake wa kiume kufariki akiwa na miezi sita pekee.
Ndoa yao ilikuwa inaendelea vyema kwa mujibu wa Bi Morano.
Alikuwa amempenda mvulana aliyeuawa wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na hakutaka kumuoa mtu mwingine.
Lakini aliambia gazeti la La Stampa, alipokuwa na miaka 112, kwamba hakuna na namna nyingine ya kufanya ila kuoa mtu mwingine
"Aliniambia: 'Ukiwa na bahati utanioa, la sivyo nitakuua'. Nilikuwa na miaka 26. Niliolewa."
Baadaye, ndoa yao ilianza kuvurugika na akamfukuza mumewe ingawa hawakuvunja ndoa yao hadi mwaka 1978 mumewe alipofariki.
Bi Morano alifanya kazi hadi alipotimu miaka 75 na aliamua kutooa tena.
"Sitaki kudhibitiwa na yeyote," aliambia gazeti la New York Times.
Ili kusherehekea siku hii muhimu, wakazi wa eneo la Pallanza karibu
na Ziwa Maggiore, ambapo amekuwa akiishi, wanaandaa maonyesho ya mitindo
yakiangazia karne tatu katika historia.
Profesa wa masuala ya
msambojeni George Church ambaye hufanya kazi katika chuo cha matibabu
cha Harvard pamoja na kundi lake la watafiti ambao wamekuwa wakifanya
utafiti kuhusu umri wa kuishi, ameambia BBC kwamba binadamu wataendelea
kuongeza muda wa kuishi.
"Nafikiri tutashuhudia ongezeko kubwa la
muda wa kuishi katika miaka michache iliyopita kutokana na teknolojia,
na pia utafiti unaofanyiwa watu wa kipekee kama vile Emma."
Hata hivyo, hajaondoka nyumba yake ya vyumba viwili kwa miaka 20.
Carlo anahisi shinikizo kuhusu majukumu ya kumtunza mwanamke huyo mkongwe, ambapo anasema ni kama kuutunza Mnara wa Pisa.
"Ile siku utaanguka, kuna mtu atalaumiwa," aliambia AFP. "Emma atakapofariki, mimi ndiye nitakayewajibishwa."
Mtu
aliyeishi muda mrefu zaidi duniani kwa mujibu wa Guinness alikuwa
Mfaransa Jeanne Calment, aliyeishi miaka 122 na siku 164. Alifariki
Agosti 1997.
Chapisha Maoni