NA MWANDISHI MAALUMU, PWANI
KLABU ya Rotary ya
Oyster Bay pamoja na madaktari na wafanyakazi wa kujitolea wametoa huduma za
matibabu kwa wakazi wa Kerege wilayani Bagamoyo. Kambi hiyo ya matibabu
imeeefanyika Jumapili tarehe 27 Novemba katika shule ya Msingi ya Kerege.
Vipimo na matibabu
vilitolewa bure kwa magonjwa kama vile malaria, upungufu wa damu, kisukari na
shinikizo la damu, masikio, pua na koo (ENT), magonjwa ya ngozi, macho pamoja
na meno.
Huduma nyingine zilizotolewa zilikuwa pamoja na ugawaji wa miwani
zilizotolewa kwa watu waliokutwa na matatizo ya macho.
Huduma za ushauri
kwa wajawazito na vifaa vya kujifungulia vilitolewa bure kwa wajawazito; huduma
za ushauri nasaha na upimaji wa UKIMWI pia zilitolewa. Kwa mara ya kwanza,
elimu ya usafi na taulo za wanawake zilitolewa kwa wasichana.
Akizungumza katika
kambi hiyo, Alfred Woiso, Rais wa Klabu ya Rotary ya OysterBay alisema, “Ni
furaha yetu kuwa hapa kwa mara nyingine tena na tunafurahi kuona wakazi wa
Kerege wamejitokeza kuja kupata huduma hizi. Tumetoa huduma kwa watu waliokuwa
na matatizo mbalimbali.
Tumeona wagonjwa wengi wenye magonjwa sugu kama
kisukari na shinikizo la damu. Inaonekana kuna haja ya kupanua wigo wa huduma
zetu kwa vile kuna mahitaji ya huduma za matibabu ya magonjwa mengine.”
Kambi hiyo ya
matibabu ilihudhuriwa na wagonjwa wapatao 800 kutoka Kerege na maeneo ya
jirani. Kambi hii inayoandaliwa na Klabu ya Rotary ya Oyster Bay imefanyika
Kerege kwa mara ya sita sasa kwa lengo la kuwasaidia wakazi wa Kerege kupata
huduma za matibabu, wakazi ambao kwa kawaida hawana uwezo wa kumudu gharama za
matibabu.
Kambi hiyo ya
matibabu imedhaminiwa na Diamond Trust Bank na kuandaliwa kwa ushirikiano na
Shree Hindu Mandal Hospital, Vital Supplies, Whitedent, vClick Concepts Inc,
MAK Books and Brains, ABACUS Pharmaceuticals, Fazel Foundation na wanachama wa
Klabu ya Rotary na Rotaractor.
Chapisha Maoni